Upo usemi kwamba hakuna kitu kipya chini ya dunia, kwamba vitu ni vile vile ila tu vinatokea kwa njia tofauti tofauti.

Hata teknolojia mpya zinazokuja sasa, siyo vitu vipya, bali ni njia mpya za kufanya vitu vile vile ambavyo tumekuwa tunavifanya miaka na miaka.

Lakini inapokuja kwenye fedha, kila mtu huwa anasahau historia.

Chukua mfano wa michezo ya upatu, haijaanza leo, ina miaka na miaka, lakini kila wakati unakuja mchezo mpya na watu wanaingia.

Chukua mfano wa kuanguka kwa masoko ya hisa, haijaanza leo, tangu miaka na miaka masoko ya hisa yamekuwa yanaanguka na uchumi kudorora, lakini watu wanaendelea kurudia makosa yale yale na kuumia.

Na hata tukienda kwenye utapeli, hakuna njia mpya ya utapeli ambayo imewahi kugundulika, njia ni ile ile ambayo imekuwa inatumiwa miaka yote na bado inatumika na watu wanatapeliwa.

Ndiyo maana leo nataka nikushauri kitu kimoja rafiki yangu, inapokuja kwenye swala la fedha, rudi kwanza kwenye historia kabla hujafanya maamuzi makubwa.

Historia ya upatu ni hii, wachukue watu wachache, wakupe fedha, halafu watu hao wakalete watu wengine, ambao watalipa fedha, kisha sehemu ya fedha hizo wanazolipa walioletwa, unawalipa waliowaleta. Ili walioletwa nao wapate fedha, wanapaswa kuletwa watu wao. Myororo unakua hivyo mpaka inafika hatua kwamba wanaoletwa hawawezi kulipwa tena na upatu unaanguka na watu kupoteza fedha.

Historia ya kuanguka kwa soko la hisa iko hivi, soko linapanda, watu wananunua zaidi, na watu wanavyonunua zaidi, linaendelea kupanda, na hapo wanaendelea kununua zaidi. Soko linapanda hivyo, mpaka inafikia hatua kwamba haliwezi kupanda zaidi au kunatokea kitu ambacho kinawapa watu wasiwasi, na hapo wachache wanaanza kuuza, hilo linafanya soko kushuka, kwa kuwa soko linashuka, wengi wanauza zaidi, hilo linazidi kushusha soko mpaka baadaye soko linaanguka kabisa.

Historia ya utapeli iko hivi, mtu anakuja kwako, anakuambia ana fedha nyingi, ziko benki au ana madini ambayo akiyauza atapata fedha nyingi, lakini amekwama, hivyo ukiweza kumsaidia kutoka alipokwama, basi akipata fedha hizo au akiuza madini hayo, atakupa fedha nyingi. Unaposikia kupata fedha nyingi, na ushahidi anakuwa amekutengenezea, unawaka tamaa, unaacha kufikiri na hapo unakuwa rahisi kutapeliwa.

Historia sahihi ya kutengeneza fedha na utajiri udumuo iko hivi, mtu anatafuta tatizo ambalo watu wanalo, anakuja na suluhisho la tatizo hilo, kisha anawauzia watu. Kwa sababu watu wana uhitaji sana wa suluhisho hilo, basi wanakuwa tayari kutoa fedha kupata suluhisho hilo. Ndiyo Rockefeller alikuwa tajiri kwa kuwapa watu mafuta, Andrew Carnegie kwa kuwapa chuma, Thomas Edison kwa kuwapa umeme, Bakhresa kwa kuwapa chakula na wengineo.

Rudi kwenye historia kabla hujafanya maamuzi ya kifedha, usijidanganye wala kudanganyika kwamba sasa hivi mambo ni tofauti, hakuna kilicho tofauti hapa duniani, historia imekuwa inajirudia kila mara. Fanya kile ambacho kina historia ya kuleta matokeo mazuri na utaweza kupata kile unachotaka.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha