Lengo kuu la kila binadamu ni kuwa huru, kuchagua maisha anayoyataka na kufanya kile anachotaka. Lakini uhuru kamili ni vigumu sana kufikiwa na mtu mmoja mmoja.

Ukiangalia historia ya dunia na sisi binadamu kwa ujumla, hilo linaonekana wazi. Kwamba hitaji letu la kutaka kupata uhuru, mara zote limekuwa linatuingiza kwenye utumwa zaidi kuliko kutupatia uhuru.

Kwa kuangalia dunia kwa ujumla na watu kwa pamoja, uhuru unaonekana kuwepo, lakini kwa kuangalia mtu mmoja mmoja, uhuru ni mgumu sana kufikiwa. Kwani kila hatua ambayo tunapiga kama binadamu, inatufanya kuwa watumwa zaidi.

Mwandishi na mwanahistoria Yuval Noah Harari kwenye kitabu chake kinachoitwa SAPIENS; A Brief History Of Humankind ametushirikisha historia fupi ya maisha yetu binadamu hapa duniani, kwa kutumia sayansi za asili (natural sciences) na bailojia ya mageuzi (evolutionary biology).

sapiens.jpg

Kwenye kitabu hiki ambacho kimeeleza historia yetu kwa kina, Yuval ameonesha mapinduzi makubwa matatu ambayo tumepitia na hatua mbalimbali kwenye mapinduzi hayo. Kwa kuangalia unaweza kuona mapinduzi hayo yalileta uhuru kwa watu, lakini yalifanya maisha ya wengi kuwa mabovu zaidi, huku wachache pekee ndiyo wakifurahia uhuru uliopatikana.

Kwenye makala hii nakwenda kukushirikisha mapinduzi hayo na hatua mbalimbali ambazo binadamu tumepitia na jinsi ambavyo zimetufanya kuwa watumwa zaidi kuliko kutufanya kuwa huru.

Moja; Mapinduzi ya fikra.

Mapinduzi ya fikra ndiyo hatua ya kwanza katika historia ambayo iliweza kututofautisha sisi binadamu na viumbe wengine, hasa walio kwenye kundi la wanyama. Sayansi ya mageuzi inatuambia kwamba huko nyuma hatukuwa na tofauti kubwa na wanyama wengine, lakini kutokana na kubadilika kwa mazingira, ndipo binadamu pia tulibadilika.

Kufikiri ndiyo kitu ambacho kimeweza kututofautisha sisi na viumbe hai wengine. Kibaiolojia, hakuna tofauti kubwa kati yetu binadamu na sokwe mtu, kinachotufanya sisi kuwa juu yao ni uwezo wetu wa kufikiri na kupanga mambo.

Wanyama wengine wanaendeshwa kwa hisia na mpango ambao tayari upo kwenye akili zao tangu wanazaliwa. Lakini sisi binadamu tunaweza kufikiri na kuyabadili mazingira yetu.

Tungefikiri uwezo wetu wa kufikiri ungetufanya kuwa huru kuliko wanyama wengine, lakini pia umetuletea kitu kimoja kinachotunyima uhuru, kitu hicho ni hofu.

Ni sisi binadamu pekee ambao tunaweza kukaa na kuhofia kitu ambacho hakipo, tunaweza kutengeneza mawazo ya kitu kisichokuwepo kabisa na kikatupa hofu kubwa.

Pia uwezo wetu wa kufikiri ulitufanya sisi binadamu kuwa dhaifu kimwili kuliko wanyama wengine. Kila mnyama ana nguvu fulani, iwe ni kwenye misuli, meno, macho, masikio na kadhalika. Lakini sisi binadamu tumepoteza nguvu hizo na kubaki na nguvu ya kufikiri.

Uwezo wa kufikiri umetufanya kuwa juu ya wanyama wengine, lakini haujatupa uhuru, maana tumekuwa tunatumia fikra zetu kutengeneza vitu visivyokuwepo na hivyo kuwa na hofu. Lakini pia sisi binadamu ndiyo viumbe pekee ambao tunajua kwamba kuna siku tutakufa, na hili limekuwa linapokelewa kwa namna tofauti baina ya watu, na limekuwa linafanya watu wasiwe huru kwenye maisha yao.

opening mind - conceptual vector illustration of cage in head wi
opening mind – conceptual vector illustration of cage in head with brain inside and hand opening it with key

Mbili; Mapinduzi ya kilimo.

Baada ya mapinduzi ya fikra, binadamu alikuwa akiishi kwa kuwinda na kuokoteza. Hakuwa na makazi maalumu na chakula chake kilitegemea upatikanaji wa wanyama, mizizi au matunda. Hali hii ilifanya ukuaji wa binadamu kuwa mdogo kwa sababu chakula hakikuwa cha uhakika.

Hivyo yakaja mapinduzi ya kilimo, ambapo sasa binadamu badala ya kurandaranda akikusanya, alikaa chini na kulima mazao pamoja na kufuga mifugo. Hii inaweza kuonekana ni hatua ambayo ilileta uhuru kwa binadamu, kwa kuhakikisha chakula kinapatikana na maisha kuwa mazuri.

Lakini huo siyo ukweli, mapinduzi ya kilimo yalimfanya binadamu kuwa mtumwa wa mazao na mifugo yake kuliko kuwa huru. Kwenye mapinduzi ya kilimo, binadamu alipoteza uhuru kwa njia zifuatazo;

 1. Kukaa eneo moja kwa ajili ya kulima mazao na kuhudumia mifugo, hivyo ule uhuru wa kuzunguka kuokoteza ulikosekana.
 2. Virutubisho kutokupatikana kwa usahihi. Wakati wa kuokoteza, binadamu alikuwa akila vyakula mbalimbali hivyo kupata virutubisho mbalimbali. Lakini ujio wa kilimo, ulimfanya binadamu kutegemea virutubisho vichache, mfano mazao mengi yanayolimwa mpaka sasa ni wanga, hivyo virutubisho vingine vilikuwa havipatikani vizuri.
 3. Kufanya kazi masaa mengi zaidi. Wakati wa kuokoteza, inakadiriwa binadamu alifanya kazi masaa mawili mpaka manne kwa siku na kupata chakula cha kutosha na hivyo kuwa na muda wa kupumzika na kukaa na wenzake. Mapinduzi ya kilimo yalikuja na mazao ambayo yalihitaji muda kulima, kupalizi na hata kuvuna. Hiyo ilipelekea binadamu kufanya kazi masaa 8 mpaka 10 kwa siku.
 4. Familia kubwa. Kutokana na upatikanaji wa wingi wa chakula kwenye mapinduzi ya kilimo, idadi ya watu iliongezeka kwa kasi. Familia ziliweza kuwa na watoto wengi, lakini watoto hao walikufa kwa wingi utotoni. Hii ilitokana na wazazi kukosa muda wa kukaa na watoto kwa wingi wa kazi za kilimo, lakini pia virutubisho havikuwa vizuri.

Mapinduzi ya kilimo yakiangaliwa kwa ujumla yake, yalifanya jamii ya binadamu kuanza kukaa eneo moja na kustaarabika, lakini yaliwafanya binadamu kukosa uhuru zaidi kuliko walipokuwa wakiokoteza.

Tatu; Ujio wa Himaya.

Mapinduzi ya kilimo yaliwafanya binadamu kukaa eneo moja, na hivyo kuanza kutengeneza jamii. Lakini kitu kimoja kilitokea, watu wanapokuwa eneo moja, kunatokea misuguano fulani baina ya watu, hasa pale rasilimali zinapokuwa za uhaba. Na kadiri idadi ya watu inavyokuwa kubwa, ndivyo misuguano inakuwa mikubwa na watu kushindwa kuelewana.

