Ni kuhusu kuahirisha mambo,
Kila mmoja wetu huwa anapata ushawishi huu,
Unapanga vizuri kabisa ni nini utafanya, na kwa wakati gani,
Lakini unapofika wakati wa kufanya, unajiambia hutafanya kwa wakati huo, kwa sababu kuna kingine muhimu zaidi kufanya.
Lakini ukiangalia kwa undani, siyo kwamba hicho kingine ni muhimu zaidi, bali kile unachoahirisha kufanya ni kigumu zaidi.
Inapofika kwenye kufanya mambo magumu na yenye changamoto, huwa tunashawishika kuahirisha kuyafanya.
Ninachokuambia leo ni usikubali kirahisi, mawazo haya yatakujia, lakini yakatae, baki na mpango wako wa kufanya kile ulichopanga kufanya.
Jiambie kwamba wakati unapanga ufanye nini ulikuwa na akili zako timamu, hivyo kuja kugeuka sasa ni kuchagua kujidharau wewe mwenyewe, kitu ambacho siyo kizuri.
Ng’ang’ana na kile ulichopanga kufanya, bila kuruhusu ushawishi wowote ukutoe kwenye kitu hicho.
Ukiweza kujikatalia wewe mwenyewe, vitu kama hivi, unaacha kuwa adui wa mafanikio yako mwenyewe.
Unapopanga kufanya makubwa na muhimu, mawazo ya kuahirisha yatakujia, usiyakubali kirahisi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,