Kama una bidhaa au huduma, ambayo uko tayari kuwauzia watu wa mbali (wasiokujua) lakini haupo tayari kuwauzia watu wa karibu (wanaokujua) basi hiyo siyo bidhaa au huduma sahihi kuuza.
Kadhalika kama unaweza kuwauzia watu wa karibu, lakini huwezi kuwauzia watu wa mbali ni makosa.
Chochote unachouza, hakikisha unakiamini sana na upo tayari kuwauzia wanaokujua na wasiokujua. Watu wasinunue kwa sababu wanakujua au hawakujui, bali wanunue kwa sababu wana uhitaji na ulichonacho ndiyo kinachowafaa.
Kama unachouza haupo tayari kukitumia wewe mwenyewe au kumshauri mtu wa karibu kwako akitumie, basi pia usiwauzie wale wasiokujua, unaweza kupata faida ya muda mfupi, lakini huna biashara ya muda mrefu.
Kadhalika kama unaweza kuwauzia wale tu unaowajua, kama watu wananunua kwa sababu wanakujua, bado hujaweza kujenga ushawishi wa watu kununua unachouza, hivyo ukishawamaliza unaowajua, umelimaliza soko, hutauza tena.
Hivyo kwenye mauzo, uza kilicho sahihi, unachokiamini na washawishi watu wanunue kitu kwa thamani yake na siyo kwa kukujua au kutokukujua.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,