Tunaishi kwa kutegemeana, licha ya kuwa kila mmoja anatakiwa kujijengea misingi ya kujitegemea.
Hata kama tutajenga misingi ya kujitegemea bado huwezi kujiita wewe ni jeshi la mtu mmoja.
Kwani kujitegemea siyo kujitosheleza.

Bado watu wengi hawajajua kuwa jukumu la maisha yao ni lao wenyewe. Watu ambao bado hawajajitambua huwa wanafikiri jukumu la maisha yao siyo lao.

Ndiyo maana huwa hawajitumi ipasavyo na kutokukoma kulalamika hovyo.

Usipojua kuwa jukumu la maisha yako ni lako, kamwe huwezi kufanikiwa. Kwani msingi wa kwanza wa kufanikiwa lazima ujue haswa nini unataka kwenye maisha yako.
Sasa kama unaona jukumu la maisha siyo lako utawezaje kujua kile unachotaka kwenye maisha yako?

Iko wazi kabisa kuna watu ambao huwa hatuwezi kuwakosa katika kila eneo la maisha yetu na watu hao siyo wengine bali ni watu wa kuwalaumu.

Kama mahusiano yako hayako vizuri basi ukiulizwa kwanini huwezi kukosa mtu wa kumlaumu kwa wewe kuwa na mahusiano hayo ambayo unayo sasa.

Ukimuuliza mtu ambaye maisha yake hayana dira, kwanini maisha yako, yako hivyo hawezi kukosa mtu wa kumtupia lawama. Kwanza anaweza kuzitupa kwa wazazi wake, serikali na hata bosi wake.

Sisi binadamu huwa hatukosi watu wa kuwatupia lawama pale tunapoona mambo yetu hayaendi vile tunavyotaka sisi.

Linapotokea tatizo, kitu cha kwanza kufikiria ni nani wa kumlaumu, Nani aliyesababisha kutokea kwa jambo hili na hiki ndiyo kinafanya maisha yetu kurudi nyuma badala ya kwenda mbele.

Iko njia rahisi sana ya kuepuka lawama kwa wengine. Njia hiyo ni kujua kabisa jukumu la maisha yako ni lako mwenyewe na chochote kinachotokea katika maisha yako kiwe kizuri au kibaya jua ni chako wewe ndiyo unahusika kwa yote na wala hupaswi kumtafuta mtu wa kumlaumu.

Jua kabisa wewe ndiyo mkurugenzi wa maisha yako. Maisha yako yakiwa mazuri au mabaya wewe ndiyo umeruhusu yawe hivyo, jua wewe ndiyo msemaji wa mwisho wa maisha yako hivyo usipoamua wewe vile unavyotaka hakuna atakayeweza kukusemea.

Tabia ya ulalamikaji imeweza kuzaa wavivu wengi ambao hawawajibiki kwenye maisha yao.

Usipowajibika na maisha yako unakuwa mzigo kwa wengine. Kila mmoja akiwajibika na maisha yake tunaifanya dunia kuwa sehemu salama ya kuishi kwa kila mmoja wetu.

Hatua ya kuchukua leo; Maisha yako ni jukumu lako na ukiamua kumtafuta mtu wa kumlaumu kwa jinsi maisha yako yalivyo huwezi kumkosa.
Kwa chochote kile kinachotokea katika maisha yako usimtafute mtu wa kumlaumu bali mtu wa kwanza kumkamata awe ni wewe mwenyewe.

Kwahiyo, huwezi kuwa bora katika eneo lolote lile katika maisha yako kama utakua ni mtu wa kutowajibika na maisha yako.

Kumbuka, ni rahisi sana kukwepa majukumu yako, lakini ni ngumu sana kukwepa matokeo ya kukwepa majukumu yako.
Usiwe mtu wa kutafuta sababu

Makala hii imeandikwa na
Mwl. Deogratius Kessy
ambaye ni mwalimu, mwandishi na mjasiriamali.

Unaweza ukatembelea mtandao wake kujifunza zaidi ambao ni http://kessydeo.home.blog

Unaweza kuwasiliana naye kwa namba 0717101505//0767101504
deokessy.dk@gmail.com

Asante sana na karibu sana.