Hakuna mtu yeyote anayeweza kufanya chochote kwako mpaka wewe utakapompa ruhusa ya kufanya hivyo.

Hakuna anayeweza kukuumiza wewe, mpaka wewe umpe ruhusa kwa kuchagua kuumia. Mtu anaweza kufanya atakacho, kwa lengo la kukuumiza, lakini hawezi kukuumiza kama wewe hujampa ruhusa. Unapokubali kuumia, unakuwa umempa mtu ruhusa ya kukuumiza.

Hata wale wanaokuibia na kukutapeli, ni wewe unawapa ruhusa ya kufanya hivyo. Hakuna anayeweza kukuibia au kukutapeli kama hujampa ruhusa ya kujua kwamba una kitu fulani na kumpa ruhusa ya kujua udhaifu wako na kuweza kuutumia kwa manufaa yake.

Hata wanaokuangusha na kukusaliti, ni wewe unawapa ruhusa ya kufanya hivyo, kwa kuwaamini na kutokufanya kazi yako ya kuhakikisha unawajua vizuri, kukubaliana kirahisi na kile wanachokuambia bila kuchunguza mwenyewe, unakuwa umewatengenezea mwanya wa kukuangusha na kukusaliti.

Rafiki, kwenye kila eneo la maisha yako, kwa yale ambayo unalaumu au kulalamikia wengine kukufanyia, jua kwamba wewe ndiye uliyewapa ruhusa, na hivyo ndiyo mtu wa kwanza kujilaumu na kujilalamikia.

Angalia ni maeneo yapo unasumbuka nayo kwenye maisha yako na kisha jiulize ni ruhusa gani umewapa watu kwenye maeneo hayo. Acha mara moja kutoa ruhusa kwa wengine na utakuwa na maisha tulivu kwako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha