Kinachofanya maisha yetu yawe magumu, kinachotufanya tuwe na msongo ni kwa sababu tunafanya leo yale ambayo tulifanya jana. Kwa kifupi tunafanya kila kitu kwa mazoea na siyo kwa sababu ni muhimu kufanya.

Hata mahusiano uliyonayo na wengine, majukumu unayokubali kutoka kwa wengine, kazi na biashara unayofanya na mengine mengi, yote ni kwa sababu ndivyo ambavyo umekuwa unafanya siku za nyuma. Hivyo umejibebesha mizigo mingi, ambayo haina maana wala umuhimu wowote kwako.

Kuondokana na hali hii, unapaswa kuanza upya, anza upya kila siku ya maisha yako. Kila siku unayoianza, fikiria huna majukumu yoyote, huna makubaliano yoyote na mtu na hulazimiki kufanya chochote. Hapo sasa unaanza kuchagua ni vitu gani ufanye kwenye siku hiyo.

Kwa kufanya hivi, kuanza upya kila mara, utafanya yale ambayo ni muhimu pekee na siyo kuhangaika na mengi ambayo siyo muhimu.

Kadhalika kwenye kazi na biashara zako, usifanye leo kile ambacho umefanya jana. Bali leo anza upya, angalia matokeo unayotaka kupata, malengo uliyonayo na kisha jiulize ni nini unapaswa kufanya leo ili ufikie malengo hayo. Sahau kabisa kuhusu uliyofanya jana, anza upya na kama kuna ulichofanya jana na bado ni muhimu basi utakifanya leo pia.

Yapeleke maisha yako kama unavyokula chakula, huanzi na sahani iliyojaa na kujiuliza kipi cha kuacha au kuondoa, badala yake unaanza na sahani tupu kisha unachagua kipi uweke na kipi usiweke. Ukianza upya una uhuru wa kuchagua yale muhimu na siyo kuhangaika na mazoea.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha