Umewahi kujifunza hili kuhusu imani za kishirikina ambazo watu wanazo, huwa zinaendana na mazingira.
Kwa mfano, watu walio maeneo ya kigoma, uchawi wao utahusishwa zaidi na kutumiana radi, kwa sababu maeneo hayo huwa yanapata radi mara kwa mara.
Watu waliopo maeneo ya pwani, utasikia wanaambiana mtu kalogewa busha, kwa sababu mazingira ya pwani yanachochea sana ugonjwa wa mabusha.
Angalia hata barabarani, sehemu zenye kona kali au mlima mkali, ambapo kuna hatari kubwa ya kupata ajali, ndiyo maeneo utasikia yanasifika kwamba kuna nguvu za giza ambazo zinasababisha ajali, lakini hutasikia hilo sehemu ambapo barabara imenyooka na ni tambarare.
Kadhalika, watu waliopo maeneo yenye wanyama wakali, utasikia wakiambiana mtu katumiwa mnyama fulani, kwa sababu wanyama hao wanapatikana kwa urahisi.
Sasa tukiacha upande huo wa uchawi na ushirikina, ambazo ni imani tu watu wamejijengea, kuna kitu kikubwa sana kuhusu mafanikio cha kujifunza hapa.
Kwamba unahitaji kuwa kwenye eneo sahihi kama unataka kupata kile unachotaka kupata.
Kama unataka kutumia radi kwa manufaa yako, lazima uwe eneo ambalo kuna uwezekano mkubwa wa kupata radi.
Kama unataka kukutana na watu sahihi kwako, lazima kwanza uwe kwenye eneo ambalo watu hao sahihi wanapatikana. Utakuwa unashangaza kama unajiambia unataka upate watu watakaokusukuma kufanikiwa halafu kutwa nzima unashinda na watu wasio na nyuma wala mbele.
Kama unataka kuanzisha biashara mpya, angalia mahitaji ambayo tayari watu wanayo na kusha kuwapatia kwa namna ambayo ni bora kuliko wanavyoyapata kwa sasa. Kuanza biashara ambayo haina wateja kabisa au inabidi utengeneze uhitaji, ni kujipa kazi mara mbili.
Na usiogope ushindani, kwamba ukiwa kwenye eneo ambalo kuna uwezekano mkubwa wa kitu kupatikana, basi wengine wengi nao watakuwa hapo. Hiyo ni nzuri kwako, kwa sababu unapata nafasi ya kufanya kwa ubora wa hali ya juu na hivyo kuwavuta wenye uhitaji kuja kwako.
Ushindani kwenye biashara ni kiashiria kwamba biashara hiyo ina uhitaji, hivyo ukiweza kutoa kwa ubora kuliko wengine, unakuwa kwenye nafasi nzuri ya kuwa na wateja wengi. Lakini kama biashara haina ushindani kabisa, ni labda wewe una akili sana kuliko wengine wote, au biashara hiyo haina uhitaji. Namba moja ni nadra sana, namba mbili ndiyo sababu mara nyingi, hivyo kuwa makini.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Hakika kila mara kila wakati lazima ujijue upo wapi na akina nani,ndege wanaofanana huruka pamoja,ndio maana kulaumu na kulalamika ni sumu kubwa katika kuyatafuta na kuyafikia mafanikio yako.
LikeLike
Hahaa ni kweli kabisa kocha, Dhana hii ni ya kutafakarisha sana.asante
LikeLike
Karibu Kalenga
LikeLike