Watu wengi wamekuwa wanakazana sana kufanikiwa kwenye maisha, lakini wakishafanikiwa wanakutana na utupu fulani ndani yao, ambao unawafanya washindwe kufurahia maisha yao.

Hii inatokana na watu kuanza na mpango wa kazi au biashara kabla ya kuwa na mpango wa maisha.

Mtu anaambiwa kazi fulani inalipa sana, au biashara fulani ina faida kubwa. Anakazana kuhakikisha anaingia kwenye kazi au biashara hiyo, anakuwa na mpango bora kwenye kazi au biashara hiyo, anajituma sana na kweli anapata mafanikio makubwa.

Lakini inapokuja kwenye maisha binafsi, mafanikio hayo yanakosa maana kwa sababu kila anachofanya hakiendani na maisha yake, hivyo mtu anajikuta kwenye mtego fulani, amefanikiwa lakini hayafurahii mafanikio hayo, hayampi uhuru ambao alifikiri angeupata.

Kuondokana na hali hii, unapaswa kuanza na mpango wa maisha kabla ya kuweka mpango wa kazi au biashara. Yaani jua kwanza ni maisha ya aina gani unayotaka kuyaishi, weka mpango wako kwa maisha hayo, kisha chagua kazi au biashara ambayo itaendana na mpango wako wa maisha.

Kwa kufanya hivi, utachagua kazi au biashara inayoendana na aina ya maisha unayotaka kuwa nayo na mafanikio yoyote utakayoyapata utayafurahia sana.

Anza na mpango wa maisha kisha weka mpango wako wa kazi au biashara uendane na mpango huo wa maisha. Hii ndiyo njia pekee ya kuwa na maisha bora utakayofurahia mafanikio unayoyapata.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha