Karibu rafiki kwenye makala ya ushauri wa changamoto mbalimbali zinazotuzuia kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yetu. Swala ni kwamba, changamoto hizi haziji kwa nia ya kutuzuia, ila sisi kushindwa kukabiliana nazo ndiyo tunajizuia kufanikiwa. Lakini ukiweza kutatua changamoto zinazokujia, unafanikiwa zaidi.

Leo tunakwenda kupata ushauri wa jinsi ya kulinda akiba yako isimezwe na matatizo unayokutana nayo. Watu wengi wamekuwa wanaelewa umuhimu wa kujiwekea akiba kutoka kwenye vipato vyao. Wanachukua hatua kweli kwa kujiwekea akiba, lakini yanatokea matatizo ambayo yanaishia kutumia akiba yote ambayo mtu amejiwekea.

Hili ni tatizo kubwa na linalowarudisha wengi nyuma, ila leo tunakwenda kupata jawabu na kuwa na hatua za kuchukua ili lisikuathiri.

 

akiba.jpg

Kabla hatujajua hatua za kuchukua kulinda akiba yako, tusome maoni ya mwenzetu aliyeomba ushauri kwenye hili.

Changamoto yangu inayonibana kufikia malengo ni kutumia akiba yangu sana hasa kwa matatizo mbalimbali yasiovumilika hadi kupelekea mshahara ninaopata kuishiwa nguvu. Natamani sana kujua namna ya kupata mkopo ili nilinde akiba yangu na mshahara kiujumla. Nadhani kwa maono yangu mkopo ndio salama ya akiba za pesa zangu. – H. Lugalo.

Aliloandika mwenzetu hapo juu ndiyo linalotokea kwa wengi.

Tena dunia ni kama huwa inatutega hivi, tukishakuwa na akiba kiasi fulani, basi linatokea tatizo ambalo linagharimu kiasi sawa na akiba ambayo tumejiwekea. Ni kama dunia inatuangalia tuna kiasi gani kisha inatuletea tatizo la kiwango hicho. Na pale ambapo hatuna akiba kabisa, matatizo mengi huwa hayatokei.

Kama umewahi kukutana na hali hiyo, kwamba ukiwa na fedha basi matatizo ndiyo yanakuwa mengi basi jua hili, siyo kwamba matatizo yamekuja kwako kwa sababu una fedha, bali unapokuwa na fedha basi unayaona matatizo mengi. Ukiwa huna fedha kabisa, unaweza kuvumilia chochote, lakini ukiwa na fedha utajiambia huna haja ya kujitesa, fedha ipo.

Hivyo basi, hatua ya kwanza kabisa ya kulinda akiba yako ni kutengana nayo na kuisahau kabisa. Kwenye kitabu cha ELIMU YA MSINGI YA FEDHA nimezungumzia dhana ninayoiita GEREZA LA FEDHA. Yaani ile fedha unayojiwekea akiba, unaiweka kwenye gereza ambalo huwezi kuitoa hata kama una shida kiasi gani. Kwa namna hii, unapokutana na shida mbalimbali, utafikiria kama mtu asiye na fedha, badala ya kukimbilia kutumia akiba ambayo ipo.

Yapo magereza mbalimbali ya kuweka fedha zako na kuzisahau kabisa, kuna akaunti maalumu za kibenki ambazo unaweza kuweka tu na huwezi kutoa, kuna aina za uwekezaji ambazo ukishaweka mchakato wa kutoa ni mrefu na pia unaweza kuweka makubaliano na mtu au kikundi na mkawa mnaweka akiba na hakuna mtu mmoja anayeweza kutoa, ni mpaka wote mkubaliane na mwanzoni mnawekeana vigezo kabisa ni nyakati zipi ambapo fedha itatolewa.

Isome kwa kina dhana hii ya GEREZA LA FEDHA kwenye kitabu cha ELIMU YA MSINGI YA FEDHA, kama bado hujapata nakala yako piga simu namba 0678 977 007 na utatumiwa au kuletewa kitabu.

Hatua ya pili ya kuchukua ili kulinda akiba yako isitumike kwa matatizo unayokutana nayo ni kuwa na aina mbalimbali za akiba. Usiweke akiba zako zote kwenye fungu moja, badala yake gawa mafungu. Na moja ya fungu muhimu unalopaswa kuwa nalo ni fungu la dharura.

Kwenye akiba unayoweka, kuwa na fungu la dharura, hii ni akiba ambayo unaiweka ili unapokutana na dharura mbalimbali uwe na njia ya kukabiliana nazo. Unapokuwa na akiba hii ya dharura, unailinda akiba yako kuu ya maendeleo au mipango mingine. Pia inakupa utulivu pale unapoweka akiba kuu kwenye gereza kwa kujua lolote likitokea una mahali pa kuanzia.

Usiwe na fungu moja pekee la akiba, kuwa na mafungu mbalimbali kulingana na uhitaji wako, lakini fungu la dharura lisikosekane.

Njia ya tatu ya kulinda akiba yako ni kupima uzito wa tatizo kabla ya kukimbilia kutumia akiba yako. Hata ukijiwekea akiba ya dharura, unahitaji kuweka vigezo kabisa kwamba dharura ni nini. Bila ya kuweka vigezo, kuna siku utakosa hela ya kula mlo mmoja na kujiambia hiyo ni dharura, kitu ambacho sicho. Hivyo ni muhimu sana kuwa na vigezo vya dharura na kisha kupima uzito wa tatizo kabla hujakimbilia kutumia akiba yako. Watu wengi wanapokutana na matatizo, huwa wanaanza kufikiria fedha walizonazo na ndiyo maana huwa wanapata matatizo yanayoendana na fedha walizonazo.

Wewe unachopaswa kufanya ni kuacha kabisa kufikiria akiba yoyote uliyonayo. Unapopata tatizo fikiria kama vile huna fedha yoyote ile, kisha jiulize unawezaje kulitatua. Matatizo mengi huwa yanakosa nguvu pale unapokuwa huna fedha za kuyatatua. Hivyo kila wakati fikiria kama usiye na fedha ili kuona uzito wa tatizo lolote ulilonalo. Na kama tatizo ni zito ambalo lina madhara makubwa, basi tumia akiba yako ya dharura, kama tatizo linaweza kusubiri, basi lisubirishe. Kuwa mzito sana kutoa akiba yako, kwa lolote lile, usikimbilie kutumia akiba yako, jipe muda kwanza kama tatizo siyo dharura hasa.

Nimalizie kuhusu mkopo, maana msomaji mwenzetu ameomba ushauri anawezaje kupata mkopo kwa sababu anaamini ndiyo salama ya akiba yake. Na nikuambie tu wazi rafiki yangu, unacheza na moto. Kama akiba zako mwenyewe huwezi kuzisimamia, kuchukua mkopo ni sawa na kujaribu kuzima moto kwa kutumia petroli, utakwisha kabisa.

Kama bado hujaweza kuwa na nidhamu ya fedha, kama hujaweza kujiwekea akiba na ukailinda wewe mwenyewe, uone mkopo kama kituo cha polisi. Kwa sababu mkopo unakuja na gharama kubwa kwako, utaulipa kwa riba, sasa kama utatumia mkopo huo kwa matatizo yako, unaziba shimo moja kwa kutoboa shimo jingine. Hutaweza kupiga hatua.

Mkopo hauchukuliwi ili kutatua matatizo yako, mkopo unachukuliwa ili kuzalishwa na kuleta faida zaidi. Hivyo kama bado hujawa na kitu kinachozalisha faida, hustahili kujihusisha na mikopo. Kazana na akiba zako kwanza, jenga gereza la akiba zako na kuza akiba zako, kuwa na fungu la akiba ya dharura na jiwekee vigezo vya akiba hiyo na zaidi kuwa mzito kutoa fedha zako na jiulize kama kuna njia mbadala.

Matatizo mengi ya kifedha tuliyonayo ni kwa sababu hatujawahi kupewa ELIMU YA MSINGI YA FEDHA, na hilo ndilo lililonisukuma kuandika kitabu cha ELIMU YA MSINGI YA FEDHA, ambacho ukikipata na kukisoma, utaweza kuelewa kwa umakini kabisa nini unapaswa kufanya inapokuja swala la fedha. Kama umeshakipata kitabu hiki kisome na fanyia kazi. Kama bado hujakipata piga simu sasa 0678 977 007 na utapata nakala yako na kuanza kujijengea uhuru wa kifedha.

elimu fedha 2

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania