Rafiki yangu mpendwa,
Jamii ina unafiki mkubwa sana inapokuja kwenye swala la fedha. Ukisimama mbele ya watu na kuwaambia unataka kuwa mwalimu watakusifia, ukiwaambia unataka kuwa padri au mchungaji watakuambia vizuri.
Lakini simama mbele ya watu na waambie unataka kuwa tajiri mkubwa, unataka kuwa bilionea na utapambana kuhakikisha unafikia hilo na ghafla watu wanakuangalia kwa jicho la tofauti. Wanakuambia una tamaa na tamaa hiyo itakupoteza. Watakuambia huna haja ya kujitesa na utajiri, ridhika tu na maisha yako ya kawaida.
Na wakiona huelezi, basi watakuja na kauli yao pendwa, kwamba pesa ndiyo chanzo cha uovu, kwamba matajiri wote ni watu wabaya, wamefikia utajiri wao kwa kuwadhulumu au kuwaumiza wengine.
Leo tunakwenda kujifunza msingi sahihi wa kusimamia kwenye upande wa fedha. Tunakwenda kupata kitu cha kutupa nguvu ya kuendelea na safari yetu ya kusaka utajiri mkubwa. Pia tunakwenda kupata majibu sahihi ya wale wanaobeza malengo yetu ya utajiri na kuyaona kama ni uovu.
Tunakwenda kujifunza hayo kupitia ‘povu’ ambalo Francisco d’Anconia alilitoa kwenye moja ya hafla ambazo alisikia watu wakisema pesa ni chanzo cha maovu. Kama humjui Francisco d’Anconia ni mmoja wa wahusika kwenye Riwaya ya Ayn Rand iitwayo Atlas Shrugged. Riwaya hii inahusu mapambano kati ya nguvu na akili ambapo akili inashinda. Uchambuzi kamili wa riwaya hii upo kwenye channel ya SOMA VITABU TANZANIA, unaweza kupata uchambuzi huo kwa kufungua; https://www.t.me/somavitabutanzania kisha bonyeza JOIN CHANNEL.
Francisco akiwa mmoja wa waliohudhuria sherehe, anasikia mtu akisema pesa ndiyo chanzo cha maovu yote. Francisco anashindwa kuvumilia hilo na anatoa moja ya hotuba bora kabisa za kuitetea pesa nimewahi kusikia. Hapo chini ni hotuba yenyewe, isome, ielewe na itumie katika utafutaji wako wa pesa.
“Kwa hiyo unasema fedha ndiyo chanzo cha maovu? Je umewahi kujiuliza nini chanzo cha fedha? Fedha ni njia ya kubadilishana thamani, ambayo haiwezi kuwepo kama hakuna bidhaa zilizozalishwa na watu wenye uwezo wa kuzizalisha.
Fedha ndiyo msingi pekee ambao watu wanataka kushirikiana kupitia kubadilishana thamani wanaweza kutumia. Fedha siyo chombo cha waombaji (moochers), ambao wanataka bidhaa yako kwa machozi au waporaji (looters), ambao wanachukua bidhaa yako kwa nguvu. Fedha inatengenezwa na watu wenye uwezo wa kuzalisha. Je hicho ndiyo unakiita uovu?
“Unapoipokea fedha kama malipo ya juhudi zako, unafanya hivyo ukiamini kwamba utabadilishana fedha hiyo kwa bidhaa na juhudi za wengine. Siyo waombaji wala waporaji wanaoipa fedha thamani. Hakuna bahari ya machozi wala silaha ambazo zina uwezo wa kugeuza karatasi ulizonazo mfukoni kuwa mkate utakaohitaji ili uweze kuishi. Karatasi unayoiita fedha ni ishara ya heshima kwa nguvu za wale wanaozalisha. Pochi yako ni maelezo ya matumaini kwamba katika wale wanaokuzunguka kuna ambao hawawezi kukiuka kanuni ya maadili ambayo ndiyo msingi mkuu wa fedha. Je huo ndiyo unaona ni uovu?
“Umewahi kujiuliza chanzo cha uzalishaji ni nini? Angalia jenereta ya umeme na jaribu kujiambia kwamba imetengenezwa kwa nguvu bila ya kufikiri. Jaribu kupanda mbegu za ngano bila ya kutumia ujuzi ambao umekuwa unatumika kuilima. Jaribu kupata chakula kwa kutumia nguvu pekee na hapo ndipo utajifunza kwamba akili ya mwanadamu ndiyo chanzo cha kila kinachozalishwa na utajiri wote ambao umewahi kutengenezwa hapa duniani.
“Lakini utasema wenye nguvu wanapata fedha kwa kuwanyonya walio dhaifu? Ni nguvu gani unayomaanisha? Siyo nguvu ya bunduki wala msuli. Utajiri ni zao la uwezo wa mtu kufikiri. Je anayepata fedha kwa kugundua mota amemnyonyaje ambaye hajagundua? Je anayepata fedha kwa kutumia akili yake amemnyonyaje asiye na akili? Mwenye uwezo anamnyonyaje asiye na uwezo? Anayejituma anamnyonyaje mvivu? Fedha inatengenezwa kwanza kabla haijaombwa au kuporwa, inatengenezwa kwa juhudi za watu waaminifu, kulingana na uwezo wake. Mtu mwaminifu ni yule anayejua kwamba hawezi kutumia zaidi ya anavyotengeneza.
“kubadilishana thamani kwa kutumia fedha ni kanuni ya watu wema. Fedha inaegemea kwenye kauli kwamba; kila mtu ni mmiliki wa akili na juhudi zake. Fedha hairuhusu nguvu yoyote kuamua thamani ya juhudi zako isipokuwa maamuzi ya hiari ya yule aliye tayari kubadilishana na wewe juhudi zake. Fedha inakupa nafasi ya kupata thamani ambayo wengine wapo tayari kulipia kwa bidhaa na nguvu zako na siyo zaidi ya hapo. Fedha inaruhusu makubaliano ambayo yana manufaa kwa pande mbili za wanaobadilishana thamani. Fedha inakutaka utambue kwamba watu wanapaswa kufanya kazi kwa manufaa yao na siyo kwa maumivu yao, kwa kupata na siyo kupoteza, kutambua kwamba wao siyo wanyama wa kubeba shida zao, kwamba unapaswa kuwapa thamani na siyo mateso, kwamba kinachowaleta watu pamoja siyo kubadilishana mateso, bali kubadilishana thamani. Fedha inakutaka uuze, siyo udhaifu wako kwa upumbavu wa wengine, bali vipaji vyako kwa fikra zao, inakutaka ununue kilicho bora kulingana na thamani na siyo cha hovyo. Pale watu wanapoishi kwa kubadilishana thamani, kwa kufikiri na siyo nguvu, bidhaa iliyo bora inashinda, mtu anayefanya vizuri na mwenye uwezo mkubwa ndiye anayefanikiwa zaidi. Hii ndiyo kanuni ya maisha, ambayo fedha ndiyo ishara yake. Je hiki ndiyo unaita uovu?
“Fedha ni chombo tu. Itakupa chochote unachotaka, lakini haiwezi kuamua kwa ajili yako. Itakupa njia za kutimiza matakwa yako lakini haiwezi kukupa matakwa. Fedha ni janga kwa wale wanaojaribu kubadili sheria ya usababishi, watu ambao wanataka kuchukua nafasi ya akili kwa kuiba bidhaa za akili.
“Fedha haiwezi kununua furaha kwa mtu ambaye hajui nini anataka, fedha haiwezi kumpa kanuni za maadili kama hajui maadili ni nini na haiwezi kumpa kusudi kama hajui nini anachotafuta. Fedha haiwezi kununua akili kwa mpumbavu, kukubalika kwa mwoga au heshima kwa asiye na uwezo. Mtu anayejaribu kununua akili za wale wenye uwezo kuliko yeye ili wamtumikie anaishia kuwa mwenye hatia kwa walio chini yake. Watu wenye akili wanamwacha lakini waongo na wahalifu huja kwake, wakivutwa na sheria ambayo hajaijua; kwamba hakuna mtu anaweza kuwa mdogo kuliko fedha zake. Je hii ndiyo sababu unaiita fedha uovu?
“Mtu asiye na uhitaji wa fedha ndiye aliye tayari kurithi utajiri, mtu ambaye anaweza kutengeneza utajiri wake mwenyewe bila kujali anaanzia wapi. Kama mrithi analingana na fedha zake zinamtumikia, kama zimemzidi uwezo zinamharibu. Lakini unaangalia na kusema fedha zimemharibu, kweli? Au ni yeye ameziharibu fedha? Usiwaonee wivu wale wanaorithi mali na wakazipoteza, utajiri wao siyo wako na hata wewe ungeupata usingefanya tofauti na wao. Usitamani kwamba urithi ungegawanywa sawa kwa wengi, kuijaza dunia na wanyonyaji hamsini badala ya mmoja hakuwezi kurudisha msingi uliojenga utajiri huo. Fedha ni nguvu inayoishi ambayo isipokuwa na mizizi hufa. Fedha haiwezi kutumikia akili ambayo hailingani nayo. Je hii ndiyo sababu unaiita ni mbaya?
“Pesa ndiyo njia ya kuishi, maamuzi unayotoa kwenye chanzo chako cha maisha ndiyo maamuzi unayotoa kwenye maisha yako. Kama chanzo ni rushwa, umeharibu maisha yako. Je umepata fedha zako kwa uhalifu? Kwa kutumia uovu na ujinga wa wengine? Kwa kuwahudumia wapumbavu ukiamini utapata zaidi ya unavyostahili? Kuwa kushusha viwango vyako? Kwa kufanya usichopenda kwa wale unaowadharau? Kama ndivyo basi pesa hiyo haiwezi kukupa furaha. chochote utakachonunua hakitakuwa na manufaa kwako bali lawama, hakitakuwa mafanikio bali aibu. Kisha utapiga kelele kwamba pesa ni mbaya. Mbaya kwa sababu haijakupa heshima? Mbaya kwa sababu haikupi nafasi ya kufurahia unyonge wako? Je hiki ndiyo chanzo cha chuki yako kwa fedha?
“Fedha itabaki kuwa matokeo na haiwezi kuchukua nafasi yako ya kuwa chanzo. Fedha ni zao la tabia njema, lakini haiwezi kukupa tabia njema wala kuondoa maovu yako. Fedha haiwezi kukupa usichostahili, siyo kwa mwili wala kwa roho. Je hiki ndiyo chanzo cha kuichukia fedha?
“Au unasema kupenda fedha ndiyo chanzo cha maovu? Kupenda kitu ni kujua na kupenda asili yake. Kupenda fedha ni kujua na kupenda ukweli kwamba fedha ni zao la nguvu bora iliyo ndani yako na njia ya kubadilishana thamani na wengine. Yule ambaye yuko tayari kuuza roho yake kwa vijisenti ndiye anapiga kelele kwamba anaichukia fedha, na ana sababu nzuri za kuichukia. Wanaoipenda fedha wako tayari kuifanyia kazi, wanajua kwamba wana uwezo wa kuipata. Wacha nikupe siri ya tabia za watu; mtu anayeidharau fedha ameipata kwa njia zisizo sahihi, anayeiheshimu ameipata kwa njia sahihi.
“Mkimbie haraka sana mtu anayekuambia fedha ni mbaya. Kauli hiyo ni ishara ya mporaji anayekuja. Kama watu wataendelea kuwa duniani na kuhitaji kushirikiana, kama wataiacha fedha, basi njia pekee inabaki kuwa mtutu wa bunduki.
“Fedha inakutaka uwe na tabia njema kama unataka kuzipata na hata kuzitunza. Watu wasio na uthubutu, wasiojiamini na kujithamini, watu wasio na maadili ya haki yao ya kuwa na fedha na hawapo tayari kuitetea kama wanavyotetea maisha yao, watu wanaoona hawastahili kuwa matajiri, hawawezi kubaki na utajiri kwa muda mrefu. Watu hao ni chambo nzuri kwa waporaji ambao hujificha kwa muda mrefu, lakini huibuka pale wanapopata harufu ya mtu anayeomba kusamehewa kwa hatia ya kumiliki utajiri. Watafanya haraka kumwondolea hatia hiyo na maisha yake, kama anavyostahili.
“Kisha utaona ongezeko la watu wasio na viwango, watu wanaoishi kwa kutumia nguvu huku wakiwategemea wanaofanya biashara kuwapa fedha za kupora, watu ambao ni matapeli. Kwenye jamii yenye maadili, watu hao ni wahalifu na sheria zimeandikwa kukulinda dhidi yao. Lakini pale jamii inapofanya uhalifu kuwa haki na uporaji kuwa sheria, watu wanaotumia nguvu kuchukua utajiri wa wale wasio na silaha, fedha hutumika kulipa kisasi. Waporaji wa aina hii huamini ni salama kumpora mtu asiyeweza kujilinda baada ya kupitisha sheria ya kuwanyima kujilinda. Lakini uporaji wao huwa sumaku kwa waporaji wengine, ambao huwapora kama wao walivyopora. Na mashindano yanaendelea, siyo kwa wanaoweza kuzalisha, bali kwa walio na ukatili usio na huruma. Pale nguvu inapokuwa ndiyo kipimo, muuaji anamshinda mdokozi na hapo jamii inaangamia kwa kusambaa kwa uharibifu na uuaji.
“Je unataka kujua kama siku hiyo inakuja? Iangalie fedha. Fedha ndiyo kipimo cha wema wa jamii. Pale unapoona biashara inafanyika kwa lazima na siyo maridhiano, pale unapoona kwamba ili uzalishe unahitaji ruhusa kwa wasiozalisha, pale unapoona fedha inaenda kwa wale wanaopewa upendeleo, pale unapoona watu wanatajirika kwa ufisadi na siyo kwa kazi na sheria haikulindi na watu hao, bali inawalinda wao dhidi yako, pale unapoona rushwa ikihalalishwa na uaminifu kuwa kujitoa sadaka, basi hapo jua jamii yako imeangamia. Fedha ni njia yenye heshima ambayo haishindani kwa bunduki wala kupatana na ukatili. Haiwezi kuruhusu nchi kuwa na nusu wazalishaji na nusu wanyonyaji.
“Pale waharibifu wanapokuja, huwa wanaanza kuiharibu fedha, kwa sababu fedha ndiyo njia peke ya kuwalinda watu na inayowapa msingi wa kuishi. Waharibifu huwa wanachukua dhahabu na kuwapa watu karatasi feki. Kwa njia hii wanaua viwango sahihi na kuanzisha viwango vinavyowanufaisha wao. Dhahabu ina kiwango sahihi cha thamani ambacho ni sawa na utajiri uliozalishwa. Fedha ya karatasi ni mkopo wa utajiri usiokuwepo, ambayo inalindwa na bunduki iliyoelekezwa kwa wale anaotegemewa kuuzalisha. Fedha ya karatasi ni cheki iliyoandikwa na waporaji kwa akaunti ambayo siyo yao kwa kutumia wema wa waathiriwa. Ogopa siku ambayo cheki hiyo itakosa cha kuchukua.
“Unapofanya ubaya kuwa njia ya kuishi, usitegemee watu kuwa wema. Usitegemee watu kubaki na maadili na kupoteza maisha yao kwa lengo la kuwalinda wasio na maadili. Usitegemee waendelee kuzalisha wakati uzalishaji unaadhibiwa na unyonyaji unazawadiwa. Usiulize ni nani anayeiharibu dunia, ni wewe.
“Unaishi kwenye wakati bora sana na wenye mafanikio makubwa na uzalishaji wa hali ya juu, lakini unajiuliza kwa nini ulimwengu huo unaanguka, wakati unadharau damu inayoupa maisha, ambayo ni fedha. Unaichukulia fedha kama watu wa kale walivyoichukulia na unashangaa kwa nini maendeleo yanarudi nyuma. Kwa historia ya binadamu, fedha imekuwa inachukuliwa na waporaji wa aina moja au nyingine, majina yanabadilika lakini njia yao ni ile ile; kuchukua utajiri kwa nguvu na kuwafunga wazalishaji, kuwadharau, kuwadhalilisha na kuwanyima heshima. Kauli kwamba fedha ni mbaya, inatokana na wakati ambapo utajiri ulizalishwa na watumwa ambao walifanya kazi ya aina moja bila ya kuboreshwa. Kwa kipindi ambacho uzalishaji ulisimamiwa kwa nguvu na utajiri kupatikana kwa kuangusha wengine, hakukuwa na cha kuangusha. Katika kipindi chote hicho, watu waliwainua waporaji kama wakuu wa upanga, madikteta wa kuzaliwa na waliowadharau watumwa, wazalishaji, wafanyabiashara na wamiliki wa viwanda.
“Kwa utukufu wa mwanadamu, kwa mara ya kwanza katika historia kumekuwepo na nchi ya fedha ambayo ni Marekani, nchi ya kufikiri, haki, uhuru, uzalishaji na mafanikio. Kwa mara ya kwanza, akili ya mtu na fedha viliwekwa huru na hakukuwa na utajiri wa unyang’anyi bali utajiri wa kazi, badala ya washika upanga na watumwa, wakatokea watengeneza utajiri wa kweli, wafanyakazi bora, waliojitengeneza wao wenyewe, wamiliki wa viwanda.
“Kama utaniambia nitaje kinachoitofautisha Marekani, ni kwa sababu pamoja na mengi mazuri, ndiyo watu wa kwanza kutumia kauli ‘kutengeneza pesa’. Hakuna lugha au taifa jingine ambalo limewahi kuwa na kauli kama hiyo; watu wamekuwa wakichukulia utajiri kama kitu kisicho badilika, ambacho ili mtu akipate, lazima akichukue kwa mwingine, kwa kuiba, kuomba, kurithi, kupora au kupata kama zawadi. Wamarekani ndiyo watu wa kwanza kuelewa kwamba utajiri unaweza kutengenezwa. Kauli ‘kutengeneza fedha’ inabeba msingi mkuu wa maadili.
“Lakini hiyo ni kauli ambayo Wamarekani wamehukumiwa nayo na mataifa ya waporaji yaliyoshindwa. Sasa mfumo huo wa waporaji umegeuza mafanikio yako kuwa aibu, maendeleo yako kuwa hatia, watu wanaofanya makubwa wanachukuliwa kama wabinafsi na viwanda na bidhaa bora kuchukuliwa kama mali iliyozalishwa kwa nguvu kwa kutumia watumwa kama mapiramidi ya Misri. Wale wanaojifanya kwamba hawaoni tofauti ya nguvu ya pesa na nguvu ya mjeledi wanapaswa kujifunza kupitia wao wenyewe.
“Kama hamtatambua kwamba fedha ndiyo mzizi wa mazuri yote, basi mnatafuta anguko. Pale fedha inapoacha kuwa njia ya kubadilishana thamani, watu wanatumika kama njia ya kubadilishana thamani. Unapaswa kuchagua upande mmoja kati ya hizi mbili, damu, mijeledi, bunduki au upande wa fedha. Unaweza kuchagua upande mmoja tu, na huna muda mwingi wa kuamua.
Rafiki, hii ni hotuba ndefu kuhusu fedha, lakini ina mengi sana ya kujifunza, inakujengea msingi imara kuhusu fedha ambapo hakuna yeyote anayeweza kukuteteresha wala kukubabaisha. Elewa msingi huu ili uweze kukabiliana na wale wanaokukejeli kuhusu fedha.
Kupata uchambuzi kamili wa kitabu cha Atlas Shrugged, ili uweze kujionea jinsi ambavyo mfumo wa kinyonyaji unaweza kuangamiza taifa, jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA, fungua; www.t.me/somavitabutanzania kisha bonyeza JOIN CHANNEL.
Rafiki, kama ungependa kuendelea kupokea makala na mafunzo mengine mazuri kwenye email yako, fungua hapa na ujaze fomu; www.bit.ly/amkaemail
Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.
Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania