Mabadiliko yoyote makubwa unayofanya kwenye maisha yako, siku 100 za kwanza huwa ni siku ngumu sana kwenye mabadiliko hayo.

Maisha yatakuwa magumu sana kwenye siku hizo 100 za kwanza, utashawishika sana kurudi kwenye kile ulichozoea, utaona hakuna manufaa kwenye mabadiliko hayo.

Na hapo ndipo wanaofanikiwa na wanaoshindwa wanapotengana. Wanaofanikiwa wanaendelea kuyasukuma mabadiliko licha ya ugumu wanaopitia. Wanaoshindwa wanayaacha mabadiliko kutokana na ugumu wanaopitia.

Tafiti mbalimbali za kitabia zimekuwa zinakuja na namba tofauti kwenye muda ambao mtu anahitaji katika kutengeneza tabia mpya. Kuna tafiti zinaonesha unahitaji siku 21, nyingine siku 66, nyingine siku 90. Lakini wewe jipe namba ya siku 100, ni namba salama na ukiweza kuivuka, tabia mpya inakuwa imejijenga.

Hivyo rafiki, tabia yoyote unayotaka kuijenga au kuivunja, mabadiliko yoyote unayotaka kufanya kwenye maisha yako, jipe siku 100 za kujitoa kweli na kutokukata tamaa hata iweje.

Cha kufanya, jiambie utaishi hivyo kwa siku 100 tu, na kama siku hizo zitaisha na bado ukaona mabadiliko hayo ni magumu kwako, basi unaweza kurudi kwenye maisha ya awali. Ila huwezi kufanya hivyo kabla siku 100 hazijaisha. Kisha jisukume kufanya kwa siku 100. Utashangaa sana siku hizo 100 zinapoisha hufikirii kurudi tena nyuma, kwa sababu unakuwa umeshazoea kabisa na huoni tena ugumu.

Je ni mabadiliko gani umekuwa unafanya kwenye maisha yako lakini hayadumu? Fanya mabadiliko hayo sasa na jiambie una siku 100 za kuishi kwenye mabadiliko hayo na usikatishe kabla siku 100 hazijaisha.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha