Kabla haijawa rahisi huwa ni ngumu.

Sasa hivi unaweza kutembea bila ya tatizo lolote, ni rahisi kwako, lakini ulipokuwa mtoto na unajifunza kutembea, kutembea hakukuwa rahisi kwako.

Sasa hivi ni rahisi kwako kuongea na watu kupitia lugha unayotumia, lakini wakati unajifunza haikuwa rahisi kwako.

Hivyo ndivyo ilivyo kwenye kazi, biashara na mengine mengi, haikuwa rahisi wakati unaanza, lakini kadiri ulivyoendelea, ndivyo ilivyokuwa rahisi.

Usisahau hili kwenye chochote unachokwenda kuanza kwenye maisha yako, jua unapoanza itakuwa vigumu kwako, lakini hilo lisikukatishe tamaa, kwa sababu baadaye itakuwa rahisi kwako.

Unapoanza biashara jua mwanzo utakuwa mgumu, kuna vitu vingi utakuwa huelewi, lakini kadiri unavyokwenda unaelewa na hatimaye inakuwa rahisi kwako.

Usikatishwe tamaa na kitu chochote kile, angalia wengine wanavyokifanya kwa urahisi na jua siyo kwamba wao wana akili sana kuliko wewe, bali wao wamefanya kwa muda mrefu kuliko wewe. Hivyo jipe muda na wewe utaweza kufanya kama wao.

Chochote unachoanza, jua hakitakuwa rahisi na hivyo jiwekee msimamo wa kuendelea kufanya na kutokukata tamaa na kuishia njiani.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha