Kuna njia tatu za kuwa na kufanya chochote unachofanya kwenye maisha yako, kuanzia kwenye kazi na biashara mpaka kwenye mahusiano.
Unaweza kuwa au kufanya kitu cha bei rahisi, hapa unatoa kilicho bei rahisi na wewe mwenyewe unakuwa wa bei rahisi na hivyo watu hawakupi thamani kubwa.
Unaweza kuwa mtu wa kufanya vitu vyako kwa haraka na hivyo kuokoa muda wa wengine na hivyo wakanufaika sana kupitia kile unachofanya.
Na unaweza kufanya kile kilicho bora, ukakifanya kwa viwango vya juu na kutoa thamani kubwa kwa wengine na hili kukuweka wewe juu.
Sasa ubaya ni kwamba, huwezi kuwa au kufanya vyote vitatu kwa pamoja, unaweza kuwa au kufanya viwili tu kwa wakati mmoja. Na hapo ndipo ugumu huwa unaanzia kwa wengi, kwa sababu wangetamani kufanya vyote vitatu lakini haiwezekani.
Unaweza kuwa rahisi na haraka, lakini hutakuwa bora.
Unaweza kuwa rahisi na bora, lakini hautakuwa haraka.
Unaweza kuwa haraka na bora, lakini hutakuwa rahisi.
Chagua viwili vitakavyokueleza wewe, ambavyo utaviishi maisha yako yote na kila utakachofanya utakifanya kwa misingi hiyo na usijisikie vibaya pale unapoacha kimoja.
Mfano kama umechagua kufanya biashara ambayo unauza vitu ambavyo ni bora kabisa na mteja anavipata kwa haraka, moja kwa moja bei yako haiwezi kuwa rahisi, hivyo usijisikie vibaya pale unapomweleza bei kubwa mteja, badala yake mweleze kwa nini bei hiyo ni kubwa na kipi anachokwenda kukipata, ambacho hawezi kukipata kwa wengine.
Ni rahisi, haraka na bora, ila unaweza kuchagua viwili tu, je unachagua nini na nini? Fanya uchaguzi wako sasa na ishi kwa uchaguzi huo.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Asante sana kocha somo nzuri sana
LikeLike