Ukuaji huu wa jamii, ulileta kitu kipya kwenye historia ya binadamu, ambacho ni himaya au falme. Himaya hizi ziliwakusanya watu pamoja na kuwepo kwa kiongozi mmoja ambaye alisimamia sheria na taratibu ili maisha ya watu yaweze kwenda vizuri.

Kama ilivyo kwa hatua nyingine, ni rahisi kuona hatua hii iliwapa watu uhuru, badala ya kuwa na misuguano ambayo hakuna wa kufanya maamuzi, uwepo wa himaya ulitatua hilo.

Lakini kama ilivyo kwa hatua nyingine, ujio wa himaya ulifanya maisha ya mtu mmoja mmoja kuwa mabovu kuliko kipindi cha nyuma. Na hizi ni njia ambazo watu walikosa uhuru zaidi kwa kuwa kwenye himaya kuliko walivyokuwa bila himaya.

 1. Ushuru. Ili kuendesha himaya hizi, watu walitakiwa kutoa ushuru ambao uliwawezesha viongozi kuendesha himaya hizo. Hivyo sehemu kubwa ya mazao ya wakulima yalikwenda kulipa ushuru, bila hata ya ridhaa yao.
 2. Vita. Himaya nyingi zilianza kupata tamaa ya kukua zaidi kwa kupindua himaya zinazozizunguka. Na hapo ndipo vita zilipoanza, ambazo ziligharimu maisha ya watu na kufanya ushuru kuwa juu zaidi.
 3. Ukoloni. Himaya ndiyo zilileta ukoloni kwa watu, baadhi ya himaya ziliamini zina nguvu na mamlaka ya kutawala watu wengine na hilo lilipelekea jamii nyingi kulazimishwa kuwa chini ya himaya fulani bila ya ridhaa yao.

Pamoja na kwamba himaya zote zilikuja kuanguka na kuzaa mataifa, lakini ujio wake uliyafanya maisha ya wengi kuwa mabovu kuliko kuwepo kwa himaya hizo.

Nne; Ujio wa Fedha.

Ili kuendesha himaya vizuri, kulihitajika njia bora ya watu kubadilishana thamani. Hapo nyuma watu walikuwa wakibadilishana mali kwa mali. Kama wewe ni mfugaji wa mbuzi na unataka mahindi, basi ulienda sokoni na mbuzi ukitegemea kubadilishana na mkulima wa mahindi. Hili lilileta changamoto moja kubwa, kwamba wewe unaweza kuwa na mbuzi na unataka mahindi, lakini mwenye mahindi hataki mbuzi, anataka samaki. Hivyo kubadilishana kulikua kugumu. Na hata himaya kukusanya ushuru ilikuwa tatizo.

Hapa ndipo fedha ilipogunduliwa, kama njia ya kubadilishana thamani. Ujio wa fedha ulionekana kurahisisha maisha, kwa sababu sasa ukiwa na mbuzi, unamuuza na kupata fedha, halafu unatumia fedha hiyo kununua mahindi.

Lakini ujio wa fedha haujatuacha salama, fedha imekuwa kama mungu ambaye kila mtu anamsujudu, fedha imeleta mafarakano makubwa baina ya jamii. Fedha pia ziliwasukuma watu kufanya kazi zaidi ili kuzipata, na kisha kuzipoteza kwa mambo yasiyo muhimu.

Tano; Ujio wa Dini.

Kabla ya himaya, watu walikuwa wakiishi kwenye jamii ndogo ndogo, na kila jamii ilikuwa na miungu wake kwa mahitaji mbalimbali. Hivyo watu walikuwa wakiamini kwenye miungu mbalimbali (polytheism), mungu wa mvua, mungu wa afya, mungu wa watoto na kadhalika.

Baada ya himaya kuanza kuibuka, ziliibuka pamoja na kitu kimoja ambacho kilizisaidia sana himaya. Kitu hicho ni dini, na siyo tu dini, bali dini ya mungu mmoja (monotheism).

Kwa kuwa watu tayari walikuwa na miungu wengi, ilihitajika nguvu kubwa sana kuondoa miungu hiyo na kuanzisha dini za mungu mmoja. Na hapa ndipo vita kubwa saba za kidini zilipoibuka, vita ambazo zimesababisha mauaji kwa watu wengi sana mpaka sasa.

Dini kuu ambazo zimetumia mabavu kusambaa ni Ukristo kupitia utawala wa Roma na Uislamu kupitia utawala wa Kiarabu.

Kama zilivyo hatua nyingine, ujio wa dini ulionekana kuleta uhuru kwa watu, kwa kuwa wataamini kwenye kitu kimoja na kuwa wamoja. Lakini dini zimeleta mgawanyiko mkubwa sana baina ya watu na kusababisha vita na machafuko ambayo yanaendelea mpaka sasa.

Sita; Mapinduzi ya sayansi.

Mapinduzi ya kilimo yalikaa na binadamu kwa muda mrefu, lakini zana zilizokuwa zinatumika kwenye kilimo zilikuwa zana duni sana. Hivyo kazi ilikuwa kubwa kwa watu na maendeleo yalikuwa ni madogo.

Kabla ya mapinduzi ya sayansi, Himaya na Dini ndiyo zilikuwa na maamuzi ya mwisho, ukweli ulikuwa ni kile kilichoandikwa kwenye vitabu vya dini au wanachosema watawala. Hakukuwa na tafiti za kutafuta ukweli zaidi, na hivyo binadamu hatukupiga hatua kubwa.

Ni baada mwamko wa karne ya 14 ndiyo watu walipata uhuru wa kufikiri na kuhoji nje ya himaya na dini. Na hapa ndipo mapinduzi ya sayansi yalipozaliwa. Mapinduzi ya sayansi yalijengwa kwenye msingi mmoja; kuna vitu vingi hatuvijui, na njia pekee ya kujua ni kujifunza na kufanya tafiti.

Haina shaka kwamba mapinduzi ya sayansi yamefanya maisha kuwa bora sana, kwa sababu ndipo madawa yalipopatikana na kuokoa maisha ya wengi, mashine mbalimbali kuanzishwa na kuchochea mapinduzi ya viwanda na hata njia za usafiri tunazofurahia sasa.

Lakini mapinduzi ya sayansi hayajatupa uhuru kamili, kwa sababu kama ambavyo dunia ilijifunza tarehe 16 julai 1945 ambapo bomu la kwanza la atomiki lilirushwa nchini Japani, mapinduzi ya sayansi yamekuja na hatari ya uwezo wa kufuta kabisa kizazi cha binadamu hapa duniani. Mapinduzi haya yametuwezesha kuzalisha silaha ambazo zinaweza kuua kila kiumbe kilichopo duniani. Silaha za nyuklia kwa sasa ni tishio. Na kipindi cha vita baridi kati ya Urusi na Marekani, watu waliishi kwa hofu kwa zaidi ya miaka 30 licha ya maendeleo makubwa yaliyokuwa yakiendelea. Hata sasa hofu bado ni kubwa juu ya mapinduzi makubwa yaliyofanyika kwenye sayansi, hasa kwenye silaha za kivita na hata ugunduzi wa silaha za kibaiolojia, kama virusi na nyinginezo.

Saba; Mapinduzi ya viwanda.

Mapinduzi ya sayansi na mapinduzi ya viwanda yanakwenda pamoja. Mapinduzi ya viwanda yamekuja baada ya mapinduzi ya sayansi, kwa kuwa sayansi ilikuja na njia bora na rahisi za kufanya mambo.

Mashine mbalimbali za kuzalisha vitu ziligunduliwa na hivyo uzalishaji kuwa rahisi na hivyo bidhaa kupatikana kwa wingi na kwa bei rahisi. Pia viwanda vilionekana ni njia ya kuongeza ajira kwa watu na hivyo kuwa na manufaa.

Lakini kama ilivyo kwa hatua nyingine, mapinduzi ya viwanda yamekuwa na madhara makubwa kwa binadamu kama yalivyokuwa mapinduzi ya kilimo. Na haya ni baadhi ya madhara hayo.

 1. Kazi nyingi kwa malipo kidogo. Mapinduzi ya viwanda yalizalisha kazi kwa watu, lakini watu walifanya kazi kwa muda mrefu huku malipo yakiwa madogo. Hili lilifanya maisha ha wafanyakazi kuwa magumu na hata kuwachosha haraka.
 2. Bidhaa nyingi zisizo na ubora. Mapinduzi ya viwanda yalikuwa na msimamo wa kuzalisha bidhaa nyingi kwa gharama rahisi ili kuuza kwa watu wengi. Bidhaa hizo hazikuwa na ubora na hivyo kuwafanya watu kununua tena na tena.
 3. Matumizi makubwa ya rasilimali za asili. Kutokana na uzalishaji kuwa mkubwa, rasilimali za asili kama miti, madini na nyingine zilitumika kwa wingi na hivyo kuleta hatari ya kuisha kwa rasilimali hizo.
 4. Uchafuzi wa mazingira. Viwanda vilizalisha taka ambazo hazikuwa rafiki kwa mazingira na hivyo kuleta madhara kwa watu na viumbe wengine.
 5. Kutengeneza walaji (consumerism). Kwa kuwa viwanda vinazalisha bidhaa nyingi ambazo zinapaswa kuuzwa kwa watu wengi, visingeweza kujiendesha kama watu siyo wanunuaji. Hivyo ziligunduliwa mbinu za kuwafanya watu wawe walaji wa bidhaa hizo. Moja ya mbinu hizo ni masoko, ambayo yanagusa hisia za watu na kuwafanya wajione hawajakamilika kama hawana kitu fulani. Leo hii kila mtu ana vitu vingi kuliko anavyohitaji, na siyo kwa sababu ni muhimu kwake, ila utamaduni huu wa ulaji umemsukuma kuvinunua.

Mapinduzi ya viwanda yamekuwa na madhara mengi sana kwa watu, na kuwanyima uhuru kuliko ilivyokuwa awali.

Nane; Mapinduzi ya teknolojia.

Kwa sasa tunaishi kwenye mapinduzi ya teknolojia, mtandao wa intaneti umebadili kabisa kila kitu hapa duniani. Mtu aliyekufa mwaka 1980 akifufuka leo anaweza kufikiri tunaishi mbinguni. Kwa sababu asingeweza kuamini kwamba unaweza kutuma ujumbe kwa mtu aliyepo bara jingine, akaupata na kuujibu hapo hapo. Kwamba unaweza kuongea na mtu aliyepo bara jingine, huku mkionana ana kwa ana, ni maajabu. Lakini ndiyo zama tunazoishi, mtandao wa intaneti umebadili kila kitu.

Na hivyo tunapaswa kuwa na uhuru mkubwa, kwa sababu teknolojia inatusaidia karibu kila kitu sasa. Lakini huo siyo uhalisia, maendeleo haya ya teknolojia yametufanya kuwa watumwa kuliko awali.

Tuchukue mfano wa mawasiliano, kipindi cha nyuma, kama ulitaka kuwasiliana na mtu aliyepo mbali, ulipaswa kuandika barua, ambayo ilichukua miezi kumfikia mtu huyo, na ili upate majibu ulisubiri miezi. Hivyo hakukuwa na mtu aliyekuwa anasukumwa kujibu kila kitu kwa wakati. Njoo leo, kwenye hiyo simu unayotembea nayo, unaingia ujumbe mfupi au mtu anapiga simu, utaacha kufanya kila unachofanya, hata kama ni muhimu, kuangalia simu au ujumbe ulioingia, ukifikiri ni muhimu zaidi.

