Kama nguo imeharibika na ukaweka kiraka, halafu kiraka hicho kikaharibika tena, wote tunajua kwamba hapo suluhisho siyo kuweka tena kiraka, bali kununua nguo nyingine mpya kabisa.

Jambo hili la msingi kabisa huwa tunashindwa kulitumia kwenye maisha yetu ka kila siku. Ni mara ngapi umekuwa unakutana na tatizo au changamoto fulani, unaitatua, lakini suluhisho lako linaleta tatizo au changamoto nyingine?

Hiyo ndiyo dhana ya kiraka juu ya kiraka, na kama ilivyo kwenye nguo, kiraka kikishachoka, unarudi kwenye msingi mkuu.

Kama kuna tatizo au changamoto ambayo umekuwa unakazana kuitatua kwa muda mrefu lakini inaendelea kujirudia, tatizo siyo changamoto hiyo, bali tatizo ni wewe binafsi. Fikra na mtazamo wako una mchango sana kwenye changamoto ambayo unakuwa unapitia.

Hivyo kukimbilia kuitatua kabla ya kubadili msingi huo, ni sawa na kuweka kiraka juu ya kiraka, unatafuta muda kidogo tu, ila ambao hautakusaidia chochote.

Kila tatizo au changamoto unayokutana nayo kwenye maisha, jiulize ni mara ya ngapi unakutana na tatizo au changamoto hiyo hiyo licha ya kuitatua siku za nyuma. Na kama ni changamoto inayojirudia, basi rudi kwenye msingi.

Rudi kwenye fikra na mtazamo wako, rudi kwenye tabia zako, rudi kwenye mazoea yako, rudi kwenye mfumo wako wa maisha na huko ndipo utakapokutana na kiini cha tatizo au changamoto inayojirudia rudia.

Usijisifie kuwa hodari wa kukabiliana na changamoto, wakati unazitengeneza wewe mwenyewe bila ya kujua. Nenda kwenye kiini na utaweza kuondokana na changamoto nyingi sana.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha