“You want praise from people who kick themselves every fifteen minutes, the approval of people who despise themselves?” – Marcus Aurelius

Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine mpya, siku bora na ya kipekee sana kwetu.
Ni nafaso nzuri kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.

Ni kawaida kwetu sisi binadamu kupenda kusifiwa au kukubalika kwa yale ambayo tunayafanya.
Huwa tunajisikia vizuri sana pale wengine wanapotusifia na kutukubali kwa kile tunachofanya.
Na huwa tunajisikia vibaya ma hata wakati mwingine kukata tamaa pale ambapo hakuna anayetusifia au kutukubali.

Kwa tabia hii, tumekuwa tunajizuia sana kufanya makubwa, kwa sababu tunapojaribu kufanya makubwa ambayo wengine hawayaelewi, hawatusifii wala kukubaliana na sisi.
Hivyo inakuwa rahisi kwetu kukata tamaa na kutokuendelea.

Rafiki, kuvunja kabisa tabia hii mbaya, hebu fikiria hivi,
Ni watu gani hao unaotaka wakukubali, watu ambao unathamini sana kusifia kwao kiasi kwamba uko tayari kuacha kitu kama hawajakusifia au kukukubali?
Ni watu hawa hawa ambao wao wenyewe hawajisifii wapa kijikubali?
Watu hawa ambao wanaweka malengo na mipango yao wenyewe, lakini inapofika wakati wa kutekeleza wanaahirisha?
Watu hawa hawa ambao wana sababu kedekede za kwa nini hawachukui hatua?
Watu hawa ambao wanapingana na wao wenyewe?
Kweli kabisa unakubali maisha yako yaamuliwe na watu ambao hata hawajaamua maisha yao?

Hii siyo sahihi, hujitendei haki kujizuia kufanya kitu kwa sababu wengine hawakubaliani na wewe, wakati wao wenyewe hawakubaliani na nafsi zao.
Kama kitu ni muhimu kwako, na kama ni sahihi, basi fanya.
Fanya siyo kwa sababu utaonekana, kukubalika na kusifiwa, bali fanya kwa sababu ni muhimu kufanya.
Na usiruhusu maisha yako yaamuliwe na watu ambao hawawezi hata kuamua maisha yao.

Uwe na siku njema, siku ya kufanya kilicho sahihi kwa sababu ni sahihi kufanya.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma

Wako rafiki katika safari ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.t.me/somavitabutanzania