Ndiyo wakati sahihi kwako kuanza.

Kwa sababu kama unasubiri mpaka uwe tayari ndiyo uanze, nina habari mbaya kwako, hutakuja kuanza, kwa sababu hakuna wakati ambao utakuwa tayari.

Kabla hujaondoa kabisa hatari ndiyo wakati sahihi wa kufanya kitu, kwa sababu hakuna namna unaweza kuondoa kila aina ya hatari kwenye kitu.

Kabla hujajua kila kitu kuhusu unachotaka kufanya ndiyo wakati mzuri wa kuanza, kwa sababu ukiwa unafanya, utajia kipi hujui na kujifunza, kuliko kabla hujaanza, utajifunza mengi ambayo hutayatumia.

Kabla kila mtu hajakubaliana na wewe, ndiyo wakati sahihi wa kuanza, kwa sababu hakuna jambo lolote ambalo kila mtu atakubaliana na wewe, kila mtu atakuwa na maoni yake, ila yako ni muhimu zaidi.

Kama unajua kuna kitu unataka kufanya, na unajua ni muhimu sana kwako kukifanya, basi unapaswa kuanza kukifanya, sasa, na siyo baadaye.

Unavyochelewa kuanza unajichelewesha na siyo kwamba unazidi kuwa bora. Unakuwa bora kwa kufanya, na siyo kusubiri mpaka uwe tayari.

Hata kama utakosea, unajifunza zaidi kwa kukosea kuliko kwa kutokufanya kabisa.

Swali ni je nini umekuwa unataka kufanya lakini unajiambia hujawa tayari? Nafasi ya kuanza unayo sasa, anza.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha