”Be attentive to what you do; never consider anything unworthy of your attention.” — CONFUCIUS

Chochote kile unachoamua kufanya, una machaguo mawili,
Unaweza kuchagua kukifanya vizuri sana, kwa viwango vya juu sana na upekee mkubwa.
Au unaweza kuchagua kutokukifanya kabisa.
Chaguo jingine tofauti na hayo mawili ni kupoteza muda wako, maisha yako na kuharibu sifa yako.
Usikubali kufanya kitu chochote kwa ukawaida au vibaya.
Kumbuka kila kitu unachoruhusu mikono yako ishike, jua unaacha alama yako pale, jua kinakutangaza.
Sasa kama vitu vinavyokutangaza wewe ni vile vilivyofanywa hovyo, haishangazi kwa nini hufanikiwi.
Kama kila kinachokutangaza kimefanywa kwa viwango vya juu, hakuna kinachoweza kukuzuia kufanikiwa.

Kuna tabia ya watu kukubali kufanys kitu ambacho hawakipendi au hawakijali, ili tu kupata fedha au kuwaridhisha wengine.
Wewe usiwe mmoja wa watu hao,
Kipaumbele chako cha kwanza kinapaswa kuwa kufanya kitu vizuri, kwa upekee ambao haujawahi kuonekana.
Na kama huwezi kufanya vizuri na kwa upekee huo, basi acha, usifanye kitu hicho.
Sifa yako unayoharibu ina madhara makubwa kuliko fedha unayokosa au wengine unaowaudhi.

Hii inakwenda kwa wale wanaofanya kazi ambazo hawazipendi, ila wanahitaji kuingiza kipato.
Kwa wale wanaofanya biashara ambazo hawazijali ila zinawaingizia faida.
Kwa wale wanaojikuta kwenye mahusiano na ushirikiano na watu wasiowajali, lakini wanaogopa kuwaangusha.
Usiwe mmoja kati ya hao,
Hata kama hupendi kile unachofanya, jilazimishe kukifanya kwa ubora wa hali ya juu.
Na kama huwezi kujilazimisha kukifanya hivyo, achana nacho, kuna mengi ya kufanya.

Asili inakulipa sawasawa na unavyofanya.
Fanya hovyo na utalipwa hovyo, fanya kwa ubora na utalipwa kwa ubora.
Huwezi kuidanganya asili, hivyo toa kwa namna unavyotaka kupokea.
Siku ya leo ikawe ya kufanya mambo kwa ubora, kuweka umakini wako wote kwenye kile unachofanya kama vile ndiyo kitu pekee kwenye maisha yako, kwa sababu ndiyo kitu pekee umechagua kufanya.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma

Wako rafiki katika safari ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.t.me/somavitabutanzania