Pata picha umeenda kwenye hoteli kupata chakula, mhudumu anakuambia unaweza kula chochote unachotaka, na ukachagua kulipa sasa au kulipa baadaye.

Kwa haraka utaona una uhuru mkubwa sana, kwamba wewe ni kuamua tu unataka kula nini, kulipa siyo tatizo, kama huwezi kulipa sasa, basi unaweza ukalipa tu baadaye.

Lakini ambacho hutakiona ni mtego uliopo kwenye uhuru huo, ukilipa sasa utalipa fedha taslimu, ukilipa baadaye utalipa kwa riba.

Hivi ndivyo maisha yalivyo rafiki, kwenye kila jambo una machaguo mawili, kulipa sasa au kulipa baadaye, uchaguzi ni wako.

Kwa mfano kwenye tabia;

Tabia mbaya zitakupa raha ya muda mrefu, lakini zitakupa maumivu makubwa baadaye. Utaona raha sasa kufanya chochote unachotaka, lakini baadaye ndiyo utayaona madhara ya kila unachofanya sasa.

Tabia nzuri zinakupa maumivu sasa hivi, lakini zinakupa raha na utulivu baadaye. Utaona unalipa gharama kubwa sasa, lakini baadaye hutakuwa na gharama ya kulipa.

Hivyo zingatia sana gharama kwenye kila maamuzi unayofanya, je unachagua kulipa gharama sasa au unapanga kuilipa baadaye. Hakuna namna unaweza kukwepa gharama, unaweza tu kuisogeza mbele na kadiri unavyoisogeza mbele, ndivyo riba unayolipa inakuwa kubwa.

Unaweza kuchagua kujitesa kwa sasa, ukapitia maisha magumu sasa huku ukianzisha na kukuza biashara yako lakini baadaye ukawa na uhuru wa kifedha. Au ukatumia fedha zako kwa namna unavyojisikia sasa, halafu baadaye ukaja kuwa na maisha magumu kwa sababu huna uhuru wa kifedha na umri umekutupa mkono.

Utalipa sasa au utalipa baadaye? Uchaguzi ni wako, lakini jua kwa hakika lazima ulipe. Na kadiri unavyochelewa kulipa, ndivyo gharama inavyokuwa kubwa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha