Divert your gaze from the world of lies. Do not trust your feelings. Only in yourself, only in your impersonal self, can you find the eternal. —DHAMMAPADA, a book of BUDDHIST WISDOM
Kuiona siku hii mpya ya leo ni jambo la kipekee sana kwetu.
Ni nafasi bora kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Tutumie muda wetu vizuri kwa yale ambayo ni muhimu.
Huwa tunafanya maamuzi kwa njia mbili,
Njia ya kwanza ni hisia, haya huwa ni maamuzi ambayo tunayafikia haraka sana pale tunapokutana na jambo au kuwa kwenye hali fulani.
Njia ya pili ni fikra, haya huwa ni maamuzi ambayo tunayafikia taratibu, baada ya kuwa tumefikiri jambo husika kwa kina.
Makosa mengi ambayo tunayafanya kwenye maisha yetu, huwa yanasababishwa na kuamini maamuzi ambayo tumeyafanya kwa hisia.
Tunakutana na hali fulani, hisia zetu zinakuja na jibu la haraka na hilo ndiyo tunalotimiza.
Baadaye tunajikuta tumetengeneza matatizo zaidi kwa kuziamini hisia zetu.
Hatupaswi kuziamini hisia zetu na kuzipa kazi ya kufanya maamuzi.
Badala yake kwa kila maamuzi unayofikia haraka kwa hisia, jipe muda kabla hujayatekeleza,
Jipe muda hisia hizo zitulie na uweze kufikiri kwa usahihi.
Kama ambavyo huwezi kutumia maji yaliyokorogeka na uchafu, unasubiri yatulie, ndivyo na akili yako ilivyo. Ikiwa imekorogeka na hisia, ni vyema kuiacha itulie.
Jambo jingine hatari kuliko kufanya maamuzi kwa hisia ni kutumia fikra zako kuhalalisha hisia hizo.
Ni rahisi sana kujidanganya, kujiambia hakuna namna nyingine, kuona umeshafanya kila linalowezekana.
Lakini huo siyo ukweli, ukweli ni kwamba unakuwa mvivu, maana kazi ya kufikiri siyo lele mama.
Usiamini hisia zako, tumia fikra zako kufikiri kwa usahihi mambo yote muhimu kabla hujafanya maamuzi.
Hili ni jambo litakalokuwezesha kufanya maamuzi bora na kuepuka changamoto mbalimbali.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Wako rafiki katika safari ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa,
Kocha Dr. Makirita Amani,
http://www.t.me/somavitabutanzania