Simu zetu zenye uwezo mkubwa zimetufanya kuwa watumwa. Mitandao ya kijamii ndiyo imeongeza zaidi utumwa huu. Sasa kila mtu amenasa kwenye simu yake. Hata watu wa karibu wanapokutana, ule ukaribu haupo tena, kila mtu yupo karibu zaidi na simu yake kuliko yule aliyekaa naye.

Utegemezi wa teknolojia pia umetufanya tuache kufikiri na kutumia akili zetu vizuri. Kwa sasa huna haja ya kufikiria kitu chochote, wewe ingia tu kwenye mtandao wa google na tafuta, utapata chochote unachotaka. Hili limetufanya tuwe tunawategemea wengine kwenye kufanya maamuzi badala ya kufikiri sisi wenyewe.

Tunajifunza nini kwenye hatua hizi na tunapaswa kufanya nini?

Somo kubwa la kuondoka nalo hapa ni kwamba kila hatua tunayopiga kama binadamu, huwa ina manufaa kwa jamii nzima ya binadamu, lakini ina madhara makubwa kwa mtu mmoja mmoja.

Hivyo ni wajibu wa kila mmoja wetu kuyajua madhara hayo na kujua namna gani ya kuyazuia yasiharibu maisha yake.

Kwa hatua za nyuma hatuna cha kufanya, lakini tunajifunza.

Kwa hatua tunazoishi sasa, mfano mapinduzi ya viwanda na teknolojia yanayoendelea, tunapaswa kujua vipaumbele sahihi kwenye maisha yetu. Kutokukubali kupelekeshwa na yale yanayotokea na badala yake kuyatumia vizuri kutufikisha kule tunakotaka.

Mwandishi Yuval kwenye kitabu chake anasema kitu kikubwa tunachopaswa kufanya sisi kama binadamu ni kujijua sisi wenyewe kwanza (know thyself) na ukishajijua, basi tumia vile vinavyokuzunguka kuwa bora. Lakini kama hutajijua wewe mwenyewe, utaendelea kutumiwa na wengine na hata vitu vingine kwa manufaa yao na siyo yako.

Na hili lina ukweli, angalia kampuni kama facebook, ina watumiaji zaidi ya watu bilioni mbili duniani, ina thamani ya zaidi ya dola bilioni 500, (kwa shilingi a kitanzania ni zaidi ya zilioni moja, yaani trilioni zaidi ya elfu moja) na mwanzilishi wake ana utajiri wa zaidi ya dola billioni 60 (sawa na tsh bilioni 130). Lakini ukiangalia kampuni hiyo, ni moja ya kampuni ambazo zinawageuza watu kuwa waraibu wa huduma zao na kuuza taarifa zao kwa wanaotangaza biashara. Bila ya kujijua wewe mwenyewe na kujua huduma kama hizo hazifai, utaendelea kutumika kuwatajirisha wengine, huku wewe ukiendelea kuwa mtumwa na maisha yako kuwa hovyo.

Kupata uchambuzi kamili wa kitabu hiki cha SAPIENS; A Brief History Of Humankind, karibu ujiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA. Kwenye kitabu hiki utajifunza historia fupi ya binadamu, tulikotoka, tulipo sasa na kule tunakokwenda. Utajifunza kwamba kumekuwa na aina mbalimbali za binadamu kabla yetu sisi. Utajifunza jinsi madaraja mbalimbali ya kibaguzi yalivyojengwa kwenye jamii zetu. Na utajifunza jinsi ya kuyafanya maisha yako kuwa bora zaidi. Kujiunga na channel hii ya SOMA VITABU TANZANIA, fungua hapa; https://www.t.me/somavitabutanzania

Rafiki, kama ungependa kuendelea kupokea makala na mafunzo mengine mazuri kwenye email yako, fungua hapa na ujaze fomu; www.bit.ly/amkaemail

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.

Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania