Tunajua hili, kwamba sisi binadamu tunasukumwa kuchukua hatua kwa hisia kuu mbili, tamaa na maumivu. Tunafanya kile ambacho kinatupa manufaa na kuacha kile ambacho kinatupa maumivu.

Kwenye tamaa, ipo nguvu kubwa sana inayotusukuma kuchukua hatua, ambayo ndani yake pia kuna maumivu kama tusipochukua hatua. Nguvu hiyo ni uhaba. Tunapojua kwamba kuna uhaba wa kitu, basi tunakithamini zaidi, kwa kuwa tunakihitaji, lakini pia kuna hatari ya kukipoteza.

Watu wengi wametumia nguvu hii ya uhaba kuwasukuma watu kufanya vitu ambavyo havina manufaa kwako.

Na mifano ipo wazi, umewahi kutoka nyumbani ukiwa huna mpango wowote wa kununua kitu, njiani ukakutana na promosheni ya kitu fulani na kuambiwa kuna punguzo la bei ambalo ni kwa siku hiyo tu, na ukashawishika kununua. Hao nguvu ya uhaba imefanya kazi kwako. Umenunua siyo kwa sababu unahitaji (maana kama ungekuwa na uhitaji kweli ungeshaenda kutafuta kitu hicho), bali umenunua kwa sababu ya hofu ya kukosa ofa hiyo ambayo ni ya leo tu.

Jifunze kufanya maamuzi yako bila ya kuathiri wa na hisia, hasa ile ya kupoteza au ya uhaba. Mara zote jua ya kwamba, kuna utele wa vitu. Na hili unaweza kulijaribu wewe mwenyewe. Kwa makusudi kabisa, fuatilia matangazo yote ya promosheni mbalimbali ambazo zina ukomo, kisha nenda katake kupata promosheni hizo baada ya muda wa ukomo kuisha, utapata bila ya shida yoyote ile.

Hata wale anaokuambia nafasi ni chache, wewe nenda muda wowote na utapata nafasi utakayo.

Jifunze kuzielewa lugha za matangazo ili zisikubabaishe na kukusukuma kufanya maamuzi yasiyo na manufaa kwako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha