Rafiki yangu mpendwa,
Kama unajihusisha na watu, iwe umewaajiri, unawasimamia, unawaongoza au kuwafundisha, motisha au hamasa ni kitu muhimu sana unachopaswa kukitumia.
Mara nyingi watu huwa hawafanyi kile wanachopaswa kufanya mpaka kuwe na kitu cha kuwahamasisha kufanya kitu hicho.
Unaweza kutumia nguvu au udhibiti kuwasukuma watu wafanye kile unachotaka wafanye, lakini hilo halitakupatia matokeo mazuri.
Hivyo njia bora ni kujua ni kitu gani kinawahamasisha au kuwapa motisha watu, kuwapa kitu hicho na wao kukupa kazi nzuri.
Kwenye kitabu cha HIGH OUTPUT MANAGEMENT, mwandishi Andrew S. Grove ametushirikisha mfumo bora wa kutoa motisha na hamasa uliotengenezwa na mwanasaikolojia Abraham Maslow.
Kwenye kitabu, Andrew ameonesha jinsi ambavyo watu tofauti wapo kwenye ngazi tofauti na hivyo wanahasishwa na vitu tofauti. Kuna watu ukiwalipa zaidi wanahamasika, kuna wengine hata ukiwalipa zaidi hawahamasiki.
Kwenye makala hii tunakwenda kujifunza ngazi tano za mahitaji ya watu na jinsi unavyoweza kuzitumia kuwahamasisha wengine. Karibu ujifunze ngazi hizi na jinsi ya kuzitumia ili uwe na ushawishi bora kwa wengine.
Kupata uchambuzi kamili wa kitabu cha HIGH OUTPUT MANAGEMENT, ambacho kina mengi sana kuhusu usimamizi wenye matokeo bora kwenye biashara au taasisi yoyote, fungua; https://www.t.me/somavitabutanzania kisha bonyeza JOIN CHANNEL.
Karibu upate sehemu ya uchambuzi huo ambayo inagusa ngazi tano za mahitaji na jinsi zinavyoweza kutumika kutoa motisha kwa wengine.
Jinsi meneja anavyoweza kuhamasisha timu yake.
Swali ambalo wengi wamekuwa wanajiuliza ni wanawezaje kuwahamasisha wengine. Jibu ni kwamba siyo rahisi kumhamasisha mtu, bali mtu anajihamasisha mwenyewe. Anachoweza kufanya meneja ni kutengeneza mazingira sahihi ambayo yatamhamasisha mtu kujituma zaidi.
Kumekuwa na njia mbili za kuwahamasisha watu, zawadi na adhabu. Zawadi inatolewa pale mtu anapofanya vizuri na adhabu pale anapofanya vibaya. Njia hizi zilikuwa zinafanya kazi vizuri kipindi ambacho kazi zilikuwa ni za nguvu. Lakini zama hizi ambapo kazi nyingi ni za akili, adhabu na zawadi havifanyi kazi vizuri.
Andrew anatuambia njia bora ya kuhamasisha ni kutumia mfumo uliotengenezwa na mwanasaikolojia Abraham Maslow ambaye alitengeneza hadharia ya hamasa kutumia mahitaji ya mtu. (MASLOW HIERARCHY OF NEEDS)
Kupitia mfumo wa Maslow, anaonesha kwamba mahitaji ya mtu ndiyo yanamsukuma kuchukua hatua. Na mahitaji haya yamegawanyika katika ngazi mbalimbali, kuanzia chini kwenda juu. Hitaji la chini lazima likamilike kabla mtu hajahamasika kwenda kwenye hitaji la juu.
Ngazi tano za mahitaji kwenye mfumo wa hamasa wa Maslow.
Kupitia mfumo wa hamasa wa maslow, kuna ngazi tano. Ngazi hizi zinaenda kwa mfuatano, kwamba lazima ngazi ya chini itimizwe kabla mtu hajaenda kwenye ngazi ya juu.
Ngazi ya kwanza; mahitaji ya msingi.
Kwenye ngazi hii ya kwanza mtu anasukumwa na mahitaji ya msingi ili maisha yake yaweze kwenda. Mahitaji haya ni chakula, mavazi na malazi. Kama mtu hana vitu hivi, hawezi kutulia kabisa.
Ngazi ya pili; mahitaji ya usalama.
Baada ya mtu kupata mahitaji ya msingi, kinachomsukuma kuendelea ni kupata usalama. Hapa mtu anajihakikishia kwamba hawezi kurudi kwenye hatari ya kukosa mahitaji ya msingi.
Ngazi ya tatu; mahitaji ya kijamii.
Hapa mtu anakuwa anasukumwa na uhitaji wa kuwa ndani ya jamii au kundi fulani. Hapa mtu anajisikia vizuri pale anapokuwa mmoja wa wale walio kwenye kundi fulani, ambalo linaendana na kile anachopenda au kuthamini. Hitaji hili ndiyo linawasukuma watu kufanya vitu kwa ajili ya wengine.
Ngazi ya nne; hitaji la kuheshimiwa na kutambuliwa.
Hapa mtu anasukumwa kufanya kitu kwa sababu anataka wengine wamwone, kumheshimu na kumtambua kupitia kile anachofanya. Kwa kifupi mtu anafanya kitu ili asifiwe na wengine. Hitaji hili lina nguvu kubwa, hasa pale mtu anapokuwa ameshajijengea sifa fulani kwa wengine, atakazana kuilinda.
Ngazi hizi nne za hamasa tulizojifunza zina ukomo, yaani mtu akishafikia ngazi hiyo, haiwezi kumsukuma tena. Mfano mtu akishakuwa na uhakika wa kipato cha kuendesha maisha yake, kipato zaidi hakiwezi kumsukuma tena, bali ngazi ya juu ndiyo inayoweza kumsukuma. Ngazi ya tano ya hamasa tunayokwenda kujifunza hapo chini haina ukomo, inajichochea yenyewe.
Ngazi ya tano; mahitaji ya kujitambua.
Hili ndiyo hitaji la juu kabisa la kila mtu, hutaji la kujitambua mwenyewe na kuwa kile ambacho mtu anataka kuwa. Hapa mtu anasukumwa na kufikia uwezo mkubwa ulio ndani yake, ambao hauna ukomo. Ngazi hii huwa inaendelea kujichochea yenyewe, kadiri mtu anavyofanya makubwa, ndivyo anavyosukumwa kufanya makubwa zaidi.
Kuna nguvu mbili zinazowasukuma watu kwenye hitaji la kujitambua, ubobezi na mafanikio. Kwenye ubobezi mtu anasukumwa na mtu kubobea zaidi kwenye kile anachofanya, kwa kuboresha ujuzi wake. Mafanikio mtu anasukumwa na matokeo anayozalisha, kwa kutaka kuzalisha zaidi.
Mchango wa fedha kwenye hamasa.
Mameneja wengi huwa wanafikiria fedha ndiyo jawabu la kuwahamasisha wafanyakazi kujituma zaidi. Kwamba ukiwaongezea watu kile unachowalipa, basi watajituma zaidi. Au ukiwaahidi kuwaongezea kipato watajituma ili kupata nyongeza hiyo.
Lakini hii siyo kweli kwa wote, kama tulivyoona ngazi tano za hamasa, fedha inafanya kazi kwenye ngazi za chini, lakini kwenye ngazi za juu, fedha haina nguvu kabisa.
Kwenye ngazi za chini, mtu anahitaji chakula, mavazi, malazi na usalama, hapa fedha ni muhimu sana. Lakini mtu akishakuwa na uhakika wa vitu hivyo, fedha inaacha kuwa hamasa kwake.
Hivyo ni muhimu kwa meneja kujua mtu yupo kwenye ngazi ipi ya hamasa ili kujua jinsi anavyoweza kumhamasisha.
Njia rahisi ya kufanya hivyo ni kuangalia kipi kinamsukuma mtu;
Kama nyongeza ya kipato ina uhitaji mkubwa kwa mtu, basi huyu yupo kwenye ngazi ya mahitaji ya msingi na usalama.
Kama kinachomsukuma mtu ni kufanya zaidi ya wengine, kutambuliwa kwa kile alichofanya, huyu yupo kwenye ngazi ya heshima na utambuzi.
Na kama mtu anasukumwa kufanya ili kuwa bora zaidi, basi huyo yuko kwenye ngazi ya utambuzi.
Rafiki, hizo ndizo ngazi tano za mahitaji unazopaswa kuzijua na kuzitumia kutoa hamasa na motisha kwa wengine ili waweze kuchukua hatua ambazo unataka wachukue.
Uchambuzi kamili wa kitabu hiki una mambo mengi sana, ambayo yatakusaidia kuweza kufanya kazi vizuri na wengine, iwe umeajiri, ni meneja au hata mashauri wa watu. Usikose kusoma uchambuzi kamili wa kitabu hiki pamoja na kupata kitabu chenyewe. Karibu kwenye channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua; https://www.t.me/somavitabutanzania kisha bonyeza JOIN CHANNEL.
Rafiki, kama ungependa kuendelea kupokea makala na mafunzo mengine mazuri kwenye email yako, fungua hapa na ujaze fomu; www.bit.ly/amkaemail
Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.
Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania