Kuna kanuni ya asili, ambayo iko wazi kabisa lakini huwa tunashindwa kuiangalia na hata kuitumia katika kufanya maamuzi yetu ya kila siku.
Kanuni hiyo ni urahisi au uharaka wa kitu, unapima pia urefu wa maisha yake.
Labda tuanze na mfano. Ukipanda mbegu ya mchicha inaota ndani ya siku 3, ndani ya wiki umeshakomaa kwa ajili ya kuliwa na ndani ya mwezi haupo tena. Ukipanda mbegu ya mbuyu, inatumia miaka kuota, inachukua miaka mingine mingi mpaka kukomaa na kuzaa mibuyu na mti huo utaishi kwa miaka mingi.
Mfano huu mdogo unatuonesha kwamba chochote kinachokuja haraka, huwa kinaondoka haraka pia. Chochote kinachokuja kirahisi, huwa kinaondoka kirahisi pia.
Sasa tutumie mfano huu kwenye biashara zetu, kuna njia rahisi za kuwapata wateja, lakini pia huwa wateja wanaokuja kwa njia hizo wanaondoka kirahisi. Mfano ni kupunguza bei, ni rahisi kila mtu kufanya hivyo. Ukipunguza bei leo utavutia wateja wengi kununua kwako, lakini kesho mshindani wako akipunguza bei, wateja wote waliokuja kwa ajili ya bei wanakuhama na kwenda kwa mshindani wako.
Lakini kama utatumia utoaji wa thamani kubwa kuvutia wateja, itakuchukua muda kuwapata wateja sahihi, lakini ukishawapata, utadumu nao kwa muda mrefu.
Hilo ni eneo moja la biashara, lakini mfano huu unatumika kwenye maeneo yote ya maisha yetu. Kwa kila maamuzi unayoyafanya, jiulize kama unatumia njia rahisi au njia ngumu. Kama ni njia rahisi ambayo yeyote anaweza kuitumia, basi jua utakachopata pia utakipoteza kirahisi.
Unataka umaarufu wa haraka kwa kufanya mambo ya ajabu mitandaoni? Kuna mwingine anaweza kufanya ya ajabu kuliko wewe na akawa maarufu kuliko wewe.
Epuka sana njia rahisi, njia za mkato na kile ambacho kila mtu anaweza kufanya, na hapo utaondokana na yale yasiyodumu.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,