Watu wanaweza wasikuambie, lakini tayari wameshakuweka kwenye viwango vyao wenyewe kupitia kile unachokifanya.

Iwe ni kazi au biashara, wale wanaohusika na wewe moja kwa moja wameshakuweka kwenye viwango na kupitia matokeo unayotoa, mtu anaweza kujua kabisa ni wewe umefanya kitu hata kama haupo.

Hivyo kuwa makini sana na kila unachofanya, kuwa makini na matokeo unayoyatoa, kwa sababu watu wanakuhukumu na kukupanga kwa matokeo unayozalisha.

Kwa kuangalia matokeo yanayopatikana, mtu anajua kabisa fulani ndiyo kafanya hivi, hata kama hakukuona wakati unafanya.

Swali la kujiuliza leo, ni je unaacha sifa gani kupitia matokeo unayozalisha.

Watu wakiona kazi yako wanasemaje, wakati wewe haupo?

Changamoto kubwa kwetu sisi binadamu ni kwamba sisi wenyewe ndiyo huwa tunakuwa wa mwisho kujua ukweli kuhusu sisi. Kila mtu anaweza kuwa anajua kitu kuhusu sisi, lakini hakuna anayetuambia.

Ili usiruhusu hilo likukwamishe, jilazimishe kuujua ukweli ambao wengine wanao kukuhusu wewe. Chunguza watu wanaonaje matokeo yako na omba watu wakupe mrejesho halisi na wa ukweli kwa kuwahakikishia hautakuumiza, hata kama ni mrejesho mbaya.

Lengo lako wewe ni kuwa bora, lengo lako ni kutoa matokeo mazuri, hivyo anayekuambia ukweli kwamba matokeo unayotoa sasa siyo mazuri ni mtu mzuri kwako, anakuonesha wapi pa kuboresha zaidi.

Unapofanya kitu, unapaswa kutoa matokeo bora kabisa unayoweza kutoa ili kujijengea sifa kwamba kazi yako ni bora na matokeo ni mazuri.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha