Rafiki yangu mpendwa,

Kuna kauli moja ambayo wale walioshindwa kwenye maisha wanapenda sana kuitumia. Huwa wanajiambia kwamba maisha hayana kanuni (fomula) kwamba wale wanaofanikiwa ni kutokana na bahati fulani ambayo walioshindwa hawajaipata.

Japokuwa kuna ukweli kwenye upande wa bahati, lakini upande wa kanuni siyo kweli. Maisha yana kanuni, kuna vitu fulani ukivifanya unajiweka kwenye nafasi ya kufanikiwa na kuna vitu ukivifanya unajiweka kwenye nafasi ya kushindwa. Tuchukue mfano mdogo, kuna wafanyabiashara wawili, wote wanafanya biashara ya aina moja na kwenye eneo moja. Mmoja huwa anafungua biashara yake saa moja kamili asubuhi na kufunga saa tatu kamili usiku, kila siku bila ya kuacha. Mwingine hana muda maalumu wa kufungua wala kufunga, lakini mara nyingi huwa anafungua saa mbili asubuhi na kufunga saa kumi na mbili jioni. Kama hakuna kingine kitakachobadilika, kama huduma wanazotoa ni sawa, unafikiri miaka mitano ijayo yupi ambaye atakuwa amepiga hatua zaidi?

Japokuwa hakuna uhakika, lakini yule ambaye anafungua mapema na kuchelewa kufunga, yupo kwenye nafasi nzuri ya kufanikiwa kuliko ambaye hafanyi hivyo. Je huyu akifanikiwa utasema ni bahati? Utaendelea kusema maisha au biashara haina kanuni?

Rafiki, kama ambavyo nimekuwa nakuambia na leo nakukumbusha tena, maisha yana kanuni, ukizijua na kuzifuata utafanikiwa, usipozijua au ukazijua na ukazipuuza utashindwa, ni rahisi kama hivyo.

Leo nakwenda kukushirikisha misingi itakayokuwezesha kupata chochote unachotaka kwenye maisha yako, hii ndiyo kanuni kuu ya maisha, ambayo ukiifuata, basi utapata kile unachotaka.

Na sitaki unisikilize mimi, bali nataka tumsikilize yule ambaye ametumia misingi hii kwa zaidi ya miaka 40 na ikamwezesha kufanikiwa sana, kiwango cha mafanikio kisichokuwa cha kawaida.

Principles-life-and-Work.jpg

Leo tunakwenda kujifunza kutoka kwa bilionea mwekezaji Ray Dalio ambaye amekuwepo kwenye uwekezaji kupitia kampuni yake ya Bridgewater tangu mwaka 1975, alianzia chini kabisa lakini sasa ni mmoja wa watu matajiri sana duniani, akiwa na utajiri wa zaidi ya dola bilioni 18, huku kampuni hiyo ya uwekezaji ikisimamia uwekezaji wa zaidi ya dola bilioni 160.

Mwaka 2017 Ray alitoa kitabu chake anachokiita Principles: Life and Work ambapo ndani ya kitabu hicho ameeleza misingi ambayo amekuwa anaitumia kwenye maisha na hata kwenye kazi na imemuwezesha kupaa mafanikio makubwa aliyofikia. Ray ameeleza kila kitu kwa lugha rahisi kabisa kuelewa. Kazi ni kwetu kusoma na kujenga misingi ya maisha yetu na kuweza kufanikiwa sana.

Kitabu cha Ray kimegawanyika kwenye sehemu tatu, MAISHA BINAFSI, MISINGI YA MAISHA na MISINGI YA KAZI. Utapata chambuzi za kina za sehemu zote tatu kwenye channel yetu ya SOMA VITABU TANZANIA, ambayo unaweza kujiunga kwa kufungua; https://www.t.me/somavitabutanzania

Kwenye makala ya leo tutakwenda kupata majibu ya maswali muhimu unayoweza kuwa unajiuliza kuhusu misingi, tutapata msingi mkuu wa mafanikio kwenye maisha ambao Ray anatushirikisha na mwisho nitakushirikisha hatua tano ambazo Ray amekuwa anatumia kufanikiwa kwenye uwekezaji.

Karibu sana ujifunze kuhusu misingi kwenye makala ya leo na baadaye ujiunge na SOMA VITABU TANZANIA kupata uchambuzi wa kina zaidi.

MAJIBU YA MASWALI MUHIMU KUHUSU MISINGI.

1) MISINGI NI NINI?

Kila mmoja wetu kuna vitu anavithamini sana kwenye maisha yake. Misingi ndiyo kitu kinachokuwezesha wewe kuishi maisha ambayo yanaendana na kile unachothamini. Misingi inaunganisha kile unachothamini na hatua unazochukua katika kufanyia kazi. Misingi inakuwezesha kukabiliana na uhalisia wa maisha ambao unakutana nao katika kufanya kile unachothamini. Misingi yako ndiyo inakusaidia kufanya maamuzi sahihi pale unapojikuta kwenye wakati mgumu au njia panda na usijue kipi sahihi kwako kufanya.

Kwa kifupi tunaweza kusema misingi ni nguzo zinazokuwezesha kuishi kile unachokithamini kwenye maisha yako.

2) KWA NINI MISINGI NI MUHIMU?

Watu wote ambao wamefanikiwa sana kwenye amisha yao, kuna misingi wanayoiishi ambayo imewasaidia kufanikiwa. Bila ya misingi, utajikuta unasumbuliwa na kila kinachokuja kwenye maisha yako bila ya kujali kama ni muhimu kwako au ndiyo kitu unachojali zaidi. Hali hiyo ya kuhangaika na kila kitu itakuwa kikwazo kwako kupata kile kilicho bora kwenye maisha yako. Kukosa misingi ni kubaya kwa mtu binafsi, lakini kwa kundi la watu (kama taasisi au kampuni) ni mbaya zaidi kwa sababu inasababisha watu kujikuta kwenye misuguano na hakuna hatua wanayoweza kupiga.

Kwa kifupi, misingi inakusaidia kujua kipi muhimu na uhangaike nacho na kipi siyo muhimu hivyo ukipuuze, hii inakupa vipaumbele ambavyo vitakuwezesha kufanikiwa.

3) MISINGI INATOKA WAPI?

Kila mtu kuna misingi ambayo anaiishi, iwe anaijua au haijui na iwe inamsaidia au haimsaidii. Kuna njia tatu za kupata misingi, moja ni kupitia uzoefu wetu binafsi, mbili ni kujifunza kutoka kwa wengine na tatu ni kutoka kwenye mifumo ambayo ipo, mfano dini, katiba na kadhalika. Kutengeneza misingi yako mwenyewe ni kugumu kwa sababu kunakutaka ujaribu na kushindwa mara nyingi ndiyo uweze kujua kipi kinafaa na kipi hakifai. Lakini ndiyo njia bora ya kujenga misingi ya maisha yako, kwa sababu itaendana na uzoefu wako binafsi. Kuchukua misingi ya wengine au ya mifumo ambayo tayari ipo ni rahisi, lakini unapaswa kuiboresha ili iendane na kile unachothamini wewe. Watu wengi wamekuwa wakibeba misingi ya wengine kama ilivyo na kinachotokea ni misingi hiyo haiendani na kile wanachothamini au wanachotaka. Hili linawapelekea kuwa na maisha ya unafiki na hivyo kushindwa kufanikiwa.

Tengeneza misingi yako mwenyewe, kupitia misingi unayojifunza kwa wengine au kutoka kwenye mifumo ambayo tayari ipo. Misingi unayoiishi unapaswa kuiamini bila ya shaka yoyote na kuifuata katika hali zote.

4) JE UNA MISINGI AMBAYO UNAITUMIA KUENDESHA MAISHA YAKO? MISINGI HIYO NI IPI?

Misingi yako ndiyo inayojenga tabia zako. Unapoingia kwenye mahusiano na watu wengine, misingi yako na ya hao wengine ndiyo inayoamua kama mahusiano hayo yatadumu au kuvunjika. Watu ambao misingi inaendana wanakwenda pamoja, lakini wale ambao misingi haiendani hawadumu kwa sababu kila wakati watakuwa wanatofautiana. Mahusiano mengi yamevunjika kwa sababu watu hawajui misingi yao na misingi ambayo wengine wanayo. Anza kwa kujiuliza wewe, angalia mahusiano yote uliyonayo, kuanzia ya mapenzi au ndoa, mahusiano ya kazi au biashara na hata mahusiano ya kindugu na kirafiki, je unaijua misingi unayoisimamia wewe? Na je unaijua misingi ambayo wengine wanaisimamia kwenye maeneo hayo? Muhimu zaidi ni je misingi yako inaendana na misingi ya wengine? Kama jibu ni hapana basi jua mahusiano hayo hayawezi kwenda vizuri, kila wakati mtakuwa na misuguano, siyo kwa sababu hampendani au kujaliana, bali kwa sababu misingi haiendani.

Kabla hujakazana kuboresha mahusiano uliyonayo na wengine, anza na misingi yako na ya hao wengine. Kama misingi inatofautiana, hakuna namna mahusiano hayo yanaweza kuboreshwa.

5) UNAFIKIRI MISINGI YAKO ITAKUSAIDIA KWA KIASI GANI, NA KWA NINI?

Misingi ambayo tunaithamini na inatusaidia sana ni ile ambayo inatokana na uzoefu wetu wenyewe. Pale unapofanya makosa, kisha ukajifunza na kuweka kwenye misingi yako, hutarudia tena makosa hayo na hivyo utaishi misingi uliyojifunza. Kila mara unapokutana na mambo magumu, kushindwa au kuumia unarudi kwenye misingi yako na kuiboresha zaidi kwa kujiuliza maswali magumu na muhimu. Kwa mfano kama umejiweka msingi kwamba hutoiba, msingi huu utafanya kazi kama utajua kwa nini umejiwekea msingi huo. Kwa mfano huo wa kutokuiba, nini kinapelekea wewe usiibe, je ni kwa sababu una huruma kwa wale ambao unawakosesha kile unachoiba? Je huibi kwa sababu kufanya hivyo ni dhambi? Au huibi kwa sababu unaogopa ukikamatwa itakuingiza kwenye matatizo? Kwa kujiuliza na kujipa majibu ya maswali haya kuhusu misingi uliyojiwekea kunakufanya uielewe misingi yako na kuifanya iendane na kile ambacho unakithamini kwenye maisha yako.

Ili kufanikiwa kwenye maisha unapaswa kuweza kufanya maamuzi sahihi katika nyakati ambazo ni ngumu. Lazima uwe tayari kukata mguu ili kuokoa maisha. Siyo kwamba ukiwa na misingi maisha yako yatakuwa rahisi, bali yatakuwa magumu kuliko hata yale unayoishi bila misingi. Lakini ugumu wake unakupa matokeo bora kwa sababu utafanya maamuzi sahihi katika nyakati ngumu.

Maswali hayo matano ni muhimu kujijibu na kuyaelewa wakati unajenga misingi yako ili uielewe vizuri, iendane na kile unachotaka na uweze kuisimamia wakati wote kitu kitakachokuwezesha kufanikiwa zaidi.

MSINGI MKUU WA MAFANIKIO KWENYE MAISHA.

Kupitia kitabu cha PRINCIPLES, Ray ametushirikisha misingi mingi sana, na utajifunza yote hiyo kwenye uchambuzi kamili utakaopatikana kwenye channel ya SOMA VITABU TANZANIA (www.t.me/somavitabutanzania)

Lakini upo msingi mkuu wa mafanikio ambao Ray ameshirikisha mapema kabisa kwenye kitabu hicho na kuendelea kuurudia mara kwa mara.

Msingi mkuu wa mafanikio kwenye maisha ni huu; ili kupata chochote unachotaka kwenye maisha, 1) amua ni nini hasa unachotaka, 2) jua ukweli ni upi na 3) jua nini unapaswa kufanya ili kupata namba moja kwa kutumia namba mbili, huku ukiwa tayari kujifunza wakati unafanya hivyo.

Unaweza kuona ni kitu rahisi, lakini hebu jiulize, ni nini hasa unachotaka kwenye maisha yako? Wengi hawawezi kujibu swali hili, wengi hawajafanya maamuzi wanataka nini na ndiyo maana wanayumbishwa na kila kitu kipya kinachojitokeza. Kadhalika kwenye ukweli, watu wengi hawaujui ukweli kwa sababu wanapenda kuona au kusikia kile wanachotaka na siyo uhalisia

Ukiishi msingi huu wa kuamua ni nini unachotaka, kuujua ukweli na kisha kupata unachotaka kupitia ukweli unaoujua, hakuna utakachoshindwa kwenye haya maisha.

HATUA TANO AMBAZO RAY AMEKUWA ANATUMIA KUFANIKIWA KWENYE UWEKEZAJI.

Kupitia kitabu cha PRINCIPLES, Ray anatushirikisha makosa makubwa aliyoyafanya wakati bado ni mchanga kwenye uwekezaji. Kosa moja lilipelekea kampuni yake kuanguka kabisa na kuanzia sifuri. Katika kutafakari makosa aliyoyafanya, Ray alijijengea hatua tano za kufuata ili asirudie tena makosa hayo. Amekuwa anatumia hatua hizo mpaka leo na zinamsaidia kufanya maamuzi sahihi.

Hatua hizo ni kama ifuatavyo;

1) Fanya kile unachopenda na kutaka kufanya na siyo kile wengine wanataka ufanye.

2) Jenga maoni binafsi kwa kufikiri wewe mwenyewe na siyo kufuata kile wengine wanafikiri au kufanya.

3) Yapime maoni yako kwa kutafuta watu wenye akili na uelewa wanaopingana na wewe na kutafuta wapi wewe unaweza kuwa unakosea.

4) Kuwa makini na kujiamini kupita kiasi na kuepuka kuwa mjuaji wa kila kitu.

5) Kukabiliana na uhalisia, kupokea matokeo unayoyapata na kuangalia ni kipi ulichofanya kuzalisha matokeo hayo ili kuweza kuboresha zaidi.

Ukifuata hatua hizi tano, kila wakati utaweza kufanya maamuzi sahihi, hasa pale unapokuwa umepata mafanikio kidogo. Kwa wengi, mafanikio kidogo huwa ni adui wa mafanikio makubwa. Hii ni kwa sababu watu wakishafanikiwa kidogo wanaamini tayari wanajua kila kitu na hawana tena cha kujifunza, hapo ndipo wanapoanza kufanya makosa ambayo yanawagharimu sana. Tutajifunza kwa mfano kutoka kwa Ray jinsi kujifanya mjuaji kulivyompa hasara kubwa, hakikisha unajiunga na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua www.t.me/somavitabutanzania

rafiki, hapa umejifunza kwa ufupi sana kuhusu misingi na umuhimu wake kwenye maisha ya mafanikio, pia umepata msingi mkuu ambao ukiishi hutabaki pale ulipo sasa. Nikukaribishe kwenye channel ya SOMA VITABU TANZANIA uweze kupata uchambuzi kamili wa kitabu Principles: Life and Work kilichoandikwa na Ray Dalio ili uweze kujifunza misingi sahihi ya kuwa nayo kwenye maisha itakayokusaidia kufanikiwa sana. Kujiunga na channel ya SOMA VITABU TANZANIA, fungua www.t.me/somavitabutanzania kisha bonyeza JOIN CHANNEL.

Rafiki, kama ungependa kuendelea kupokea makala na mafunzo mengine mazuri kwenye email yako, fungua hapa na ujaze fomu; www.bit.ly/amkaemail

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.

Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania