Sisi binadamu tuko vizuri na haraka sana kwenye kuhukumu.
Na hukumu zetu za haraka ni NZURI au MBAYA.
Kwa kila jambo linalotokea, kwa haraka sana tunaliweka kwenye kundi moja kati ya makundi hayo mawili, NZURI au MBAYA.
Kama kitu kinaendana na tunavyotaka tunasema ni kizuri, kama hakiendi tunavyotaka tunasema ni kibaya.
Lakini ukiyaangalia maisha yako, utaona mara nyingi hukumu hizo siyo sahihi.
Yale uliyojiambia kwa haraka ni mazuri yanakuja kuonekana ni mabaya, na yale uliyojiambia ni mabaya, yanakuja kuonekana ni mazuri.
Mfano mzuri ni magumu ambayo kila mmoja huwa anapitia kwenye maisha yake.
Wakati wa magumu hayo, kila mtu huona ni mabaya na kutamani asingepitia hali hiyo.
Lakini baada ya kuvuka magumu hayo, ndiyo mtu unagundua kwamba magumu hayo yamekufanya kukua na kuwa imara kuliko ulivyokuwa kabla ya magumu hayo. Japo hukuyapenda, yamekuwa msaada mkubwa kwako.
Pia kuna wakati unakutana na hali fulani yenye manufaa kwako, unajiambia umepata kitu kizuri, baadaye unakuja kugundua kwamba kitu hicho kimekuharibia kuliko kilivyokunufaisha.
Tunachojifunza hapa ni kuwa na subira kabla hatujakimbilia kwenye kuhukumu kama kitu ni kizuri au kibaya. Jukumu letu ni kukabiliana na maisha kama yanavyokuja, kufanya kile tulichopanga kufanya na kuchukua hatua sahihi kulingana na hali tunayopitia.
Uzuri au ubaya wa kitu tuuachie muda na utasema wenyewe. Muda ni mwalimu mzuri, muda ni tiba, muda ni jawabu. Kipe kitu chochote muda na utaweza kukielewa kwa kina na kuchukua hatua sahihi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Ni kweli kocha, kusubiri kunakufanya ujue ukweli kama ulivyo, kuliko kukimbilia kuhukumu mapema. Asante sana.
LikeLike