Kusubiri mpaka uwe umekamilika ndiyo adui wa mafanikio ya wengi.

Watu wengi wamekuwa wanasubiri sana, wazianze kitu mpaka pale wanapokuwa wamekamilika, wanapokuwa na kila kitu wanachotaka.

Kwa bahati mbaya sana, hakuna wakati wowote kwenye maisha yako ambao utakuwa umekamilika na kuwa na kila unachotaka.

Hivyo basi, kama unataka kutoka hapo ulipo sasa, kama unataka kupiga hatua zaidi kwenye maisha yako, basi weka kipaumbele kwenye kuanza.

Anza sasa boresha baadaye ndiyo unapaswa kuwa msimamo wako.

Ukianza kabla hujawa tayari una nafasi ya kuboresha zaidi kadiri unavyokwenda. Lakini kusubiri mpaka uwe tayari kwa kila kitu huwezi kuanza.

Hebu jiulize ni kitu gani ambacho umekuwa unasubiri kuanza kwa sababu unajiona bado hujawa tayari, kisha angalia ni wapi unapoweza kuanzia sasa na kuendelea kuboresha kadiri unavyokwenda.

Kipaumbele chako ni kuanza, na ukishaanza wewe angalia ni wapi unaweza kuboresha zaidi. Kwa kupiga hatua hizo ndogo ndogo utaweza kufikia mafanikio makubwa sana.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha