Kama kazi yako haihusishi mitandao ya kijamii, kutumia mitandao wakati wa kazi ni kutoroka kazi yako.

Kama kazi yako haihusishi matumizi ya simu, kutumia simu wakati wa kazi ni kutoroka kazi yako.

Kama kazi yako haihusishi majungu na kufuatilia maisha ya wengine, kufanya mambo hayo wakati wa kazi ni kutoroka kazi yako.

Hili ni jambo ambalo kila mtu anapaswa kulijua, kwamba kazi yako kuu ni kufanya kazi yako, na kutokuruhusu usumbufu wa aina nyingine ukuondoe kwenye kazi yako.

Lakini cha kushangaza, wengi wanaruhusu kusumbuliwa kwenye kazi, wanavipa umakini vitu ambavyo havistahili kupewa umakini wowote.

Kila unapoianza kazi yako, jipe muda wa kuzama hasa kwenye kazi hiyo na kutokuruhusu usumbufu kwenye muda huo. Wakati wa kazi, kazi inakuwa ndiyo kipaumbele cha kwanza kwako na ukishaipa kipaumbele sahihi, utapata matokeo ambayo ni bora.

Fanya kazi wakati wa kazi na hayo mengine yaruhusu wakati ambao siyo wa kazi. Kuchanganya kazi na mambo mengine ni kujizuia wewe mwenyewe usipige hatua.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha