Habari rafiki?

Jana nilikushirikisha makala fupi ya mambo 20 ya kufanya  kila siku ili mwaka wako 2020 uwe bora sana.

Mambo hayo 20 niliyaweka kwa orodha bila ya maelezo mengi, lengo likiwa mtu upate kile cha kwenda kufanyia kazi mara moja.

Mambo mengi yameeleweka na wengi, lakini kuna machache ambayo wengi wameonesha kutokuelewa na wengine hata kupinga kwamba hayawezekani.

Hivyo kwenye makala hii ya leo nakwenda kutoa ufafanuzi kwenye mambo manne ambayo wengi hawajayaelewa au wameyapinga.

elimu fedha 2

Karibu sana ujifunze na kwenda kuchukua hatua ili maisha yako yaweze kuwa bora sana, hasa kwa mwaka 2020.

  1. Punguza sana au acha kabisa kutumia mitandao ya kijamii kama haikuingizii kipato.

Mitandao ya kijamii imekuwa chanzo cha wengi kupoteza muda mwingi wa maisha yao. Pia imekuwa chanzo cha wengi kupata msongo na sonona kutokana na kufuatilia maisha ya wengine na kujilinganisha nao, kitu ambacho siyo sahihi kwa sababu wengi huigiza kwenye mitandao hiyo.

Hivyo ili kuepuka kupoteza muda na utulivu wako, na ili kupata amani ya moyo na kuepukana na msongo na sonona, acha kabisa kutumia mitandao ya kijamii. Jaribu hili kwa mwaka 2020, ile mitandao ambayo inachukua muda wako mwingi na kila ukiingia unatoka ukiwa unawaonea wengine wivu kwa mambo mazuri yanayoendelea kwenye maisha yao, acha kuitumia mara moja.

Ukiacha kutumia mitandao hii utajikuta ukiwa na muda mwingi wa kufanya kazi zako, kujifunza kupitia kusoma vitabu na hata muda wa kukaa na wale watu wa karibu na muhimu kwako.

Tumia mitandao hii ya kijamii kama tu inakuingizia kipato, kama unafanya biashara na unatangaza kupitia mitandao hii na inakuletea wateja, basi endelea kutumia kwa madhumuni ya biashara. Tofauti na hapo achana nayo.

Mitandao ya kijamii inaingiza fedha kupitia wewe, wewe ndiyo bidhaa inayouzwa na mitandao hii kwa wale wanaotangaza biashara zao. Hivyo kama na wewe huingizi fedha kupitia mitandao hii, achana nayo, usikubali kuuzwa kwa wengine.

Wapo wanaosema kama siyo mitandao ya kijamii hawawezi kukutana na maarifa mazuri kama haya. Hilo siyo kweli, maarifa mazuri yanapatikana pale unapoyatafuta, na mitandao ya kijamii siyo sehemu nzuri kwako kujifunza.

Hivyo acha kutumia mitandao ya kijamii 2020, labda kwa lengo la kibiashara pekee.

  1. Usianze siku yako kwa kufuatilia habari.

Habari nyingi ni hasi au zenye kuibua hisia kwa wafuatiliaji wake. Fungulia chombo chochote cha habari au tembelea mtandao wowote unaotoa habari na utaona habari gani zinapewa kipaumbele. Ni habari za kutisha au kusisimua. Habari za mauaji, ajali, mapigano, wizi, utekaji, ukatili na nyingine kama hizo.

Unapoianza siku yako kwa habari za aina hii, unavuruga kabisa akili yako. Unajikuta umepata hasira au kukata tamaa na kuona dunia haina maana. Hata mambo ambayo ulipanga kuyafanya hutaweza kuyafanya kwa hamasa kubwa pale ambapo umeshakutana na habari za kutisha au kukatisha tamaa.

Ndiyo maana nakushauri usianze siku yako kwa habari, sijakuambia usifuatilie kabisa habari (japo hilo ni jema ukiliweza), ila usianze nazo kwenye siku yako. Anza siku yako kwa kusali/kutahajudi, kusoma vitabu, kupangilia siku yako na kisha kuanza majukumu muhimu kwako kikazi au kibiashara. Mwisho wa siku wakati umeshakamilisha yale muhimu, hapo sasa unaweza kupitia habari ili ujue nini kinaendelea.

Ukifanya hivi utajikuta unakuwa na siku tulivu, siku ambayo umeweka umakini wako kwenye yale muhimu kwako kufanya na siyo kuvurugwa na habari za mambo yanayoendelea, ambayo hayakuhusu moja kwa moja.

Wapo wanaosema ni muhimu kuanza na habari kwa sababu kunaweza kuwa na kitu muhimu unapaswa kujua kabla siku haijaanza, labda kuna daraja limeharibika hivyo usipoanzana habari hutajua. Nasema hiyo siyo sababu yenye mashiko ya kuruhusu siku yako ichafuliwe na habari nyingi hasi. Na nikuambie kitu kimoja rafiki yangu, kama kuna habari muhimu kweli, itakufikia hata kama hufuatilii habari. Tukienda na mfano huo wa daraja kuharibika, hivi unafikiri unahitaji chombo cha habari kujua hilo? Kila mtu atakuwa anazungumzia hilo na hivyo utajua tu.

Kadhalika kwa habari nyingine ambazo ni muhimu, wale wanaokuzunguka watakuwa wanazizungumzia, hivyo kama ni kitu chenye umuhimu utakijua tu.

Usikubali kuharibu siku yako kwa kuanza na habari, anza siku yako kwa mipango yako na kisha imalize kwa habari.

  1. Usitoe ushauri kwa mtu ambaye hajakuomba, usichukue ushauri kwa ambaye hujamwomba.

Ushauri ni kitu ambacho unapaswa kuwa nacho makini sana wakati wa kutoa na hata kutokea.

Tuanze na kutoa, kamwe usitoe ushauri kwa mtu ambaye hajakuomba umshauri, unaweza kuona unamsaidia mtu huyo, lakini utakuwa unapoteza muda wako bure. Watu huwa hawafanyii kazi ushauri ambao hawajautafuta wenyewe. Unaweza kumwona mtu yupo kwenye hali fulani na kufikiri ushauri wako utamsaidia, ukamshauri vizuri na ukashangaa hafanyii kazi yale uliyomshauri. Hii ni kwa sababu mtu huyo hajawa na maumivu ya kutosha kumsukuma kutaka kutoka pale alipo sasa na ushauri wako ni kelele tu kwake. Mtu anayekuja kwako na kukuomba ushauri, ni mtu ambaye ameshaumia vya kutosha na anataka njia ya kuondoka kwenye maumivu, huyu ukimshauri anazingatia. Hivyo kama mtu hajakuomba ushauri, usijisumbue kutoa ushauri wako.

Tukienda kwenye kupokea ushauri, usichukue ushauri wa mtu ambaye hujamwomba akushauri. Hii ni kwa sababu mtu anaweza kuona jambo fulani kwa nje na akajumuisha kwamba tatizo lako ni hili na hatua za kuchukua ni hizi. Lakini mtu huyo anakuwa hajajua kwa undani unapitia nini hivyo ushauri huo unakuwa siyo sahihi. Kama unataka ushauri, mtafute mtu ambaye unamwamini, mweleze kile unachopitia bila ya kuficha chochote, kisha yeye awe na taarifa sahihi na kukushauri kwa usahihi. Lakini siyo ule ushauri wa juu juu ambao watu wanatoa kwa kuona mambo ya nje bila kujua yale ya ndani.

Huwa nasema ushauri wa bure utaona gharama yake pale unapoanza kuufanyia kazi. Huwa siyo ushauri sahihi. Hivyo chukua ushauri kwa watu ambao ni sahihi, watu wenye uzoefu au ujuzi na ambao wanaielewa hali yako. Na siyo kuchukua ushauri kwa kila anayekuambia ungefanya hivi au ungefanya vile. Kadhalika usikimbilie kutoa ushauri kwa mtu ambaye hajakuomba, kwa sababu unakuwa hujaelewa kwa undani anapitia nini na utakachomshauri hatofanyia kazi.

Wapo wanaosema mbona mimi natoa ushauri kupitia makala hizi wakati sijaombwa. Ukweli ni kwamba mimi sijakuletea maarifa haya nyumbani kwako, au kukulazimisha usome, bali wewe umeyatafuta au kukutana nayo na kuona yanakufaa, hivyo ukasoma. Kuna wengi wanakutana na maarifa haya, lakini wanayapita, kwa sababu hayana maana au umuhimu kwao. Lakini wewe umeyapokea, kwa sababu kuna kitu unatafuta na hivyo unayathamini. Hivyo wajibu wangu ni kushirikisha maarifa sahihi ambayo mtu akiyatumia anaweza kupiga hatua kwenye maisha yake, lakini siwezi kumlazimisha mtu asome au kuchukua hatua.

  1. Usijisumbue kuwabadilisha watu, watu huwa hawabadilishwi.

Watu huwa hawapendi kubadilishwa, na wakigundua mtu anataka kuwabadilisha basi wanaleta upinzani mkubwa kuhakikisha hilo halitokei.

Watu huwa wanaweza kubadilika kama watachagua kubadilika wao wenyewe, lakini siyo kulazimishwa kubadilika, hivyo ndivyo saikolojia ya binadamu ilivyo.

Hivyo usijisumbue kumbadili mtu yeyote yule, hutaweza, utaishia kuibua tu migogoro isiyo na manufaa.

Kama unataka mtu mwenye sifa fulani, mtafute mtu mwenye sifa hizo na siyo kumchukua yeyote na kujiambia utambadilisha, unajidanganya.

Kwenye mahusiano, iwe ni ya mapenzi au ndoa, chagua mtu ambaye sifa alizonazo sasa unaweza kwenda nazo na siyo kujiambia utambadilisha.

Kwenye ushirikiano wa biashara au kazi, chagua kushirikiana na mtu ambaye sifa unazoziona sasa kwake unaweza kwenda nazo.

Na hata unapoajiri, angalia sifa ambazo mtu anazo na kama unaweza kwenda nazo.

Usijidanganye kwamba sifa fulani ambayo mtu anayo unaweza kuibadili, unatafuta matatizo wewe mwenyewe.

Mtu mmoja amewahi kuulizwa anawezaje kuwafanya wafanyakazi wake kuwa na tabia nzuri, alijibu kwa kusema; “siwaambii wafanyakazi wawe na tabia nzuri, bali naajiri watu ambao tayari wana tabia nzuri”.

Rafiki, huo ndiyo ufafanuzi wa mambo manne ambayo watu waliuliza sana kwenye makala ya 20 KWA 20, naamini yameeleweka vizuri na utakwenda kufanyia kazi ili mwaka wako 2020 uwe bora sana kwako.

Kama hukusoma makala hiyo unaweza kufungua hapa na kuisoma; https://amkamtanzania.com/2019/12/27/20-kwa-20-fanya

Nikukaribishe twende pamoja kwa mwaka 2020 hasa kwenye usomaji na uchambuzi wa vitabu kupitia channel ya SOMA VITABU TANZANIA, kujiunga na channel hiyo fungua hapa; https://www.t.me/somavitabutanzania

Wako rafiki katika safari ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa,

Kocha Dr Makirita Amani,

Rafiki, kama ungependa kuendelea kupokea makala na mafunzo mengine mazuri kwenye email yako, fungua hapa na ujaze fomu; www.bit.ly/amkaemail

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.

Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania