Karibu tena rafiki yangu kwenye makala ya ushauri wa changamoto mbalimbali unazopitia kwenye maisha yako na zinazokuzuia kufikia mafanikio makubwa.

Ni watu wachache sana waliofikia mafanikio makubwa kwa sababu hao ndiyo walio tayari kukabiliana na kila changamoto wanayokutana nayo na kuishinda.

Hivyo kama na wewe umejitoa kweli kufanikiwa, basi jua huwezi kuzikimbia changamoto unazokutana nazo, hupaswi kukubali kwamba ndiyo mwisho, bali unapaswa kupambana, kuzitatua na kusonga mbele.

Leo tunakwenda kupata ushauri kwenye changamoto ya kuanzisha biashara ambayo huna ujuzi au uzoefu nayo.

Ushauri mzuri wa biashara ni kwamba unapaswa kuanza biashara ambayo wewe mwenyewe una ujuzi au uzoefu nayo au unaipenda sana kiasi cha kuweza kuifuatilia kwa karibu.

Business-Plan.jpg

 

Lakini kuna wakati unaona fursa eneo fulani, na wewe huna ujuzi wala uzoefu, je uache fursa hiyo ipite hivi hivi? Si sahihi, kama kuna fursa umeiona, unapaswa kuitumia. Hapa tunakwenda kujifunza jinsi ya kuitumia fursa hiyo kwa kuvuka changamoto ya kukosa ujuzi na uzoefu.

Kabla ya kupata ushauri kamili, tupate maoni ya msomaji mwenzetu aliyetuandikia kuomba ushauri kwenye hili;

Mimi nimeajiriwa na huwa natamani sana kufanya biashara ya Duka la spea za magari madogo na makubwa Changamoto niliyokua nayo ni :

  1. Namna ya Kupata Mtaji
  2. Sehemu maalumu ya kuanzisha hiyo biashara.
  3. Sina elimu ya ufundi wa magari mimi ni Daktari

Naomba msaada Tafadhali.

H. Francis.

Rafiki yetu ametushirikisha vizuri hapo juu, nia yake ya kufanya biashara ya spea, lakini ana changamoto kubwa tatu ambazo zinamkwamisha. Hapa tutakwenda kupata majibu ya changamoto zote tatu na yatakuwa na msaada kwa yeyote aliyekwama kwenye changamoto za aina hii.

  1. Namna ya Kupata Mtaji.

Njia bora ya kupata mtaji wa kuanza biashara ni kupitia akiba zako mwenyewe. Usianze biashara kwa mtaji wa kukopa au kuomba kwa wengine. Kuanza biashara ni majaribio, mwanzoni utajifunza mengi kwa kupata hasara na kukosea. Hupaswi kujifunza hayo kwa fedha za wengine ambazo unapaswa kuzirejesha, tena kwa riba.

Kwa kuwa umeajiriwa, basi weka mpango wa kukusanya mtaji kwa ajili ya kuanza biashara yako na jipe muda wa kukusanya mtaji huo.

Nashauri ufanye hivi; kwenye benki ambayo unapokelea mshahara wako, nenda kafungue akaunti maalumu ambayo unaweza kuweka fedha lakini huwezi kutoa. Benki karibu zote zina huduma hii, ila majina yanatofautiana.

Ukishafungua akaunti ya aina hiyo, waelekeze kwamba mshahara wako unapoingia tu, wanakata kiasi fulani na kupeleka kwenye akaunti hiyo. Hivyo kila mwezi kuna kiasi cha fedha kitakwenda kwenye akaunti maalumu ya kukusanya mtaji wa kuanza biashara.

Jipe muda, kulingana na mtaji unaohitaji na kiasi unachoweza kutenga kila mwezi, usiwe na haraka, badala yake kuwa na subira. Wakati unaendelea kukusanya mtaji huo, endelea kujifunza kwa kina kuhusu biashara unayotaka kwenda kuanzisha.

MUHIMU; Kujifunza zaidi kuhusu kupata mtaji kupitia akiba soma kitabu cha ELIMU YA MSINGI YA FEDHA, piga simu 0678 977 007 kukipata.

  1. Sehemu maalumu ya kuanzisha hiyo biashara.

Kuna maswali matatu muhimu sana unayopaswa kujiuliza na kujijibu kabla hujaanzisha biashara yoyote ile.

Swali la kwanza ni je kuna uhitaji? Je watu wana uhitaji au changamoto ambayo wanatafuta suluhisho lake?

Swali la pili ni je wateja waliopo wana mudu kupata kile unachotaka kuwauzia? Kunaweza kuwa na uhitaji, lakini watu wakawa hawana uwezo wa kutimiza mahitaji yao.

Swali la tatu ni je wateja wapo wa kutosha kuiwezesha biashara yako kujiendesha vizuri. Siyo unaona mtu mmoja anaulizia kitu na kusema ni fursa. Hapa pia unaangalia washindani, kama tayari kuna wengi wanafanya biashara kama hiyo na hawana wateja, kwenda wewe ni kujipeleka kwenye matatizo.

Hivyo basi, hii ni kazi (home work) yako na unapaswa kuifanya kwa umakini mkubwa. Wakati unaendelea kukusanya mtaji wako, ambao najua utachukua siyo chini ya mwaka mmoja, anza kufanya utafiti wako.

Tembelea wauzaji mbalimbali wa spea na ongea nao kujifunza. Kama wewe una gari basi nunua spea maeneo tofauti ili kujifunza. Fuatilia upatikanaji wa spea.

Nashauri utenge mwaka mmoja wa kujifunza kwa kina kuhusu biashara ya spea, jua kila kitu unachoweza kujua kuhusu biashara hii, faida inapatikanaje, wateja wakuu ni wapi, mzigo mzuri unapatikana wapi na changamoto zake ni zipi. Na hili lifanye kama ni utafiti ambao unafanya ili uhitimu masomo ya chuoni, andika kila unachojifunza kwa kila unachochunguza.

Pia katika wakati huo, chagua maeneo ambayo unaona yanakufaa kwa biashara hii, maeneo ambayo yana ukaribu na unapokaa au unapofanya kazi, ili angalau uweze kuona biashara yako mara kwa mara.

Epuka sana kuanzisha biashara mpya, ambayo huna uzoefu nayo eneo ambalo ni mbali na ulipo, utadanganywa na kuibiwa.

MUHIMU; Kujifunza zaidi kuhusu kuanzisha biashara ukiwa kwenye ajira, soma kitabu BIASHARA NDANI YA AJIRA, piga simu 0678 977 007 kukipata.

  1. Sina elimu ya ufundi wa magari mimi ni Daktari

Ni muhimu sana ujue kiundani ile biashara ambayo unaifanya, lakini siyo lazima uweze kufanya kila kitu wewe mwenyewe.

Kwenye kila biashara, kuna pande mbili, upande wa kwanza ni wa utaalamu na upande wa pili ni wa biashara. Wewe unapokwenda kuanzisha biashara hii, hauendi kama mtaalamu bali unakwenda kama mfanyabiashara au mjasiriamali.

Na siku zote kazi ya mjasiriamali ni kuja na wazo kisha kukusanya watu sahihi wa kufanyia kazi wazo hilo.

Hapa unahitaji kujua upande wako ni upi, ambao ni wa biashara, hivyo unapaswa kujua kila kitu kuhusu biashara ya spea za magari, na kwa mwaka nilioshauri ujifunze, utayajua mengi sana.

Kwa upande wa utaalamu, hapo tafuta mtu mwaminifu ambaye unaweza kushirikiana naye, yeye analeta utaalamu na wewe unaleta biashara, kwa pamoja mtafanya kitu kikubwa sana.

Changamoto kubwa ya wafanyabiashara wengi wadogo ni kwamba wao ndiyo wataalamu na wao ndiyo wafanyabiashara, hivyo huwa wanaegemea zaidi kwenye utaalamu wao na kusahau kukuza biashara zao, ndiyo maana huwa hazikui, kwa sababu wataalamu huwa wanaona kila kitu wanaweza kukifanya vizuri wenyewe. Ni wagumu sana kuajiri watu wengine wawasaidie kufanya kile ambacho wao wanafanya.

Wewe unaenda kwenye biashara hii siyo kama mtaalamu, na wala usijifanye mtaalamu, wewe nenda kama mjasiriamali, ambaye umeiona fursa, kisha tengeneza timu yako yenye hao wataalamu unaowahitaji. Kuwa na mpango bora wa namna biashara hiyo itakavyokwenda na hilo litakusaidia sana.

Unapoanza biashara hii, hakikisha unaweka mfumo mzuri wa uendeshaji wa biashara, ambao hautamtegemea mtu mmoja na hilo litakupa uhuru wako mapema sana.

MUHIMU; Kujifunza jinsi ya KUTENGENEZA MFUMO WA BIASHARA ambao utakupa wewe uhuru mkubwa, jiunge na KISIMA CHA MAARIFA, kuna mafunzo hayo. Tuma ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa wasap namba 0717396253 na utapewa maelekezo.

Rafiki, ushauri huu kwenye changamoto hizi tatu unamfaa yeyote anayetaka kuanza biashara lakini anakwama kutokana na changamoto hizi. Fanyia kazi ushauri huu pamoja na kupata rasilimali nilizoshauri kwenye makala hii na kwa hakika utaweza kuanzisha biashara kubwa, yenye mafanikio na inayokupa wewe uhuru mkubwa, hata kama huna ujuzi au uzoefu kuhusu biashara hiyo.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania