Maswali hayo mawili yatakuokoa na mambo mengi sana, kama utachukua muda wa kujiuliza kabla hujafanya maamuzi yoyote, hasa ya manunuzi.
Hebu fikiria, umetoka nyumbani kwenda kwenye shughuli zako, hukupanga kununua chochote, lakini unarudi nyumbani una furushi kubwa la vitu ulivyonunua.
Ukiulizwa kwa nini umenunua, utajibu ulikutana na ofa ambayo kama usingechukua hatua usingeipata tena. Au ulikutana na kitu ambacho umekitafuta muda mrefu na usingechukua hatua hutokipata tena.
Rafiki, hayo yote ni majibu ya kujifariji, majibu ya kuficha makosa uliyoyafanya baada ya kuruhusu hisia zako zifanye maamuzi badala ya kufikiri.
Umekutana na mtu au tangazo kwamba kuna ofa ya kitu fulani, na inaisha leo, ukakimbilia kununua kwa sababu hutaki kukosa ofa hiyo, siyo kwa sababu unataka sana kitu hicho, ila kwa sababu unaamini hutapata tena siku nyingine.
Nikuhakikishie kitu kimoja rafiki yangu, hakuna kitu ambacho huwa kinatokea mara moja tu, au kitu ambacho kikishapita hakirudi tena. Pia kuna vitu vichache sana unavyokutana navyo ambavyo hiyo ndiyo siku ya mwisho unaweza kuvipata na kwa hakika siyo vile vinavyouzwa.
Hizo ni lugha za kibiashara ambazo zimelenga kukuteka kisaikolojia kwa kuibua hisia zako na kufanya maamuzi ya haraka.
Sasa jiwekee ulinzi wa kisaikolojia, ulinzi ambao utakuzuia usifanye maamuzi yoyote ya haraka.
Kujijengea ulinzi huo, jiulize mwaswali hayo mawili;
Je ni muhimu? Hisia zako zikiona kitu kinaisha, zinaibuka na kukutaka uchukue hatua. Unaweza kununua chakula cha mbwa ambacho kinauzwa nusu bei wakati huna hata mbwa, kilichokusukuma ni nusu bei. Hivyo mara zote kabla hujafikia maamuzi jiulize je ni muhimu? Je ni kitu ambacho kina mchango kwenye maisha yako, kitu ambacho una matumizi nacho kweli?
Je inaweza kusubiri? Hili ni swali muhimu sana unalopaswa kujiuliza. Kila kitu unachosukumwa kukifanya, ambacho hakikuwa kwenye mipangilio yako, weka utaratibu wa kujipa muda wa kusubiri kabla ya kufanya. Jipe siku moja zaidi, ulishakaa siku nyingi bila ya kitu hicho, umekutana nacho leo, dunia haitaisha leo kama hutakinunua. Hivyo jiambie utafanya maamuzi kesho, kisha nenda zako. Kama usiku hutalala kwa sababu unakiwaza kitu hicho, basi kesho yake kakinunue. Lakini kama usiku utalala vizuri kabisa, bila hata kusumbuka, basi achana nacho, siyo muhimu kama unavyodhani, ni hisia zako tu zilikuzidi nguvu.
Ukiwa mtu wa kufanya maamuzi kwa hisia, utaishia kufanya maamuzi ya hovyo, kwa sababu kila mtu ana mbinu za kuteka hisia zako. Jilazimishe kufikiri kabla hujafikia maamuzi na utapunguza makosa unayofanya.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Shukran sana kocha makala hii imesimama watu waipitie ina ushaur wa makosa meng sana tunayofanya ktk maisha toka nijifunze namna ya kutuliza hisia zangu haswa kwa wanaouza vitu kwa matangazo ya nusu bei au promotion imenisaidia sana kuepuka kununua nisiyohitaji
Kuchochewa tamaa kuna mfanya mtu kufanya maamuzi ambapo baadae hisia zinaposhuka ndiyo unakuja kuelewa kumbe hata ulichokinunua hakikua na uharaka na umuhimu ki hvyo!
Kila mtu asome makala hii na kitabu cha predictable irrational cha Heriel kujifunza nguvu ya kisaikolojia iliyojificha ktk kufanya maamuzi tukijua tumefanya maamuz kwa kufikiri sahihi kumbe ni hisia zimechochewa
LikeLike
Asante Hendry.
LikeLike
Biashara nyingi wapo vinzuri kwenye masoko ili kuweza kukushawishi kununuwa bidhaa,kabla ujaenda shopping jitahidii kuandika vitu vya kununuwa kwanza
Asante sana kocha
LikeLike
Karibu Mary
LikeLike