Maamuzi yoyote, yawe mazuri au mabaya, ni bora kuliko kutokufanya maamuzi kabisa.

Usipofanya maamuzi, unabaki umekwama na hakuna matokeo yoyote unayopata.

Unapofanya maamuzi na yakawa siyo sahihi, unakuwa umejifunza kipi sahihi na kipi siyo sahihi kufanya. Hilo litakunufaisha kwa sababu utaweza kufanya maamuzi bora.

Ukifanya maamuzi na yakawa sahihi utapata matokeo mazuri na kuweza kupiga hatua kwenye maisha yako.

Ipo nukuu ya Mark Twain inayosema maamuzi mazuri yanatokana na uzoefu na uzoefu unatokana na maamuzi mabovu. Hii inazidi kutuonesha kwa nini tunapaswa kufanya maamuzi, kwa sababu haijalishi ni sahihi au siyo sahihi, yana manufaa kwetu.

Kitendo tu cha kufanya maamuzi kinakupa kujiamini zaidi kuliko kutokufanya maamuzi. Unapofanya maamuzi maana yake umechagua kitu au upande utakaousimamia, hilo litakutaka ujiamini zaidi.

Kamwe usikubali kupoteza muda wako kwa kutokuwa na maamuzi kwenye jambo lolote lile. Kusanya taarifa zote muhimu unazopaswa kuwa nazo na kisha fanya maamuzi. Maamuzi hayo yatakupa nafasi ya kujifunza zaidi na kujijengea uzoefu bora zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha