Watu wengi hawafurahii kazi au biashara wanazofanya kwa sababu hawafanyi kwa ajili yao. Wanafanya kwa ajili ya watu wengine au kwa ajili ya kupata kitu fulani.
Sasa kwa kufanya hivyo, unaweza kuwaridhisha wengine na unaweza kupata unachotaka, lakini utulivu wa ndani hutaweza kuupata.
Sababu sahihi ya kufanya chochote unachofanya ni kwa kuwa ndiyo kitu sahihi kwako kufanya. Kwamba ungefanya, hata kama hakuna anayekuona au anayekupa kile unachotaka.
Ni kweli unahitaji fedha na hivyo unachofanya lazima kikuingizie kipato, lakini hiyo isiwe ndiyo sababu pekee. Fanya kile kilicho sahihi kwako kufanya.
Na katika kufanya huko, zingatia mambo haya matatu;
Moja ni kuweka kazi, jitume, jisukume kuweka kazi ili uweze kutoa mchango kamili kupitia kile unachofanya. Usikubali kufanya kwa uvivu.
Mbili ni uaminifu, lazima uwe mwaminifu sana kwenye kile unachofanya, usidanganye wala kulaghai, fanya kilicho sahihi na timiza ulichoahidi.
Tatu ni kuwasaidia wengine, chochote unachofanya, jiulize kina mchango gani kwa wengine, kinawasaidiaje kutoka pale walipokwama sasa. Kwa kuwaangalia wengine, utasukumwa kufanya kile kilicho sahihi.
Kwa kujifunza haya rafiki, hupaswi kujikuta tena njia panda ukijiuliza ufanye nini. Kwa sababu unajua unachopaswa kufanya, kazi yako, na kuweka juhudi, uaminifu na kuwasaidia wengine.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,