“In short, you must remember this—that if you hold anything dear outside of your own reasoned choice, you will have destroyed your capacity for choice.”
—EPICTETUS, DISCOURSES, 4.4.23

Ni jambo la kushukuru sana kwa mimi na wewe kuweza kuiona siku hii nyingine mpya ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA,
Mwongozo wetu ni AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA,
Msimamo wetu ni KAZI, UPENDO NA HUDUMA.
Kwa kusimamia maeneo hayo matatu, siku ya leo itakuwa bora sana kwetu.

Asubuhi ya leo tutafakari ADUI MKUU WA FURAHA…
Adui mkuu wa furaha ni kujishikiza na vitu, kuweka mategemeo na matumaini yetu kwenye vitu ambavyo vipo nje ya uwezo wetu.
Kujenga utu wetu kwenye vitu ambavyo tunaweza kuvipoteza muda wowote ule.
Kutaka kile tulichonacho tuendelee kuwa nacho muda wote.

Hili ni tatizo kwa sababu kila kitu kinabadilika, hakuna chochote kinachobaki kama kilivyo sasa.
Hivyo kama umejenga utu wako kwa vitu vya nje, vinapobadilika vinakuumiza na hilo linakukosesha furaha.
Unapojishika na kazi yako au biashara yako au mali zako, pale unapopoteza vitu hivyo inatikisa utu wako wote.
Utajiona hufai tena kwa sababu kile ulichokuwa unajitambulisha nacho hakipo tena.

Kuondokana na hali hii usijishike na chochote, usijiambia bila ya kitu fulani maisha yako hayawezi kwenda.
Na chochote cha nje unachotumia sasa, kitumie wakati unacho na jua wakati wowote unaweza kukipoteza.
Inapotokea umekipoteza, na hilo litatokea, hutashtuka wala kuumia kwa sababu ulishajua hilo litatokea na kuwa tayari kwa ajili ya hilo.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kutokujishikiza au kujitambulisha na kitu chochote kilicho nje ya udhibiti wako, bali kutumia kila kitu kwa wakati ambao bado unacho.
#UsijishikizeNaVilivyiNjeYaUdhibitiWako #KilaKituKinaMwishoWake #KuwaTayariKupoteza

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1