Mpendwa mwanamafanikio,
Hakuna binadamu ambaye hajawahi kuahirisha mambo. Ni asili ya binadamu kuwa na uvivu wa kufanya jambo fulani.
Na inapotokea jambo la kufanya linakuwa kama linakizuizi fulani basi hapo hapo binadamu anachukilia kama sababu ya kuahirisha kile alichokuwa anataka kukifanya.
Kama ingekuwa watu hawaahirishi basi leo hii tungekuwa na dunia bora sana.
Watu wanapata mawazo bora yanayozalishwa na akili lakini ni watu wachache sana wanatii mawazo yao na kuyafanyia kazi.
Dunia inaongozwa na watu ambao wanatumia akili zao vizuri na na njia rahisi ya kuingamiza dunia isiendelee ni watu kutofikiri na kutumia akili zao vizuri.
Matunda ya dunia ya leo yametokana na matokeo ya watu wenye kufikiri na kutumia akili zao vizuri. Na siku wakitumia migomo ya akili dunia haitokuwa na maendeleo.
Na watu wanaahirisha vitu vingi kwa sababu siyo muhimu sana kwao. Kitu kama ni muhimu utawezaje kukiahirisha?
Iko hasara moja ambayo Seneca amesema pale watu wanapoahirisha mambo. Seneca anasema, pale tunapoahirisha mambo maisha yanaendelea kwa kasi.
Huwa tunajidanganya sisi wenyewe kuwa tunapoahirisha mambo tunafikiri tunamkomoa mtu kumbe wala, tunajikomoa wenyewe na hasara nyingine ni kwamba dunia haisimami kutusikiliza sababu zetu, bali maisha yanaendelea kwa kasi ya ajabu.
Unapoahirisha mambo dunia haisimami hivyo ni unajichelewesha mwenyewe kule unakotaka kufika.
Usiahirishe kitu, acha maisha yako yaende kila siku kama vile kurasa za vitabu, kila siku kurasa moja ya kitabu na usiruke siku hata moja.
Mtu ambaye anamaliza majukumu yake anayagusa maisha yake kila siku. Maliza kazi ili uguse maisha yako na ya wengine pia.
Kuahirisha mambo haisaidii kitu katika maisha yetu, hivyo tunaalikwa kufanya kazi ambayo tunapaswa kufanya.
Tuige mfano wa moyo, moyo ni kiungo pekee ambacho hakijawahi kuahirisha kufanya kazi tokea umezaliwa na siku usipofanya kazi basi na wewe huna uhai.
Fanya kwa sababu ni wajibu wako kufanya na siyo vinginevyo.
Hatua ya kuchukua leo; Usijisumbue kuahirisha mambo kwani kwani hata ukiahirisha dunia inaendelea kwa kasi hakuna kitu kinachosimama bali wewe mwenyewe ndiyo unajichelewesha.
Kwahiyo, fanya kile unachotakiwa kufanya kila siku, na jua unapoahirisha mambo kuna watu wanakutegemea, kila unachofanya jua una athiri maisha ya watu wengine.
Umekuja duniani kutumika na siyo kutumikiwa.
Kila la heri rafiki yangu.
Makala hii imeandikwa na
Mwl. Deogratius Kessy
ambaye ni mwalimu, mwandishi na mjasiriamali.
Unaweza kuwasiliana naye kwa namba zifuatazo; 0717101505/0767101505
deokessy.dk@gmail.com
Pia, mwandishi anakualika kuweza kujifunza zaidi kupitia mtandao wake wa Kessy Deo, unaweza kuingia kwa kutumia link hii hapa http://kessydeo.home.blog
Asante sana na karibu sana