Njiti ndogo ya kiberiti inawasha moto mkubwa ambao unaweza kupika au kuunguza kitu kikubwa.

Je unafikiri kilichopika au kuunguza ni njiti ile ya kibiriti? Najua unajua siyo. Kama ingekuwa hivyo, tungetegemea njiti hiyo ya kiberiti iweze kuunguza maji ukiyawasha, au kuunguza mchanga ukiuwasha kama unayowasha kuni au mafuta.

Sababu inayopelekea njiti ya kiberiti iweze kuwasha kuni, mkaa na mafuta na ishindwe kuwasha maji au mchana ni kile kilichopo ndani ya kitu kinachowashwa.

Ndani ya kuni, mkaa na mafuta kuna nishati kubwa sana ambayo imelala, nishati hii ikiamshwa, inafanya makubwa sana, inatoa moto mkubwa. Njiti ya kiberiti inafanya tu kazi ya kuamsha nishati hiyo iliyolala.

Ndani ya mchanga au maji hakuna nishati kama iliyopo kwenye kuni na mkaa, ndiyo maana njiti ua kiberiti haiwezi kuwasha moto kwenye mchanga au maji.

Hivi pia ndivyo ilivyo kwenye hamasa.

Kuna hamasa ya nje na hamasa ya ndani. Hamasa ya nje ni ile unayoipata kupitia wengine na yale yanayotokea nje yako. Hamasa ya ndani ni ile inayoanzia ndani yako.

Katika hamasa hizi mbili, ya ndani ndiyo yenye nguvu kubwa na yenye uwezo wa kufanya makubwa. Lakini mara nyingi huwa inakuwa imelala. Hivyo huhitaji hamasa ya nje ili kuiamsha. Kama kiberiti kinavyowasha moto mkubwa kwenye kundi au mafuta.

Hivyo basi, hamasa ya nje huwa inafanya kazi pale tu unapokuwa na hamasa ya ndani inayoweza kuamshwa. Kama ndani yako hakuna hamasa kabisa, hamasa ya nje haiwezi kukusaidia. Kukazana kutumia hamasa ya nje ili usukumwe kupiga hatua, ni sawa na kuwasha njiti ya kiberiti na kuiweka kwenye maji ukitegemea maji hayo yawake moto, inaishia kuzima.

Nafikiri unaanza kupata picha kwa nini huwa unapata hamasa unapowasikia wale waliofanikiwa, unatoka ukiwa na nguvu kweli, lakini kesho yake unakuwa umepoa kabisa, hamasa yote imetoweka kabisa.

Siyo kwa sababu hamasa ya nje haifanyi kazi, bali ni kwa sababu haijaifikia hamasa sahihi ya ndani ambayo itashika moto ambao hauzimi.

Hivyo wajibu wako ni mmoja, kujua ilipo hamasa yako ya ndani ili uweze kuiamsha kwa hamasa ya nje. Jua ni kipi hasa unachojali zaidi kisha jipe hamasa kwenye eneo hilo.

Hamasa bora ni ile ya ndani, hivyo hamasa yoyote ya nje unayoitumia, inapaswa kwenda kuamsha hamasa ya ndani. Ni muhimu ujue hamasa yako ya ndani iko wapi na unawezaje kuifikia ili uweze kufanya makubwa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha