Utakapoanza kufanya kazi yako, kwa viwango ambavyo umejiwekea wewe mwenyewe ili uweze kufikia mafanikio makubwa, utawakaribisha wengi ambao watakuja kwako na mambo mbalimbali.

Wapo ambao watakukatisha tamaa kwamba kazi unayoifanya haiwezekani, wakikutaka ufanye tu kawaida, kwa sababu hakuna anayeweza kuelewa hicho unachofanya.

Kuna ambao wataenda mbali zaidi na kuhakikisha wanakukwamisha katika kufanya kazi hiyo.

Kuna ambao watakudharau kwa namna unavyofanya, wakiamini huwezi kufanya makubwa.

Kuna ambao watakupuuza, hawatajihusisha na wewe kabisa.

Kuna ambao watakupa moyo kwamba unaweza na kukutaka uendelee.

Sisi ni binadamu, na moja ya udhaifu wetu ni kujali sana jinsi gani wengine wanatuchukulia kwenye kile tunachofanya.

Hivyo ni rahisi sana kukata tamaa pale watu wanapokukatisha tamaa, au kutaka kuwaonesha kwamba hawapo sahihi.

Lakini hayo yote siyo muhimu kwako wala kwao, ukichukua hatua hizo, unakuwa umepoteza muda wako na kuwapa watu hao sababu zaidi za kukushambulia.

Kilicho muhimu zaidi kwako ni kuifanya kazi yako, kwa viwango ambavyo umechagua bila ya kutetereka wala kuangalia wengine wanakuchukuliaje.

Mwisho wa siku, kitakachokuinua wewe ni kazi yako na siyo majibu yako kwa wale wanaokupinga. Hivyo weka nguvu na muda wako kwenye kazi yako, hiyo ndiyo muhimu kwako na inayostahili muda mchache na nguvu ulizonazo.

Weka kazi sasa na kuna wakati utafika hutahitaji hata kujitetea, maana kazi yako itaeleza yenyewe.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha