Ipo kauli kwamba safari ya maili elfu inaanza na hatua moja. Siyo kwamba ukishapiga hatua moja safari imemalizika, bali msimamo wako kwenye kupiga hatua moja kila wakati ndiyo utakaokamilisha safari hiyo.

Hakuna asiyeweza kupiga hatua moja, lakini mbona ni wachache wanaofika mwisho wa safari?

Kinachowatofautisha wengi wanaopiga hatua moja na wachache sana wanaofika mwisho wa safari ni msimamo.

Msimamo wa kuendelea kupiga hatua moja bila kuchoka, kuendelea kupiga hatua moja hata pale mambo yanapokuwa magumu na kuwa na kila sababu ya kuacha safari hiyo.

Hivyo ndivyo ilivyo kwenye maisha yetu ya kila siku, msimamo kwenye hatua tunazochukua ndiyo unaoleta mafanikio.

Tukiangalia kwenye biashara, wengi wanaanza biashara, lakini wachache sana ndiyo wanaofanikiwa, wengi wanaishia kuwa kawaida au hata kufunga biashara zao. Lakini wale wachache ambao wanaendelea kupiga hatua, kujifunza na kujaribu vitu vipya, kukazana kuwa bora kila wakati, ndiyo wanaofanikiwa kwenye biashara zao.

Tukienda kwenye kazi, kila mtu anapokuwa anaanza kazi yake anakuwa na mipango mikubwa ya ukuaji na kufika ngazi za juu. Pale mwanzoni mtu anaanza mipango hiyo ya ukuaji, lakini katikati anakutana na vikwazo na changamoto mbalimbali. Hapa wengi huchagua kuwa wa kawaida na kuachana na mipango ya ukuaji, na mambo yanaishia hapo. Wachache wanaoendelea na mpango licha ya kukutana na magumu, ndiyo wanaofika ngazi za juu.

Angalia kwenye asili, tone moja la maji linalianguka kwenye jiwe si chochote, lakini tone hili linapojirudia kila wakati bila kuacha, mwamba mgumu unavunjwa.

Msimamo ndiyo mpango mzima rafiki yangu, ukishachagua nini unachotaka, na kujua nini unapaswa kufanya ili kufika unakotaka, kinachobaki ni wewe kufanya kama ulivyopanga, bila kuacha, inyeshe mvua, liwake jua, wewe utafanya.

Kwa sababu msimamo ndiyo kitu pekee kitakachokufikisha unakotaka na kukupa unachotaka. Bila msimamo, hata uwe na nini, huwezi kufanikiwa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha