No person hands out their money to passersby, but to how many do each of us hand out our lives! We’re tight-fisted with property and money, yet think too little of wasting time, the one thing about which we should all be the toughest misers.”
—SENECA, ON THE BREVITY OF LIFE, 3.1–2
Kuiona siku hii nyingine mpya na nzuri sana kwetu ni nafasi ya kipekee sana.
Siyo kwa akili zetu wala nguvu zetu tumeweza kuiona siku hii.
Hivyo tunapaswa kushukuru kwa nafasi hii, na njia bora ya kushukuru ni kutumia vizuri muda wetu.
Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA,
Mwongozo wetu ni AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA,
Msimamo wetu ni KAZI, UPENDO NA HUDUMA.
Kwa kusimamia maeneo hayo matatu, siku ya leo itakuwa bora sana kwetu.
Asubuhi ya leo tutafakari KUWA BAHILI WA MUDA WAKO…
Mtu akija kwako na kukuambia hebu nipe elfu 10 hapo, lazima kwanza utamuuliza ni kwa ajili ya nini. Tunathamini sana fedha zetu na hivyo huwa hatuzigawi hovyo.
Mtu akiingia kwenye shamba lako na kujimilikisha kama lake, ugomvi mkubwa utaibuka, hutakubali mtu achukue mali yako kirahisi hivyo. Tunalinda sana mali zetu zisichukuliwe na yeyote.
Lakini kuna kitu kimoja chenye thamani kubwa mno kwetu, ambacho hatukithamini ma kukilinda kama tunavyofanya kwenye fedha na mali zetu.
Kitu hicho ni muda.
Mtu yeyote anaweza kuchukua muda wetu kama anavyotaka na wala tusiulize kwa nini anafanya hivyo.
Umekaa unafanya kazi yako, mara inaingia simu au ujumbe, unaacha kazi na kuanza kujibu. Bila hata ya kujiuliza kama ni muhimu kweli.
Tunaruhusu watu wajimilikishe maisha yetu watakavyo, bila ya kuweka ulinzi mkali kama ambao tumeuweka kwenye mali zetu.
Unaruhusu watu waingilie maisha yako kama wanavyotaka wao wenyewe, na hilo linakuzuia wewe kupiga hatua.
Rafiki, kitu cha kwanza unachopaswa kukithamini sana na kuwa na ubahili nacho ni muda wako. Usikubali mtu yeyote achukue muda wako au kuingilia maisha yako kwa urahisi.
Kwa sababu muda pekee ndiyo rasilimali yenye thamani kubwa, ambayo umepewa kwa uchache na ukishaipoteza huwezi kuipata tena.
Fedha unaweza kuzipata, mali pia, lakini poteza sekunde moja na imetoka hiyo, huwezi kuipata tena.
Uwe na siku bora sana ya leo, siku ya kuwa bahili wa muda wako kwa kuuthamini na kuulinda kuliko unavyolinda fedha na mali zako, kwa sababu muda wako ni zaidi ya vitu hivyo.
#MudaNiZaidiYaMali #KuwaBahiliWaMudaWako #KupotezaMudaNiKupotezaMaisha
Wako rafiki katika safari ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.t.me/somavitabutanzania