Rafiki yangu mpendwa,

Kuna njia kuu mbili za kujifunza kwa wengine ili uweze kufanikiwa.

Njia ya kwanza ni kuwaangalia wale waliofanikiwa na kujua misingi wanayoiishi ili na wewe uweze kuiishi na kufanikiwa. Wanasema mafanikio huwa yanaacha alama, hivyo ukiziona alama hizo na ukaziishi, una nafasi kubwa ya wewe kufanikiwa pia.

Njia ya pili ni kuwaangalia wale walioshindwa na kujua misingi wanayoiishi ili uweze kuepuka kuiishi. Kwa sababu ukifanya kile ambacho walioshindwa wamefanya, utapata matokeo ambayo nao wameyapata ambayo ni kushindwa.

Sasa wote tunajua, jamii zetu zimejaa watu wengi sana ambao hawajafanikiwa kuliko wale waliofanikiwa. Katika watu 100 wanaokuzunguka, ni watano pekee wanaokuwa na mafanikio ya kawaida na mmoja kati ya hao watano anakuwa na mafanikio ya juu zaidi. 95 waliobaki wanakuwa na maisha ya kawaida kabisa na wanakuwa hawajafikia mafanikio.

ushauri wa walioshindwa.jpg

Hivyo katika hali ya kawaida, unazungukwa na watu wengi ambao hawajafanikiwa kuliko waliofanikiwa. Hili lina hatari kubwa, kwa sababu sisi binadamu ni viumbe wa kijamii na hivyo huwa tunapenda kufanya yale ambayo wengine wanafanya. Unapozungukwa na walioshindwa, ni rahisi sana na wewe kushindwa pia.

Hatari nyingine kubwa ya kuzungukwa na wale walioshindwa ni aina ya ushauri wanaokuwa wanakupa. Watu hao huwa wanakuwa na maoni ambayo siyo sahihi, lakini wanayaamini sana na wanataka kila mtu aamini kama wanavyoamini wao. Hivyo unapojaribu kufanya kitu kinyume na wanavyoamini wao, watakupinga, kukukosoa na hata kukukatisha tamaa. Hivyo usipokuwa imara na kukabiliana na watu hawa, hutaweza kupiga hatua.

Ili ufanikiwe, lazima ufanye vitu vyako tofauti na wale wanaokuzunguka, ambao wengi hawajafanikiwa. Lakini utakapojaribu kufanya hivyo, wataibuka wengi wa kukushauri, kukukosoa na kukupinga. Watakuambia kile unachofanya unakosea, watakuonesha njia bora ya kufanya unachopaswa kufanya.

Ni rahisi kuwasikiliza watu hawa, kwa sababu ni wengi na pia ni wa karibu, lakini ukifanya hivyo, jua umechagua kujiangamiza mwenyewe. Kwa sababu unapokea ushauri kutoka kwa ambao hawajafanikiwa, ambao nao wamesikia au kupokea kwa wengine na siyo kwamba wana uzoefu na kitu hicho.

Njia rahisi kwako ya kukabiliana na watu hawa ni kwa kuwauliza swali moja muhimu sana; HUO MPANGO WAKO UMEKUFIKISHA WAPI?

Unapofanya kitu cha tofauti, halafu anajitokeza mtu wa kukushauri au kukukosoa kwa namna unavyofanya, usikasirike wala kupingana naye, bali wewe muulize swali moja, huo mpango wako umekufikisha wapi? Hayo unayonishauri nifanye wewe umeyafanya na yakakufikisha wapi?

Kwa maswali hayo, ukweli utajiweka wazi wenyewe, kwamba kile anachokuambia hakijawa na matokeo mazuri kwake au hajawahi hata kukifanyia kazi, hivyo moja kwa moja kinakosa nguvu na unabaki huru kuendelea na mambo yako bila ya kubughudhiwa na wale walioshindwa.

Mfano umechagua kuishi maisha yako kwa kuthamini muda wako na kuutumia kwenye vitu vyenye manufaa pekee na siyo visivyo na manufaa. Hivyo ukaamua kwamba hutafuatilia habari na wala hutatumia mitandao ya kijamii. Wengine watakaposikia mpango wako huo watakupinga sana, watakuambia utaachwa nyuma, hutajua kinachoendelea na pia utakosa kujenga mtandao wako kupitia mitandao hiyo ya kijamii. Wakati wanakuorodheshea hayo yote, usikimbilie kujitetea, bali wewe uliza swali moja; huo mpango wako wa kufuatilia kila aina ya habari na kuwa kwenye mitandao yote ya kijamii umekifikisha wapi? Kwa mwaka mmoja uliopita hebu onesha manufaa uliyoyapata kwa kufuatilia habari na mitandao ya kijamii. Kama mtu huyo ataweza kuonesha matokeo ya uhakika, labda ni fedha, maarifa aliyoyapata na yakamfanya awe bora au chochote kizuri na kinachoonekana wazi, basi msikilize na jifunze zaidi kwake. Lakini kama hawezi kukuonesha, basi puuza ushauri wake.

Kadhalika utakapotaka kupata mafanikio makubwa zaidi na hivyo kupanga kufanya kazi kwa muda mrefu zaidi ya wengine, watakuja kwako na ushauri wa kila aina. Watakuonesha kwamba unapaswa kufanya kazi masaa fulani kwa siku, kwamba unapaswa kupata mapumziko na mengine mengi. Wewe rudi kwenye swali lako, kwa yule anayekushauri, muulize yeye anafanyaje kazi zake, na kisha muulize mpango wake huo umemfikisha wapi?

Unapouliza swali hili, mtake mtu akuoneshe matokeo halisi na siyo mawazo ya kujifariji. Mawazo ya kujifariji ni kama mtu anaposema; sina fedha lakini nina furaha na mafanikio ya kweli ni kuwa na furaha. Hayo ni mawazo ya kujifariji, kwa sababu unalinganisha vitu ambavyo havipaswi kulinganisha. Fedha na furaha havina uhusiano wowote, lakini vyote ni muhimu. Hivyo kama unajiambia huna fedha ila una furaha, kuna tatizo mahali.

Rafiki, nimalizie kwa kukushirikisha kitu kimoja muhimu sana nilichojifunza kuhusu ushauri, watu wengi ambao wanakuwa tayari kukupa ushauri kabla hujawaomba ni wale ambao hawajafanikiwa. Wana muda mwingi wa kufuatilia maisha ya wengine na kuja na ushauri kwa kila mtu. Na hiyo ndiyo sababu ya kwanza unapaswa kuwa na wasiwasi na ushauri wowote unaopewa na mtu ambaye hujamwomba akushauri.

Wale waliofanikiwa wako bize sana na mambo yao kiasi kwamba hawajui nini kinaendelea kwenye maisha yako. Hivyo kama unataka kupata ushauri wao, ni lazima wewe uende ukawaombe wakushauri, uwaeleze kwa kina hali yako, na hapo ndipo wanapoweza kukushauri.

Lakini wale ambao hawajafanikiwa, wana viherehere kweli vya ushauri, wanajua kila unachopaswa kufanya, lakini hawajawahi kufanya wao, au hata kama wamewahi kufanya basi hakijawapa matokeo yoyote mazuri yanayoweza kukushawishi na wewe ufanye. Swali lako ni moja, huo mpango wao umewafikisha wapi na waweze kukionesha matokeo ambayo wao wameyapata kwa kufanyia kazi kile wanachokushauri. Kama hawawezi kukuonesha hilo, basi wapuuze na endelea kufanya yale uliyopanga.

Rafiki, kama ungependa kuendelea kupokea makala na mafunzo mengine mazuri kwenye email yako, fungua hapa na ujaze fomu; www.bit.ly/amkaemail

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.

Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania