“Kifo siyo kizuri na wala siyo kibaya, bali ni sheria pekee ambayo inaleta usawa kwa watu wote.” —Seneca
“Unachoona kinatokea kwa wengine, jua na kwako kitatokea pia. Unapoona jirani yako amefiwa na mzazi au mtoto, jua na wewe yatakukuta pia, hivyo kuwa na maandalizi sahihi” – kocha Dr Makirita Amani.
Maombolezo ni sehemu ya maisha yetu sisi binadamu. Hii ni kwa sababu kuna mambo mengi ambayo huwa yanatokea ambayo hatukutarajia yangetokea kwa wakati au namna yalivyotokea.
Na pia maombolezo hayalingani, mtu aliyefiwa na ndugu hawezi kuwa na maombolezo sawa na aliyefiwa na mtoto wake ambaye alikuwa anamtegemea sana.
Hivyo maombolezo yanategemea sana ukaribu wa watu na namna walivyotegemeana.
Watu wengi wamekuwa wana maombolezo yasiyo na ukomo, hasa pale watu wa karibu kwao wanapofariki. Na hili limekuwa linapelekea watu hao kushindwa kuwa na maisha bora.
Mwanafalsafa Seneca kwenye moja ua insha zake aliyoiandika kwa Marcia, aliweza kumfariji njia bora ya kuvuka maombolezo na kuweza kuwa na maisha yenye furaha licha ya kumpoteza mtoto wake ambaye alimpenda sana.
Kuna mengi sana ambayo Seneca ameshauri kwenye insha hiyo, ambayo utayapata kwenye uchambuzi wake uliopo kwenye channel ya SOMA VITABU TANZANIA, lakini hapa nakwenda kukushirikisha njia moja unayoweza kuanza kuitumia mara moja na itakupa matokeo mazuri.
Njia hiyo ni kutumia furaha na upendo.
Seneca anasema unapokuwa unaomboleza kuhusu kifo cha mtu wako wa karibu, basi jiulize swali hili; je unaomboleza kwa sababu hukumpenda mtu huyo au kwa sababu unaona ungeweza kumpenda zaidi kama angeishi muda mrefu zaidi?
Kama jibu ni hukumpenda wakati akiwa hai, huna haja ya kuomboleza, kwa sababu kwa asili binadamu huwa hatujali sana kuhusu kitu tusichokipenda au kukifurahia.
Kama jibu lako ni ungeweza kumpenda zaidi pia huna haja ya kuomboleza kwa sababu ulipata nafasi ya kumwonesha upendo mtu huyo kwa wakati uliokuwa naye na hivyo unapaswa kushukuru kwa hilo.
Rafiki, unaona jinsi unavyoweza kutumia upendo kumaliza maombolezo, kwa kujua kwamba kama hukumpenda mtu, basi hata huko aliko atakuwa na hasira na wewe akikuona unaomboleza, maana utakuwa ni unafiki. Na kama ulimpenda pia huko aliko atakuwa na hasira na wewe kwa sababu utakuwa ni ubinafsi kwako kutaka abaki na wewe milele.
Seneca ametushirikisha njia nyingine nzuri sana za kuondokana na maombolezo yasiyo na mwisho.
Ametuonesha kwa nini kifo ni kitu kizuri, na ndiyo ukombozi kamili wa binadamu.
Ametufundisha jinsi ambavyo kila tulichonacho tumekipeshwa tu, na ipo siku kitachukuliwa.
Na pia ametuonesha kwamba, muda wetu hapa duniani ni mfupi mno ukilinganisha na muda ambao dunia imekuwepo, hivyo wajibu wetu ni kuutumia muda huo vizuri.
Pata uchambuzi kamili wa insha ya Seneca inayoitwa Consolation To Marcia na ujifunze njia hizi za kukabiliana na maombolezo.
Unaweza kupata uchambuzi huo kwenye channel ya SOMA VITABU TANZANIA kujiunga fungua; https://www.t.me/somavitabutanzania
Rafiki, kama ungependa kuendelea kupokea makala na mafunzo mengine mazuri kwenye email yako, fungua hapa na ujaze fomu; www.bit.ly/amkaemail
Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.
Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania