Fikiria wewe ni kiwete, halafu unaamua kuingia kwenye shindano la kupigana mateke.

Wenzako wana miguu miwili na wako vizuri, wewe una mguu mmoja ambao ni mzima, mwingine haupo kabisa au una udhaifu.

Kinachotokea ni unaishia kutoa faida kwa kila mtu, maana kila mtu ataweza kukupiga wewe mateke, lakini haitakuwa rahisi kwako kuwapiga mateke.

Ukiwa kiwete lakini ukajilazimisha kuingia kwenye shindano la kupigana mateke, unaishia kushindwa vibaya na wengine kunufaika kupitia wewe.

one legged man.jpg

Swali ni wewe ni kiwete kwenye nini na shindano la mateke ni nini?

Najua unajua huu ni mfano, lakini unahusisha maisha yako na safari yako ya kuelelea kwenye mafanikio. Na unataka kujua ukiwete wako uko wapi na shindano lako la mateke ni lipi.

Kabla hatujaingia ndani kwenye hili, nikushirikishe kauli ya bilionea mwekezaji Charlie Munger ambaye amewahi kunukuliwa akisema; “If you’re going to live a long time, you have to keep learning. What you formerly knew is never enough. So if you don’t learn to constantly revise your earlier conclusions and get betters ones…you’re like a one-legged man in an ass-kicking contest.”

Akimaanisha; Kama utaishi kwa muda mrefu, unapaswa kuendelea kujifunza. Ulichokuwa unajua huko nyuma kamwe hakikutoshi. Hivyo kama hutajifunza kuendelea kuboresha kile unachojua na kikawa bora zaidi, huna tofauti na mtu mwenye mguu mmoja anayeshiriki shindano la kupigana mateke.

Rafiki, naamini unaipata picha hapo, kwamba unapokuwa na madhaifu, halafu unakwenda kushindana na watu ambao wana uimara kwenye madhaifu yako, unaishia kuwa manufaa kwao na kushindwa vibaya.

Kiwete chako kiko wapi?

Kiwete chako kipo kwenye tabia ya kutokupenda kujifunza mara kwa mara.

Kama hujifunzi vitu vipya kila siku, unabaki nyuma.

Kama tangu umehitimu masomo yako hujawahi kujifunza vitu vipya, umechagua wewe mwenyewe kuwa kiwete.

Kama unajiambia hupendi au huna muda wa kusoma vitabu, umekubali ukiwete na utaendelea kuwa hivyo.

Shindano la mateke ni nini?

Shindano la mateke ni shughuli yoyote inayohusisha akili kufanya.

Kazi ya aina yoyote ile ni shindano la mateke, kwa sababu inahitaji akili na ubunifu kuifanya.

Biashara ndiyo shindano kuu la mateke, kwa sababu biashara zina ushindani mkali sana, na yule mwenye kuijua biashara yake vizuri, akatoa thamani kubwa, ndiye anayeshinda kwenye biashara.

Maisha kwa ujumla ni shindano la mateke, tunakutana na magumu na changamoto nyingi kwenye maisha ambazo zinahitaji akili na ubunifu katika kuzitatua.

SOMA; MUHIMU; Bidhaa Za Mafunzo, Ukocha Na Ushauri Za Kocha Dr. Makirita Amani.

Unavyoshiriki shindano la mateke huku unajijua ni kiwete.

Sasa fikiria tangu umehitimu masomo yako na kupata kazi, hujawahi kujifunza kitu kipya na kikubwa kuhusu taaluma yako au kazi unayofanya. Halafu unaona watu wengine wanakupita tu, wanakuja watu wapya na kupewa vyeo ila wewe umebaki pale pale. Hapo jua upo kwenye shindano la mateke na wewe ni kiwete, wenzako watanufaika na wewe utaumia.

Umeingia kwenye biashara kwa sababu ulisikia wengine wakisema inalipa sana. Tangu umeingia kwenye biashara hiyo hujawahi kusoma au kujifunza chochote kuhusu biashara kwa ujumla, masoko, mauzo, saikolojia ya wateja, kudhibiti mzunguko wa fedha na mengine kama hayo. Lakini kila siku unalalamika biashara ni ngumu. Wakati kwako biashara ni ngumu, kuna wenzako unaona wanapiga hatua kwenye biashara hiyo hiyo bila hata ya kutumia nguvu kubwa. Unaweza kujiambia wana bahati au namna fulani, lakini usichojua ni kwamba unashiriki kwenye shindano la kupigana mateke wakati wewe ni kiwete, huwezi kushinda.

Upo kwenye madeni, kipato chako hakitoshelezi, kila kikitoka unalipa madeni na matumizi, kinaisha kabla hata matumizi hayajakamilika, hivyo unarudi tena kukopa. Hivyo ndivyo miaka yako inaenda, unapokea fedha, unalipa madeni halafu unaanza tena kukopa. Miaka inaenda na hakuna hatua unayopiga, unaanza kujiambia kuna chuma ulete, au anayekulipa kuna namna anakufanyia ili usipate uhuru uendelee kumtegemea. Rafiki, fungua macho, wewe ni kiwete na unashiriki kwenye shindano la kupigana mateke. Hujawahi kujifunza chochote kuhusu fedha, wewe unajua unapata fedha na kutumia basi. Huwezi kushinda mchezo huo wa fedha kwa kiwete hicho ulichonacho.

Upo kwenye ndoa au mahusiano lakini kila siku hakuna amani, likiisha moja linakuja jingine. Hujawahi kukaa chini na kujiambia unataka kujifunza kuhusu mahusiano, saikolojia ya jinsia tofauti kwenye mahusiano, asili ya binadamu na tabia na mambo mengine. Unafikiri mahusiano yako yatakuwa mazuri yenyewe tu, kitu ambacho hakitokei. Ujue hapo unashiriki kwenye shindano la mateke wakati wewe ni kilema.

Rafiki, hii ni mifano michache, lakini kwenye maeneo mengi ya maisha yako una hali kama hii. Angalia eneo lolote ambalo linakupa changamoto kwenye maisha yako, na utaona wazi kwamba hujawahi kuweka juhudi za makusudi kuwa bora kwenye eneo hilo. Na hapo ndiyo utaona wazi kwamba umechagua kushiriki shindano la mateke wakati unajijua ni kiwete.

Ponya kiwete chako kwanza.

Baada ya kujua kiwete chako kiko wapi, usikazane kuendelea na shindano la mateke kwa mategemeo kwamba mambo yatakuwa bora yenyewe.

Badala yake unapaswa kuponya kiwete chako haraka ili usiendelee kushindwa kwenye shindani ulilopo.

Njia pekee ya kuponya kiwete chako ni kujifunza vitu vipya kila siku na kukazana kuwa bora leo kuliko ulivyokuwa jana.

Njia za kujifunza zipo nyingi, hapa nakutajia zile za uhakika, ambazo unapaswa kuzitumia kila siku ili kuwa bora.

Moja; soma vitabu. Kwenye kila eneo unalotaka kuwa bora, chagua vitabu 10 bora kwenye eneo hilo na visome kwa undani kwa namna ya kuvielewa. Vitabu hivi unapaswa kuvirudia mara kwa mara, kwa sababu ndiyo vinakuwa mwongozo mkuu kwenye maisha yako. Kila unaposoma kitabu, kuna kitu unajifunza, sasa unapokitumia, unakuwa bora zaidi.

Mbili; shiriki kozi au mafunzo mbalimbali. Tafuta kozi au mafunzo yanayotolewa kwenye lile eneo ambalo una changamoto kisha shiriki. Kozi na mafunzo ya aina hii huwa yana manufaa zaidi ya usomaji kwa sababu unakuwa na mtu mwingine anayeelekeza na pia unashirikiana na wengine kwenye kujifunza. Unaposhirikiana na wengine, unajifunza mengi na kwa haraka.

Tatu; kuwa na kocha na menta. Kocha ni mtu anayekupa msukumo wa wewe kufanya kile ambacho unajua unapaswa kufanya, ila ukiwa mwenyewe huwezi kufanya. Ukiwa mwenyewe ni rahisi kuahirisha, lakini ukiwa na kocha hakukubalii kirahisi na pia anakupa mwongozo wa kufanya kile unachopaswa kufanya ili upate matokeo mazuri. Menta ni mtu ambaye tayari ameshafika kule ambapo wewe unataka kufika, hivyo anakushika mkono ili na wewe ufike. Menta atakuambia vitu gani vya kufanya na vipi vya kuepuka kufanya ili ufike kule unakotaka kufika. Hawa ni watu wawili muhimu sana unaopaswa kuwa nao kama unataka kushinda shindano lolote ulilopo sasa.

SOMA; Karibu Kwenye Channel Ya Soma Vitabu Tanzania Upate Vitabu Na Chambuzi Za Vitabu.

Shiriki shindano huku ukiendelea kujiboresha zaidi.

Rafiki, kujifunza na kujiboresha hakuna mwisho. Siku utakayojiambia umefika mwisho au kilele, siku utakayojiambia umeshajua kila kitu, ndiyo siku unayoanza kuanguka.

Hivyo mara zote kaa kwenye mazingira yanayokuhamasisha kujifunza na kuwa bora zaidi.

Kila unapokutana na ugumu au changamoto, kabla hujakimbilia kuweka nguvu na mazoea, rudi kwanza kwenye kujifunza, ni wapi unakosea mpaka unakaribisha magumu na changamoto hizo.

Ukiyaendea maisha kwa mtazamo huu, utaweza kufanya makubwa sana na hakuna lolote litakalokushinda.

Utashiriki shindano la kupigana mateke huku ukiwa na miguu yako miwili imara, lakini pia wengi watakaokuwa wanashindana na wewe watakuwa ni viwete hivyo utakuwa kwenye nafasi nzuri ya kushinda.

Swali la kujipa jibu na kuchukua hatua.

Rafiki, katika kumaliza makala hii ya leo, naomba ujiulize swali hili, kisha ujipe jibu na kuchukua hatua ili maisha yako yasiendelee kubaki pale yalipo sasa.

Swali; ni eneo gani kwenye maisha yangu ni kiwete lakini nashindana kwenye mateke? Jipe jibu, ponya kiwete chako na pata mafanikio makubwa.

Rafiki, kama ungependa kuendelea kupokea makala na mafunzo mengine mazuri kwenye email yako, fungua hapa na ujaze fomu; www.bit.ly/amkaemail

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.

Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania

one legged man.jpg