Watu wanaweza wasikubaliane na wewe, na wengi watakupinga au kukukosoa, hilo siyo tatizo lako, ni tatizo la mtazamo wao.

Lakini kama watu hawakuelewi, hilo ni tatizo lako wewe, na siyo tatizo lako, hata kama watu hao uelewa wao ni mdogo.

Kwa chochote unachofanya au kusimamia, hakikisha unaweza kumweleza mtu yeyote akaelewa kwa hakika unafanya nini au kusimamia nini. Kukubali au kukataa hiyo ni juu yake, lakini kuelewa, ni juu yako.

Chochote unachofanya au kusimamia, unapaswa kuweza kukieleza kwa umakini na usahihi kwenye sentensi moja, ambayo mtu yeyote anaweza kuielewa. Na kama huwezi kufanya hivyo, basi wewe mwenyewe hujakielewa kitu hicho.

Hili ni muhimu sana kwenye biashara, watu wengi wamekuwa wanashindwa kuwashawishi wateja kununua wanachouza, kwa sababu hawawezi kuwaelezea kwa lugha rahisi na inayoeleweka. Wanaeleza mambo mengi ambayo yanaishia kumchanganya kabisa mteja.

Wewe usiwe hivyo, elewa biashara yako na kile unachouza kiasi kwamba unaweza kueleza kwa sentensi moja na bibi yako asiyejua kusoma wala kuandika akaweza kukuelewa.

Sentensi hiyo moja inapaswa kueleza manufaa ya kile unachouza na kwa nini mtu akinunue hicho badala ya kununua kingine.

Ukiweza kuielewa biashara yako kwa undani kiasi hicho, kuitangaza na hata kuuza hakutakuwa tatizo kwako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha