Ili uweze kufanikiwa, kitu muhimu kwako ni kufanya kitu muhimu kuwa kitu muhimu.
Ni rahisi sana kujidanganya kwenye umuhimu, pale unapokuwa na kitu unataka kufanya, unajiaminisha ni muhimu.
Mfano, ukiwa na fedha na ukakutana na nguo inayouzwa na ukaipenda, utajiambia ni muhimu kwako kuinunua, na utajipa sababu nyingi, kwamba hujanunua nguo mpya siku nyingi, una mtoko karibuni unaohitaji nguo mpya au hutaipata kwa bei nzuri kama leo. Hapa utajiaminisha kwamba hicho ni kitu muhimu kufanya.
Lakini ukikutana na nguo hiyo hiyo ukiwa huna fedha, inaacha kuwa kitu muhimu. Haikusumbui kwa namna yoyote ile, wala hujuti kwa kuikosa, kwa sababu unajua huna fedha na huwezi kuipata.
Huu ni mfano mmoja, lakini ndivyo tunavyoyafanya mambo mengi kwenye maisha yetu, huwa tunatengeneza umuhimu kulingana na matakwa yetu na siyo uhalisia.
Hivyo kama unataka kufanikiwa, ni lazima uweze kufanya kitu muhimu kuwa kitu muhimu, yaani kile muhimu kweli ndiyo kinapaswa kupata umuhimu.
Kwa kujua ni wapi unataka kufika, na kujua utawezaje kufika unakotaka kufika, kisha ukachukua hatua sahihi, hapo unafanya kilicho muhimu. Kwenda nje ya mpango huo, haijalishi unajiaminisha kiasi gani kwamba ni muhimu, haitakuwa muhimu.
Chochote unachofanya, jiulize kinachangiaje wewe kufika kwenye mafanikio makubwa unayofanyia kazi, kama hakina mchango, usifanye, hata kama umeshajiaminisha ni muhimu.
Umuhimu unapaswa kupimwa kwa matokeo unayotegemea kupata na siyo kwa matakwa yako binafsi na hisia zako kwa wakati husika.
Mara zote kumbuka hili, kitu muhimu kwako ni kufanya kitu muhimu kuwa kitu muhimu. Na siyo kutengeneza umuhimu ili kutimiza matakwa yako, bali kupima matokeo unayotegemea kupata na kile unachopaswa kufanya.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Ahsante kocha kweli matakwa yetu ndiyo mfadhaiko wetu
Huwa vitu vingine si muhimu kama tunavyojidanganya ni vya muhimu ila ni kipaumbele tunachokua nacho kwa wakati huo unapofanya maamuzi ndiyo maana kuna wakati unakuja kugundua kuna mambo hayakua muhimu kama ulivyokua unafikiria
Mfano kuchukua mkopo kwa vile unasifa ya kukopesheka utajikuta unauchukua tu na muda huo utajilazimisha ni muhimu kuna mambo yanakuĺazimu kufanya kwa wakati huo kwa vhle unayo pesa.
LikeLike
Dah! Ukweli MTU. Vizuri sana kocha kwa hili.
LikeLike
Dah! Ukweli mtupu, kazi nzuri sana kocha. Ahsante.
LikeLike