Kikwazo cha kwanza kwa mtu kuwa na maisha bora ni furaha.

Tumedanganywa sana kwamba kuna njia fulani ya kuwa na furaha ya kudumu kwenye maisha yetu.

Tumeambiwa ukishapata hiki na kile, ukishafika kiwango fulani cha elimu au cheo fulani, basi utakuwa na furaha. Tukaweka nguvu, tukasahau maeneo mengine ya maisha yetu na kufanyia kazi kitu kile kimoja ambacho tuliamini tukikipata au kukifikia tutakuwa na furaha ya kudumu.

Cha kushangaza tunapofikia kitu hicho, tunapata furaha ya muda mfupi tu, halafu tunarudi kwenye hali ya kawaida, tunaanza kuona kuna hatua zaidi za kupiga.

happiness is a problem.jpg

UKWELI KUHUSU FURAHA.

Unachopaswa kujua ni kwamba kwenye haya maisha hakuna furaha ya kudumu. Kama tulivyojifunza hapo juu, maisha ni mateso, kila mtu kuna kitu anateseka nacho.

Na Mark anatuambia, kile ambacho mtu anacho, ndiyo kinachomtesa. Tajiri anateseka na utajiri wake, masikini anateseka na umasikini wake. Wenye familia wanateseka kwa sababu ya familia zao, wasiokuwa na familia wanateseka kwa sababu hawana familia.

Kwa kifupi hakuna namna unaweza kuyakimbia mateso ya dunia, kwa sababu chochote ulichonacho, hicho ndiyo kitakachokutesa.

Ni asili yetu sisi binadamu kutokuridhika na kile ambacho tayari tumekipata, na hii imekuwa na manufaa kwetu kama binadamu kwa ujumla. Kwa sababu imetusukuma kuwa bora zaidi na kupiga hatua.

Hebu fikiria kama watu wangeridhika na usafiri wa farasi, leo tusingekuwa na magari. Kila tunachoteseka kukipata, tukishakipata tunakiona ni cha kawaida na kuona kingine bora zaidi tunachoweza kufikia.

Furaha ni tatizo kwenye jamii zetu kwa sababu tumekuwa tunadanganywa kuna namna ya kuifikia furaha ya kudumu, kitu ambacho hakiwezekani, kwa sababu ni kinyume kabisa na asili yetu sisi binadamu.

Tunaambiwa tukishafika sehemu fulani basi furaha ni yetu, na katika kuhangaika huko kuitafuta furaha, ndiyo tunaipoteza.

NJIA PEKEE YA KUPATA FURAHA.

Mark anatuambia, furaha inapatikana katika kutatua matatizo tuliyonayo, na siyo tukishatatua matatizo. Sijui kama umeelewa vizuri hapo, yaani unapata furaha wakati wa kutatua matatizo yako, zile hatua unazochukua ndiyo zinakufanya ujisikie vizuri. Lakini ukishatatua tatizo hilo, hupati tena furaha, kwani unaona tatizo kubwa zaidi, unapoanza kulitatua tena ndiyo unapata furaha.

Hivyo basi, kama unataka kuwa na maisha bora na yenye furaha, kila wakati kuwa na tatizo ambalo unalitatua. Yafanye maisha yako kuwa mwendelezo wa kutatua matatizo na kupiga hatua zaidi, na hapo utakuwa na maisha bora, maana hiyo ndiyo asili yetu binadamu.

Na ukiangalia hilo ni kweli kabisa, angalia kwenye jamii zetu, huenda wewe au mtu mwingine unayemjua, alianzia chini kabisa, akawa anafanya kazi sana, anajituma sana na maisha yake yalikuwa tulivu. Akafanikiwa na kufika utajiri wa juu, halafu ghafla anaanza kuwa na maisha ya hovyo, anaanza kufanya mambo ambayo huko nyuma hakuwa anafanya na mwishowe anapoteza kila alichopata. Kinachokuwa kimetokea kwa watu kama hawa ni wanakuwa wameanza na tatizo la kutatua, wakiamini wakishalitatua basi maisha yao yatakuwa na furaha ya kudumu. Wanatatua tatizo hilo, halafu wanabaki bila ya tatizo jingine la kutatua, na hapo ndipo wanaanza kutafuta matatizo yanayowapoteza zaidi.

AKILI YAKO INAPENDA MATATIZO.

Akili zetu binadamu huwa haziwezi kukaa bila ya tatizo la kuhofia, ndiyo maana licha ya kuwa tunaishi kwenye zama ambazo hali ya maisha ni bora, bado watu wana hofu kubwa sana na vitu visivyokuwa na uhalisia. Kama hakuna tatizo unalolifanyia kazi, akili yako itatengeneza matatizo ya kukufanya uhofie.

Hivyo hatua ya pili ya kuwa na maisha bora ni kutatua matatizo, kuwa na maisha yenye furaha, tafuta matatizo unayofurahia kuyatatua na yatatue. Unapotatua tatizo moja, tafuta jingine na uendelee kutatua.

Hii ni sehemu ya uchambuzi wa kitabu The Subtle Art of Not Giving a F*ck kilichoandikwa na Mark Manson. Kupata uchambuzi kamili wa kitabu hiki ambacho kinatupa mafunzo ya njia mbadala ya kuwa na maisha bora ambayo ni kinyume na hamasa chanya tunazopata kila siku, karibu ujiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA. Kujiunga na channel hii fungua; www.t.me/somavitabutanzania