Muda huwa haupatikani, bali muda unatengenezwa.
Ukijiambia kwamba ukipata muda utafanya kitu fulani, unajidanganya.
Kwa sababu huwezi kupata muda, bali unaweza kutengeneza muda.
Wote tunajua jinsi ambavyo mambo ya kufanya ni mengi na muda wa kuyafanya ni mchache.
Hivyo kufikiri kuna siku muda utajitokeza wenyewe, ni kujifariji tu.
Utapata muda kama utachagua kuacha baadhi ya vitu unavyofanya sasa, ili kufanya kile ambacho ni muhimu zaidi. Lakini kama hautakuwa tayari kutengeneza muda, kwa kuamua kuacha baadhi ya vile vinavyopoteza muda wako sasa, kamwe hutakuja kuwa na muda.
Mfano mzuri ni pale mtu unapojiambia kwamba husomi vitabu kwa sababu hupati muda wa kufanya hivyo. Hivyo unapita wiki, mwezi na hata mwaka bila ya kusoma kabisa, kisingizio ni muda.
Lakini hujawahi kukaa wiki hujala kwa kisingizio kwamba huna muda wa kula, au kukaa wiki bila ya kuoga kwa sababu huna muda. Unapata muda wa kufanya vitu hivyo kwa sababu ni muhimu zaidi kwako, upo tayari kuacha vitu vingine, ili tu ufanye hivyo muhimu.
Na hivyo pia ndivyo unavyopaswa kufanya kwa yale mengine muhimu kwako, kama kuanzisha biashara ya pembeni au kujifunza kupitia usomaji wa vitabu, kwa kuchagua kuacha baadhi ya vitu unavyofanya sasa, ili kupata muda wa kufanya yale muhimu kwako.
Muda ulionao sasa, hapo ulipo sasa ndiyo muda sahihi kwako kuchagua kilicho sahihi kwako kufanya. Usijiambie kesho utakuwa na muda zaidi, kama leo huwezi kutengeneza muda, basi jiambie wazi kwamba hutaki kufanya kitu hicho, au siyo muhimu kwako, kuliko kujificha kwenye kisingizio cha muda.
Muda sahihi ni ule unaoutengeneza wewe mwenyewe na siyo wa kusubiri mpaka ujitokeze wenyewe.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Ahsante sana
Umeandika kweli la maana muda haupo kukungojea wewe bali unatengeneza muda kwa yale muhimu na hapa ndipo unaona umuhimu wa kuwa na orodha ya mambo ya kufanya unatenga muda gan utekeleze na ni muhimu kuwa na nidhamu binafsi unapopanga muda huo unapofika unahakikisha unafanya kweli!!!
LikeLike
Karibu Hendry
LikeLike
Asante sana kocha
Nimejifunza kitu muhimu sana kweli muda ni changamoto ya waajiliwa wengi,ila tunawenza kutengenenza muda tukafanya vitu muhimu ili kufika kwenye uhuru wa kifedha
LikeLike
Vizuri Mary,
Fanyia kazi kile ulichojifunza.
LikeLike