“As for me, I would choose being sick over living in luxury, for being sick only harms the body, whereas luxury destroys both the body and the soul, causing weakness and incapacity in the body, and lack of control and cowardice in the soul. What’s more, luxury breeds injustice because it also breeds greediness.”
—MUSONIUS RUFUS, LECTURES, 20.95.14–17

Kitendo cha kuiona siku hii nyingine mpya ya leo, ni kiashiria kwamba kazi yetu hapa duniani bado haijaisha.
Tumepewa tena zawadi ya siku hii ya leo, ili twende tukaikamilishe kazi hiyo.
Hivyo tusipoteze muda kwa yale yasiyo muhimu.
Leo twende tukaishi msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA, mwongozo wetu wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA, na msimamo wetu wa KAZI, UPENDO NA HUDUMA.
Kwa kusimamia maeneo hayo matatu, siku ya leo itakuwa bora sana kwetu.

Asubuhi ya leo tutafakari UGONJWA AU ANASA?
Ukiambiwa uchague ugonjwa au anasa, utachagua nini?
Wengi tutakimbilia kuchagua anasa, kwa sababu ugonjwa unaumiza, anasa ni raha.
Tutajibu hivyo kwa sababu tunaangalia juu juu na kuona matokeo ya muda mfupi na siyo ya muda mrefu.
Unapoangalia kwa kina na kuangalia matokeo ya muda mrefu, utagundua anasa ina madhara kuliko mgonjwa.

Kama mstoa Musonius anavyotuambia, ugonjwa unaathiri mwili pekee, lakini anasa inaathiri mwili na roho.
Ugonjwa utasumbua mwili wako tu, na utaweza kuutibu au kuuvumilia kama hautibiki.
Lakini anasa, inaharibu mwili, inaharibu roho yako, inavuruga mahusiano yako na kutikisa imani yako.
Anasa inajenga tamaa ambayo haishibi na hivyo kukufanya kuwa mtumwa wa anasa zaidi.

Tunapaswa kuwa na tahadhari kubwa sana tunapojikuta kwenye hali au mazingira yanayotupa anasa.
Kwa sababu ni vigumu sana kuyaona madhara yake wakati yanakuathiri, utakuja kuona baadaye madhara yakiwa yameshakuwa makubwa.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuulinda mwili wako na roho yako dhidi ya anasa ambazo zinakuzunguka kwenye maeneo mbalimbali ya maisha yako.
#AnasaNiSumu #JilindeDhidiYaAnasa #KuwaNaKiasi

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1