“Anything that can be prevented, taken away, or coerced is not a person’s own—but those things that can’t be blocked are their own.”
—EPICTETUS, DISCOURSES, 3.24.3

Ni siku nyingine mpya, siku nzuri na ya kipekee sana kwetu.
Tumeipata nafasi nyingine bora sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA,
Mwongozo wetu ni AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA,
Msimamo wetu ni KAZI, UPENDO NA HUDUMA.
Kwa kusimamia maeneo hayo matatu, siku ya leo itakuwa bora sana kwetu.

Asubuhi ya leo tutafakari SIYO MALI YAKO…
Una jirani yako ambaye amepata safari ya kikazi ya muda mrefu.
Ana gari yake na akakuomba akuachie kwa kipindi atakapokuwa safarini.
Na akakuambia unaweza kuwa unaitumia kwa shughuli zako mbalimbali ili isiharibike kwa kukaa tu bila kutumika.
Unatumia gari hiyo kila siku mpaka kila mtu anajua ni yako.
Je wewe utajiambia hiyo ni gari yako?
Jibu ni hapana, huwezi kujiambia hivyo kwa sababu unajua muda wowote mmiliki wake atarudi na kuichukua gari hiyo.

Cha kushangaza ni kwamba, karibu kila kitu ulichonacho kwenye maisha yako kinaendana na mfano huo wa gari.
Japo unajiambia ni mali yako, kwa hakika siyo, umeazimwa tu kwa muda.
Kitu chochote ulichonacho, ambacho unaweza kukipoteza muda wowote bali hiyo siyo mali yako.
Mali ulizonazo unaweza kuzipoteza, unaweza kuibiwa na hata kutaifishwa na serikali, siyo mali zako, bali umepewa uzitumie kwa muda.
Hata afya yako siyo mali yako, kuna mengi yaliyo nje ya uwezo wako ambayo yanaweza kuathiri sana afya yako.

Kwa kujua haya, ina maana hakuna haja ya kujisumbua kupata mali?
Jibu ni hapana, hatujui haya ili kukata tamaa, bali tunayajua ili kuweza kutumia vizuri kila tulichonacho, tukijua ya kwamba hakitadumu milele.
Na kitu pekee ambacho kipo kwenye umiliki wetu moja kwa moja ni fikra zetu, hizi tunaweza kuziongoza tutakavyo.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kujua vingi unavyojiambia ni mali zako siyo, hivyo uweze kuvitumia vizuri wakati bado vipo kwako.
#TumiaVizuriUlichonacho #UnachowezaKupotezaSiyoChako #FikraNdiyoMaliYako

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.t.me/somavitabutanzania