Hadithi za watu wote ambao waliwahi kufanikiwa sana lakini baadaye wakaanguka huwa zinaeleza maisha ya watu hao wakati walipokuwa kwenye kilele cha mafanikio.

Kilele cha mafanikio ndiyo sehemu hatari kuliko zote katika safari ya mafanikio. Kwa sababu ndiyo sehemu ambayo mtu anaanza kuporomoka na kuanguka.

Ni kanuni ya asili kwamba kitu chochote kinachofika kwenye kilele kinaanza kushuka au kuanguka. Na hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye safari ya mafanikio, unapofika kwenye kilele, kinachofuata ni kuanguka.

Hivyo moja ya njia za kuhakikisha unaendelea kuwa na mafanikio maisha yako yote, ni kuepuka kufika kwenye kilele cha mafanikio. Kila unapofikiri kwamba umefika kwenye kilele, jikumbushe kwamba hapo ndiyo unaanza kuanguka na hivyo fikiria upo chini kabisa.

Njia bora ya kuepuka kufika kwenye kilele cha mafanikio ni kuwa tayari kujifunza kila siku. Na ili uweze kujifunza kila siku, lazima uwe tayari kukubali kwamba hujui.

Watu wengi huanza kuanguka pale wanapofikiri kwamba tayari wanajua kila kitu. Hapo ndipo wanaacha kujifunza, wanapata kiburi na dharau na hizo ndiyo zinawaangusha.

Wewe kuwa mnyenyekevu, jua kuna mambo mengi huyajui na haijalishi umefika juu kiasi gani, bado una nafasi ya kwenda juu zaidi.

Pia kila siku kazana sana kuepuka mazoea. Kila siku jisukume kufanya kitu kipya na siyo kurudia kile ambacho umefanya jana.

Kilele cha mafanikio ni sehemu hatari sana kwako kuwepo, kila unapoanza kupata fikra kwamba umefika kwenye kilele, pambana nazo haraka na jifunze na jaribu vitu vipya.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha