Kuna vitu vingi vinatokea kwenye maisha yetu na tunafikiri ni miujiza au bahati mbaya, lakini siyo, ni vitu ambavyo tumevitengeneza wenyewe au tumeruhusu vitokee kwa kujua au kutokujua.
Mfano mtu anapojikuta kwenye madeni au amefilisika, hili halitokei kama muujiza au ajali, bali hatua za kifedha ambazo mtu huyo amekuwa anachukua kwa muda ndiyo vimemfikisha hapo alipofika.
Kile unacholisha maisha yako leo, ndiyo kinatengeneza matokeo ya kesho. Matokeo unayopata leo yametengenezwa na hatua ulizochukua huko nyuma.
Mwili ulionao ni matokeo ya vyakula ambavyo umeruhusu viingie kwenye mwili wako.
Akili, fikra na mtazamo ulionao sasa ni matokeo ya maarifa na taarifa ulizoruhusu ziingie kwenye akili yako.
Imani uliyonayo ni matokeo ya upendo na kujali ulikotengeneza kwenye maisha yako.
Ulicholisha maisha yako jana ndiyo kimekufikisha hapo ulipo leo, unacholisha leo ndiyo kinatengeneza kesho yako.
Hivyo kabla hujakimbilia kusema ni muujiza, bahati mbaya au ajali, angalia maisha yako vizuri, utaona ni jinsi gani ulitengeneza kile kilichokutokea. Na kwa kujua hili, utajizuia ili usirudie tena kile ulichofanya kikaleta matokeo uliyopata.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,